ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, January 14, 2016

Wahamiaji haramu 48 wafukuzwa

Afisa Uhamiaji mkoa wa Dar es Salaam, Naibu Kamishna, Johannes Msumule akizungumza katika mkutano na Waandishi wa Habari.
Afisa Uhamiaji mkoa wa Dar es Salaam, Naibu Kamishna, Johannes Msumule akizungumza katika mkutano na Waandishi wa Habari.

IDARA ya Uhamiaji Mkoa wa Morogoro imewatia mbaroni wahamiaji haramu 48 na kuwafukuza nchini na baadhi yao kufikishwa mahakamani kwa kuingia nchini na kufanya kazi kinyume cha sheria.

Wahamiaji haramu hao walikamatwa kwa nyakati tofauti kuanzia Septemba mwaka jana hadi Januari mwaka huu kutokana na msako mkali uliofanywa na maofisa wa idara hiyo katika maeneo mbalimbali ndani ya mkoa huo.

Naibu Kamishna wa Uhamiaji wa Mkoa wa Morogoro, Agustino Haule, alisema hayo jana ofisini kwake mjini hapa alipokuwa akielezea hatua mbalimbali zinazochukuliwa na idara hiyo katika hatua ya kukabiliana na wimbi la wahamiaji haramu na walioingia nchini na kufanya kazi kinyume cha sheria.

Alisema wahamiaji haramu kutoka mataifa mbalimbali walipatikana katika msako uliofanyika maeneo mbalimbali ikiwemo viwandani, shuleni, majumbani na katika taasisi mbalimbali zilizopo mkoani Morogoro. Hivyo aliwataja wahamiaji haramu hao ni kutoka katika nchi za Kenya, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

“Msako huu wa kuwakamata wahamiaji haramu unaendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali mkoani Morogoro na hadi sasa wahamiaji haramu 48 wamekamatwa katika maeneo mbalimbali kwa kipindi cha Septemba mwaka jana hadi Januari mwaka huu,” alisema Naibu Kamishna wa Uhamiaji Mkoa wa Morogoro.

Hivyo alisema baadhi ya wahamiaji hao tayari wameshafikishwa mahakamani na kutozwa adhabu na pia kurejeshwa nchini kwao na wengine kesi zao zikiendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa.

HABARI LEO

No comments: