Klabu ya Simba imesema ina shida na fedha, lakini haiko tayari kupokea kwa mafungu fedha za mauzo ya mshambuliaji wake wa zamani wa kimataifa, Emmanuel Okwi waliompiga bei Klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia.
Okwi, raia wa Uganda aliyecheza kwa mafanikio Msimbazi, kwa sasa anacheza soka la kulipwa nchini Denmark.
Simba inastahili kupokea dola 300,000 (zaidi ya Sh. milioni 600), lakini Etoile du Sahel pamoja na kukubali kulipa fedha hizo, imesema inaweza kufanya hivyo kwa kulipa kwa awamu na siyo zote mara moja.
Novemba 20 mwaka jana, Kamati ya Nidhamu za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Ulimwenguni (Fifa), iliiamuru klabu hiyo ya Tunisia kuilipa mara moja Simba kiasi hicho cha fedha na riba ya asilimia mbili kwa kila mwaka tangu mchezaji huyo alipouzwa.
Msemaji wa Simba, Haji Manara alisema jana kuwa hawatakuwa tayari kupokea fedha hizo kwa mafungu na badala yake wanataka walipwe mara moja.
"Wametuomba wafanye malipo kwa awamu mbili, sisi tumeona hiyo siyo sahihi, tunataka kulipwa fedha zote mara moja kwa sababu deni liko muda mrefu sasa," alisema manara.
"Kamati ya Nidhamu ya Fifa iliagiza fedha hizo kulipwa mara moja, na sisi tunasisitiza tulipwe fedha yote mara na haraka kama ilivyoagizwa."
Katika kuhakikisha Simba inalipwa fedha zake, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limekuwa likiwasiliana na Fifa na mamlaka ya usimamizi wa soka Tunisia (FTF).
Iwapo klabu hiyo itashindwa kulipa fedha hizo kwa muda uliopangwa, itakumbana na hatari ya kushushwa daraja au kupokwa alama kwenye ligi wanayoshiriki.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment