Mbali na TBC ambayo kutokana sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), inayolazimisha kampuni za ving’amuzi kurusha matangazo ya televisheni hiyo bure, hali inayofanya ionekane eneo kubwa la nchi, wabunge hao walisema hata vituo binafsi vya televisheni vinavyorusha matangazo hayo moja kwa moja, zitazuiwa hivi karibuni.
Vituo vingine vya televisheni vinazorusha matangazo hayo moja kwa moja ni Azam na Star.
Jana, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisisitiza kwamba TBC haitoonyesha majadiliano ya moja kwa moja ya Bunge kuanzia mkutano huu wa pili wa Bunge la 11 na badala yake yatarekodiwa na kuonyeshwa usiku.
Juzi Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, alisema kipindi hicho kitaonyesha matukio muhimu yaliyojiri bungeni kwa saa moja licha ya kwamba kuanzia kukatishwa kwa maswali na majibu saa tano mpaka saa saba mchana kinapoisha kipindi cha asubuhi kabla ya kuingia tena saa 10:00 jioni mpaka saa 1:45 jioni ni takribani saa saba.
Baadhi ya wabunge wa upinzani waliozungumzia suala hilo, walisema serikali kusema inakatisha matangazo hayo kwa sababu ya kuongezeka kwa gharama na kufikia Sh. bilioni 4.2, hazina msingi.
Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT- Wazalendo), Zitto Kabwe, ambaye aliianzisha hoja hiyo, alisema tangu akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), amekuwa akilishauri shirika hilo namna ya kuongeza gharama lakini hakuna walichokifanya.
“Kila Waziri anayeingia ninamshauri. Kwa mfano, sasa hivi kuna ving’amuzi, tukisema kila mtu mwenye king’amuzi tumuwekee Sh. 500 kwa ajili ya kuisaidia TBC na yenyewe ijiendeshe kama shirika la umma bila matangazo, kwa mwaka watakuwa na zaidi ya Sh. bilioni 40.
“Sehemu kama Uingereza, kila mtu analipa fedha kwa ajili ya BBC (Shirika la Utangazaji la Uingereza) ndiyo maana wao hawana matangazo,” alisema Zitto.
Alisema hoja nyingine kama za watu kuacha kazi na kuhangaikia televisheni, hazina msingi kwa sababu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 18 inatoa uhuru kwa wananchi kupata habari.
“Kwa hiyo ukiangalia mambo yote hapa utaona kuna kitu kimejificha ndiyo maana mimi hata kwenye kamati ya uongozi nilisimamia msingi wa katiba,” alisema Zitto.
Kutokana na hali hiyo, Zitto alisema ni dhairi kwamba matokeo ya vipindi vya Bunge kurushwa moja kwa moja, viliigharimu CCM haswa kwenye kashfa ya Escrow iliyosababisha wapoteze viti vingi kwenye serikali za mitaa.
Katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Desemba 14, 2014 CCM ilikiri kuporomoka kwa asilimia 12 kwenye uchaguzi huo.
Mbunge wa Simanjiro, James ole Millya, alisema serikali inataka kujigeuzi kuwa ya kidikteta baada ya kuona athari ilizopata kwenye Bunge la 10 kwa wabunge kuiangusha serikali mara kadhaa.
“Kwenye matangazo ya moja kwa moja wananchi wanaona kila kitu. Huko tunakokwenda watasitisha mambo mengi tu ili kinachojadiliwa bungeni kisijulikane. Sote tunajua walichoambulia baada ya kashfa ya Escrow kujadiliwa bungeni huku wananchi kwa ukaribu sana wakiwa wanafuatilia mjadala ule,” alisema.
Alisema serikali kubana vyombo vya habari na kuwanyima wananchi haki ya kupata habari, haitakuwa njia nzuri ndiyo maana wao wanahangaika kuonyesha hawakubaliani na njia hiyo ya serikali kuficha udhaifu wao.
Kwa upande wa Mbunge wa Malindi, Ali Saleh Ali, alisema serikali ilijua suala la Zanzibar litatikisa kwenye Bunge hili ndiyo maana ikapanga mapema kulidhibiti Bunge.
“Serikali wanapata taarifa mapema ndiyo maana hata leo kuanzia asubuhi umeona askari wamejaa hapa kwa sababu walijua tutatoka wakadhani labda kutakuwa na fujo. Vivyo hivyo walijua kuwa tutasema ukweli wa suala la Zanzibar hapa na hali yake ya kisiasa ndiyo maana wameamua kukata matangazo ili wananchi wasione,” alisema.
Alisema kauli ya Nape ni utekelezaji wa matamanio yake ya tangu mwaka 2013 na kwamba aliona serikali na chama chake kinabanwa kutokana na Bunge kuonekana moja kwa moja.
“Februari 25, 2013, aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook kuwa ni vyema utaratibu wa kurusha mikutano ya Bunge moja kwa moja ukasitishwa,” alisema Saleh.
Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya, alisema serikali inaendeleza mpango wake wa kuhakikisha hakuna hata chombo kimoja kinachorusha moja kwa moja matangazo hayo ndiyo maana imeanza na TBC.
“Eti wanasema watu hawafanyi kazi wanaangalia TV, kuna kazi gani walizowapa? Hebu wawape kazi uone kama hawatafanya,” alisema Bulaya.
WABUNGE CCM WALONGA
Mbunge wa Jimbo la Donge, Sadifa Khamis Juma, aliiambia Nipashe kwamba hoja iliyotolewa na serikali ililenga ilijikita kwenye msingi wa gharama ambazo shirika limekumbwa nazo.
“Unajua siasa za bara ni tofauti na za Zanzibar. Kule ili uwe maarufu inategemea ni jinsi gani unatoa huduma lakini bara wengi wanakuwa maarufu kwa sababu ya vyombo vya habari.
“Yote hayo si mabaya, lakini kama gharama imekuwa kubwa ni bora au zinatakiwa kupelekwa kwingine si vibaya kwa sababu wananchi kupata huduma ni muhimu kuliko umaarufu kwa sababu hata mimi umaarufu wangu umechangiwa na vyombo vya habari,” alisema Sadifa.
Naye Mbunge wa Shinyanga Mjini, Stephen Masele, alisema kwa sababu hoja iliyowasilishwa na waziri ilijikita kwenye gharama, ni vyema wapinzani wangekaa ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria waangalie namna ya kupata fedha za kugharamia matangazo hayo.
“Hili suala haliathiri wabunge wa upinzani tu, hata wa CCM pia. Kwa hiyo ni vyema wangekaa hapa ili tuone namna ya kupata fedha ya kugharimia TBC,” alisema.
NAPE ANENA
Usiku wa kuamkoa jana, Nape alifanya mkutano na waandishi wa habari na kueleza kwamba wapinzani hawana sababu ya kuwa na wasiwasi kwa kuwa lengo la serikali si baya na wala haiwahofii hata kidogo.
“Mimi tena nawaambia waikosoe serikali iwezavyo ili ifanye kazi na si hao tu. Hata wa CCM wafanye hivyo. Hivi kweli kwa baraza lile (Baraza la Mawaziri) kuna mtu wa kumhofia?,” alihoji.
Alisema Wabunge wa CCM ni zaidi ya asilimia 70 ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria, hivyo ni wazi kwamba hawana jambo lolote la kuhofia.
Mbunge wa Bukoba Mjini (Chadema), Wilfred Lwakatare, alisema ni jambo lisiloingia akilini kusema kipindi cha Bunge kitakachorushwa kwa saa saba kinaweza kurushwa tena kwa saa moja na kutenda haki kwa watu wote.
“Wataenda kuchuja na kupitisha kile ambacho kinawapendezesha wao. kama wanasema watu hawafanyi kazi kwa sababu ya kuangalia televisheni kuanzia saa sita, basi wafute vipindi vyote kuanzia muda huo mpaka usiku,” alisema.
Alisema ni wazi kwamba wana wasiwasi ambao unachagizwa na nguvu ya wingi wa upinzani Bungeni.
KASHFA ZILIZOLITIKISA BUNGE
Kashfa kubwa iliyotikisa nchi katika kipindi cha awali cha Rais Kikwete ilikuwa ni Richmond ya mwaka 2008. Hii ilitokana na tatizo kubwa la uhaba wa umeme na serikali kulazimika kutafuta njia za dharura za kutatua tatizo hilo, zikiwamo zilizodaiwa kukiuka taratibu na sheria.
Baada ya kashfa hiyo kuchunguzwa na taarifa kutolewa bungeni, aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, alilazimika kujiuzulu baada ya kutakiwa ajipime kutokana na mazingira ya kashfa hiyo.
Wengine waliong’oka madarakani kwa kujiuzulu ni mawaziri wa Nishati na Madini kwa vipindi tofauti, Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha.
EPA
Mwaka 2008 iliibuka kashfa nyingine ya wizi wa mabilioni katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (Bot) ambapo vigogo kadhaa walitumia mbinu chafu kuchota zaidi ya Sh. bilioni 133 katika akaunti hiyo.
Katika wizi huo ulioitikisa nchi, wahusika walitajwa kutumia vivuli vya siasa kupitisha nyaraka bila kufanyiwa uhakiki. Ilimalizika kwa baadhi yao kufikishwa mahakamani na wengine ambao hawakutajwa kusamehewa na Rais Kikwete wakidaiwa kurejesha fedha walizoiba.
Katika kipindi hicho, yalipofanyika mabadiliko ndani ya Baraza la Mawaziri aliyekuwa Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, hakurudi huku Gavana wa BoT, Dk. Daudi Balalli akitimuliwa.
RIPOTI YA CAG 2012
Mwaka 2012, ilipotolewa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kujadiliwa bungeni, ulitokea mtikisiko mkubwa uliowang’oa mawaziri sita na manaibu wawili.
Waliong’olewa ni Dk. Cyril Chami (Viwanda na Biashara), Omary Nundu (Uchukuzi), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), Dk. Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), Mustafa Mkulo (Fedha) na William Ngeleja (Nishati na Madini) na manaibu waziri wawili; Athumani Mfutakamba (Uchukuzi) na Dk. Lucy Nkya (Afya na Ustawi wa Jamii).
OPERESHENI TOKOMEZA UJANGILI
Desemba 2013, Operesheni Tokomeza Ujangili (Otu), iliyoanzishwa na serikali nayo ilizua mtikisiko mwingine uliowang’oa madarakani mawaziri wanne ambao wizara zao zilielezwa kushindwa kusimamia vizuri utekelezaji wake.
Mawaziri waliong’olewa ni Dk. Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani ya Nchi), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Mathayo David Mathayo. Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), aliamua kujiuzulu kwa kile alichokiita kupima uzito wa matokeo ya operesheni hiyo.
AKAUNTI YA TEGETA ESCROW
Novemba 2014, ripoti 0ya PAC bungeni baada ya kuchambua ile ya CAG, iliyochunguza Akaunti ya Tegeta Escrow, ilisababisha mawaziri kung’olewa.
Mawaziri hao ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka.
Watumishi wengine walioguswa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema, Wenyeviti wa Kamati ya Nishati na Madini, Victor Mwambalaswa, Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, William Ngeleja na Kamati ya Bajeti, Andrew Chenge na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi.
CCM KUPOTEZA SERIKALI ZA MITAA
Katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika mwaka 2014, ingawa CCM iliingia kwenye uchaguzi huo ikiwa na faida ya kupita bila kupingwa katika vijiji 2,708, mitaa 644 na vitongoji 26,300, kupitia operesheni za Movement For Change (M4C), Vua Gamba Vaa Gwanda, Delete CCM na Mkachamchaka Kuelekea mwaka 2015 (V4C), upinzani ulinyakua viti vingi kuliko wakati mwingine wowote.
Hali hiyo inadaiwa kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na kashfa ya Escrow ambayo ilikuwa imepamba moto kipindi hicho. CCM ilikiri kuwa imeporomoka kwa asilimia 12 katika matokeo ya uchaguzi huo.
Chama hicho kilisema, kimeporomoka kutoka asilimia 96 mwaka 2009 hadi asilimia 84 mwaka 2014.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, aliwaambia waandishi wa habari kwamba asilimia 16 ya viti walivyopata wapinzani bado ni ndogo ikilinganishwa na miaka 22 tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini.
UPINZANI WAWATOLEA UVIVU POLISI
Baada ya juzi wabunge wa upinzani kutolewa nje ya ukumbi wa bunge kwa kichapo kutoka kwa polisi, jana walitoka tena kimya kimya na kuwatolea hasira zao askari waliokuwa nje ya jengo la kutokea ukumbini.
Tangu asubuhi jana, kabla ya kuanza kwa kikao cha Bunge, kulikuwa na idadi kubwa ya askari wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU), ambao walikuwa wamevalia mavazi maalumu ya kuzuia risasi.
Wabunge wa upinzani walipotoka nje ya ukumbi wa Bunge, baada ya kipindi cha maswali na majibu kwisha, askari hao walisogelea eneo la mlango wa kutoka kwenye ukumbi huo.
Kitendo hicho kiliwafanya baadhi ya wabunge hao kuanza kuwazomea polisi hao na kila mmoja kusema alilojisikia.
Baadhi ya maneno yaliyokuwa yakitamkwa dhidi ya polisi hao ni pamoja na “leo cheni hamuibi” , ‘ingieni tena leo Bungeni mkachangie na nyie” ‘leo hampati wa kumpiga”, “nendeni mkachangie ndani huko, kikao cha familia kinaendelea”, “leo hamuibi tumewa-time”, “Ingieni ndani kwenye kikao cha NEC kinaendelea huko” “Hebu waangalieni, watoto wa maskini mnakubali kutumiwa”.
Wengine walikuwa wanasema, “leo mmekuja wapya ili muibe vizuri, hamuambulii kitu, mtaendelea kutumiwa hivyo hivyo".
Naye Zuberi Kuchauka wa Liwale (CUF), anayedaiwa kupigwa na askari hao juzi na kuachwa na fulana, alikuwa akinyoosha juu kidole chake kilichokuwa kimefungwa kitambaa akidai aliumizwa na askari hao.
“Nawaambieni hii damu mliyoimwaga mtailipa. leo hamumpigi mtu hapa nawaambia,” alisema.
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bunge, Freeman Mbowe, alipozungumza na waandishi wa habari jana, alisema kuna wabunge wa upinzani wamelalamika kwamba wameibiwa vitu mbalimbali vikiwamo mikufu, simu na pochi.
Kwenye maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu, Mbowe alitaka serikali itoe tamko juu ya polisi kutumia nguvu kupita kiasi ikiwa ni pamoja na lilivyotumia kuwatoa wabunge juzi na hali ilivyo Zanzibar kwa sasa.
Baada ya swali hilo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema polisi kazi yake ni kuhakikisha amani na utulivu vinakuwapo wakati wote na kwamba watu wafanye kazi zao kama ilivyopangwa.
Alisema kuna mazingira yanayofanya polisi watumie nguvu na kwamba jambo la msingi ni kuwasaidia polisi kwa kutii sheria.
CHADEMA WATOA TAMKO
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimepinga hatua ya serikali ya kufuta urushaji moja kwa moja matangazo ya bunge kupitia TBC, na kwamba serikali ya awamu ya tano inaonyesha kuwa na hofu katika kujibu na kutekeleza shughuli zake kwa vitendo.
Chadema, kupitia Kaimu Ktibu Mkuu wake, Salum Mwalimu, jana iliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa hatua hiyo ni dalili ya uendeshaji nchi kidikteta na kuondoa haki ya Watanzania kufahamu kinachojadiliwa bungeni kupitia televisheni ya umma.
Aliomba kimelitaka Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), kutokubali kuminywa kwa vyombo vya habari katika kutekeleza majukumu yao.
Mwalimu alisema katiba ya nchi imevunjwa kwa kuwanyima haki Watanzania kupata, kutafuta habari na kuzisambaza kwa kuwa sababu zilizotolewa na serikali kwamba matangazo hayo ni gharama kubwa hazina msingi na wala ukweli wowote.
Mwalimu alisema madai ya Waziri wa Waziri Nape kwamba urushaji matangazo hayo ni ghali na yanafikia Sh. bilioni 4.2 kwa mwaka si ya kweli, kutokana na ukokotozi wa gharama hizo kutowekwa hadharani.
“Haiwezekani kuondoa matangazo ya bunge ambayo hufuatiliwa na Watanzania wengi, kwa walio vijijini hawawezi kuangalia marudio ya matangazo ya bunge saa nne hadi saa tano usiku kwani wanakuwa wamelala na gharama si kubwa kama ilivyoelezwa. Ziwekwe wazi Watanzania tutalipia,” alisema Mwalimu.
Alisema kwamba mapato ya serikali yaliyoongezeka katika awamu ya tano, yatumike katika kulipia matangazo hayo kwa kuwa suala hilo ni la kitaifa.
Alisema tangu mkutano wa pili wa Bunge la 11 uanze mjini Dodoma, uundwaji wa kamati za kudumu za bunge kwa ajili ya kuisimamia serikali, uteuzi wa wenyeviti na wajumbe wa kamati hizo haukuzingatia uzoefu wa watu.
Alisema uzoefu wa nchi zingine duniani ni kwamba matangazo ya bunge au shughuli za kitaifa, huwa na chaneli maalumu ambayo muda wote hurusha, tofauti na televisheni za watu binafsi ambazo haziwezi kumudu gharama hizo.
WADAU WAZUNGUMZA
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali la Sikika, Irenei Kiria, akizungumzia suala hilo la TBC kutorusha matangazo moja kwa moja, alisema kilicho nyuma ya pazia ni mkakati wa kupunguza uwajibikaji ndani ya Bunge hilo kwa visingizio tofauti.
Alisema vizuizi hivyo vilianza kuonekana tangu kwenye Kamati za Bunge kwa kutoweka wabunge wenye uwezo wa kuibua mambo mbalimbali, jambo ambalo linaonyesha wanakwepa kuwapo kwa uwajibikaji.
“Tunachoona kuna nguvu inaogopa mambo fulani ambayo hawataki yaonekane au kusikika kwa wananchi kupitia luninga ya serikali ambayo inaonekana sehemu kubwa nchini,” alisema.
Alisema kurusha kipindi cha Bunge si jukumu la serikali bali ni Bunge lingepaswa kuhakikisha vipindi vyake vinaonekana kwa wananchi.
Kuhusu kuzuiwa kwa waandishi wa habari kufanya kazi zao, alisema ni kuweka vizuizi ili kuhakikisha wananchi hawapati habari zinazotakiwa jambo ambalo si sahihi.
Alisema wananchi wana haki ya kujua kinachojadiliwa na wawakilishi wao na siyo kusubiri vipunguzwe na kwamba kuwaeleza kuwa walikuwa wanaangalia TV muda mwingi halina mashiko kwa kuwa wanaweza kuangalia vipindi vingine kwa muda huo.
Imeandaliwa na Fredy Azzah, Dodoma, Mwinyi Sadallah, Zanzibar, Christina Mwakangale na Salome Kitomari, Dar
CHANZO: NIPASHE
3 comments:
Very strange! Magufuli naye anakubaliana na hili?
Wadau. Tunaipenda nchi yetu na iweze kujulikana katika dunia sionwajue tu Kenya, Uganda! Kama matangazo ya ndani ya Bunge na kuwajua jinsinwabunge wanavyochanhia hoja kwa mantiki ya maendeleo ya wananchi ni kujidanganya na kuwadanganya hata walenwanaopenda kuchangia maendeleonna kuwekeza! Ni aibu tupu malumbanonna kuwazuia wapinzani ambao ndio chachu ya mabadiliko.. KAMWE hakuna mabadiliko ndani ya CCM ya k8na JM NP!!!?
ccm mbele kwa mbele hapa kazi tu.haaaaaaaaaaaaaaaaaa.
Post a Comment