Monday, January 4, 2016

TRL NA RAHCO WAAGIZWA KUKARABATI RELI NDANI YA SIKU 3


Waziri wa Ujenzi , Uchukuzi na Mawasiliano Mhe Profesa Makame Mbarawa  amezitaka Menejimenti za  Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) na Kampuni Hodhi ya Reli Rahco kufanya kila linalowezekana kuondoa athari za mafuriko ya mvua zilizoikumba eneo la stesheni za  Kilosa na Mzaganza ambako reli imekatika.
Mhe Waziri ameutaka uongozi huo kutumia ujuzi wao wote na wahandisi na mafundi wake  kurejesha tuta la reli katika hali ya kawaida ili huduma ziweze kuanza ndani ya siku 3 zijazo.
Aidha aliwataka Viongozi na wananchi wa eneo hilo la Mzaganza na Kidete kuzingatia kilimo chenye tija ambacho kitazuia mmong’onyoko wa ardhi ambao unafanya mafuriko yatokee killa mwaka. Eneo la zaidi ya kilomita 2 la tuta la reli  limekumbwa na mmong’onyoka (wash away) na hivyo kulazimisha kusitisha huduma za reli tokea Januari 1, 2016.
Waziri Mbarawa akifuatana na Maafisa Waandamizi wa Wizara yake na wale kutoka TRL na Rahco alifika eneo hilo asubuhi jana Januari 3 , 29016 kukagua uharibifu huo unaosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi lakini pia na shughuliza kibinadamu  ambazo hazizingatia kilimo cha kisasa.
Wakati taarifa hii inaandaliwa uongozi wa Rahco tayari umeshaanza kufanya mchakato wa ununuzi wa vifaa maalum vinavyohitajiwa na TRL ili kuikamilisha kazi ya ukarabati  wa eneo hilo kama ilivyoagizwa na Mheshimiwa Profesa Mbarawa.
Akizingumza na waandishi wa Habari aliofuatana nao Waziri Mbarawa alisema uharibifu huo wa eneo la Kilosa , Kidete, Godegode na Gulwe muda wake  umeifika upatiwe ufumbuzi wa kudumu. Ameahidi muda sio mrefu  kuitisha  kikao cha wataalamu ili kutafakari kwa kina kadhia hiyo ambayo sasa inaonesha kuwa kaburi la mapato ya Serikali linapatiwa ufumbuzi wa kudumu. “ Haiwezekani vichwa vyote hivi Wizarani , Rahco, TRL, Sumatra vishindwe kuja na jibu” Alisisitiza Waziri.
Wakati huo huo Uongozi wa TRL umewaomba radhi wateja wake na wananchi kwa ujumla kwa usumbufu wa kukosekana huduma muhimu wanayoitegemea. Aidha umewahakikishia kuwa TRL ikiishirikiana na Serikali na tasisi zake husika inafanya jitihada za dhati  kurekibisha eneo lililoathiriwa na mafuriko na kwamba wawe na subira na muda sio mrefu huduma za reli zitarejea kama kawaida.

Imetolewa na Afisi ya Uhusiano kwa niaba ya
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TRL Mhandisi Elias Mshana.
Dar es Salaam,
Januari 04, 2016

No comments: