ANGALIA LIVE NEWS

Friday, January 29, 2016

Samatta yuko Ubelgiji kukamilisha dili.

Mbwana Samatta ameanza safari yake ya kutimiza ndoto ya kucheza soka la kimataifa Ulaya na sasa yuko mjini Brussels, Ubelgiji kukamilisha taratibu za kujiunga na Klabu KRC Genk.

Hata hivyo, Samatta amekwenda huko bila ya barua kutoka kwa mwajiri wake wa zamani, Mabingwa wa Afrika -- TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Meneja wa nahodha huyo wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Jamal Kisongo alisema jana kuwa pamoja na Samatta -- mshindi wa Tuzo ya Mchezaji Bora Afrika mwaka jana kuondoka bila barua, lakini amepewa baraka zote na mmiliki wa Mazembe Moise Katumbi.

Kisongo alisema kama taratibu za usajili wa kimataifa zitakamilika mapema kupitia njia ya mtandao wa mawasiliano ya kompyuta (internet), basi Samatta ataanza kuvaa jezi za Genk wiki ijayo.

"Mazungumzo ya awali na KRC Genk yalishakamilika na kinachofuata ni kukamilisha taratibu. Katumbi alimpigia simu Samatta Jumanne wiki hii na kumtaka kuanza safari ya kwenda Ubelgiji kwa vile mambo mengi yanaweza kufanya kupitia mtandao," alisema Kisongo.

Samatta juzi usiku aliandika katika tovuti kuwa amewasili salama nchini Ubelgiji.

Samatta alionyesha kuwa na msimamo wa kutaka kuichezea Klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Ubelgiji na kuitosa Nantes ya Ufaransa, ambayo bosi wake Katumbi alikuwa anashinikiza ajiunge nayo.

Hata hivyo, meneja wa Samatta alisema mchezaji huyo atakuwa na nafasi kubwa ya kucheza akiwa na KRC Genk kuliko kama angeamua kwenda Nantes.
CHANZO: NIPASHE

No comments: