ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, January 26, 2016

Twiga albino apatikana Tanzania

Twiga anayejulikana kitaalamu kwa jina la ‘Omo’ likimaanishwa twiga mweupe au Albino (Kushoto) akiwa mbugani Tarangire, Picha ya kulia inamwonyesha twiga huyo akiwa na twiga wenzake wa kawaida
Mwanasayansi Dk Derek Lee amegundua twiga albino kwenye hifadhi ya mbuga ya Tarangire iliyopo katika Mkoa wa Arusha nchini Tanzania.


Mtafiti huyo Dk Derek Lee, alipiga picha mbalimbali zikiwa zinamwonyesha mnyama huyo akiwa katika kundi kubwa la twiga, huku akiwa na rangi ya kipekee ikilinganishwa na twiga wengine duniani.

Dk Lee, alimgundua twiga huyo wakati akifanya utafiti kwenye mbuga hiyo na nyingine za wanyama za barani Afrika,

Taarifa iliyoripotiwa na shirika la habari nchini Uingereza kupitia gazeti la Dailymail zimeeleza kuwa, twiga huyo adimu kupatikana duniani iwapo atahifadhiwa atakuwa kivutio cha pekee katika mbuga hiyo.

Twiga huyo anayejulikana kitaalamu kwa jina la ‘Omo’ likimaanishwa twiga mweupe/mwenye ulemavu wa ngozi ‘albino’, alionekana akizunguka katika mbuga hiyo katikati ya twiga wengine. Dk Lee ambaye pia ni mtaalamu wa viumbe na mwanzilishi na mwanasayansi kutoka Wild Nature Instute, alimnasa twiga huyo katika kamera yake wakati akifanya uchunguzi huo kuhusu wanyama.

Lee (45) alisema: “Omo ni ‘leucistic’ hii inamaanisha seli zake nyingi katika ngozi hazina uwezo wa kutengeneza rangi, hivyo anakuwa ni albino, lakini hawi mweupe katika ngozi yake yote na wakati mwingine anakuwa na macho mekundu au ya bluu kama ilivyo kwa albino.

“Ni hali ya kimaumbile ‘Omo’ni aina pekee ya twiga ambaye anajulikana duniani na ndiye pekee aliyeonekana Afrika kwa takribani miaka mitatu sasa, pia tuligundua uwapo wa wanyama kadhaa wakiwamo nyati na mbuni albino katika mbuga ya Tarangire,” alisema

“Omo anaonekana kwa nadra sana na mara nyingi anapoonekana huwa pamoja katika kundi kubwa la twiga wengine ambao huwa hawaonyeshi kushangazwa na rangi aliyonayo.” “Kwa utafiti uliofanyika twiga huyo kwa sasa ana umri wa miezi 15, aliishi mwaka wake wa kwanza kwa kunusurika kuuawa na wanyama wakali kulingana na utofauti wake, kipindi ambacho ni cha hatari kwa twiga wadogo hasa kutokana na kushambuliwa zaidi na simba, chui na fisi ambao huwatafuna,” alisema.

Alisema uwezekano wa twiga huyo kukua kwa sasa ni mkubwa, lakini bado wanyama wakubwa wamekuwa wakimwinda na binadamu kwa ajili ya nyama za porini, na huenda rangi aliyonayo inaweza kumfanya yeye kuwindwa zaidi.

“Sisi na washirika wetu ambao wanafanya kazi katika mbuga mbalimbali na wanaopambana na ujangili tupo kwenye mazungumzo ili kumsaidia Omo huyu na wengine watakaopatikana kuhifadhiwa vizuri ili waishi kwa muda mrefu. Tunaimani kwamba wataishi miaka mingi na baadaye atazaa na kupata watoto watakaofanana na yeye na hivyo kuongeza vivutio vya twiga weupe duniani,” alisema Dk Derek.

Imetafsiriwa na Herieth Makwetta,wa Mwananchi kwa msaada wa mitandao mbalimbali ya kimataifa-
    

1 comment:

Anonymous said...

Kwa yeyote yule alieiwasilisha hii makala kwa wasomaji wa kiswahili anatakiwa kuwa makini ili kuepuka upotoshaji wa makala halisi. Huyo twiga mweupe au rare an extremely white giraffe sio albino bali isipokuwa ana hali ya maumbile ndani ya mwili wake inayojulikana kama "leucism" na nakuwa na hiyo hali ya leucism ndiko kulikompelekea huyo twiga kukosa rangi yake ya kawaida. Au kama wataalam walivyosema ya kwamba, her body surface cells are not capable of making pigment, but she is not an albino. Na hasa inawezekana ya kwamba kingo za macho yake bado zimebakia na rangi yake ya kawaida kwani kama tunavyojua ili uthibitike kuwa albino basi ngozi yote ya macho pamoja na nyusi hata kope zitakuwa zitakuwa zimefanana na ngozi ya mwili. Na vile vile hilo jina la Omo alilopewa huyo twiga sio la kitaalam bali waongozaji wa watalii nyumbani wamempa jina hilo kutokana na weupe wake wakimfananisha na sabuni ya Omo. Kumwita albino labda kutaka kuwapa kazi wachawi kumwangia usiku na mchana kuvipata viungo vyake, kazi ipo.