Dar es Salaam. Kiongozi wa ACT-Wazalendo Zitto Kabwe, amesema chama chake kimetumia Sh656 milioni ikiwa ni mapato na matumizi katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana na chaguzi ndogo.
Zitto alitangaza mapato hayo juzi wakati akitoa maazimio ya Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo iliyokutana Februari 13, Dar es Salaam.
Alisema wameamua kuweka wazi gharama hizo kama walivyohaidi katika kuzingatia tunu ya uwazi ya ACT-Wazalendo, kwa masilahi ya Watanzania.
“Tumeamua kuweka wazi ili Watanzania wajue tulichokipata na tulikitumia. Nitoe changamoto tu kwa vyama vingine kikiwamo CCM kutangaza mapato na matumizi yao katika uchaguzi uliopita,” alisema Zitto.
Mbali na hilo, Zitto alisema kamati kuu pia, imeazimia kufanya siasa za maendeleo kipindi cha miaka mitano na kuachana na vijembe, vurugu na kejeli ambazo hazina msingi kwa chama hicho.
“Kaulimbiu yetu itakuwa ni ‘siasa na maendeleo’.Tunataka kuwatumikia wananchi kwa kushiriki katika miradi ya maendeleo,” alisema Zitto.
Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo Bara, Msafiri Mtemelwa alisema baadhi ya fedha hizo walizipata kutoka kwa wadau mbalimbali huku kiongozi wa chama hicho akiwa miongoni mwa watu waliochangia ili kufanikisha uchaguzi huo.
No comments:
Post a Comment