Chato. Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Chato mkoani Geita, imemhukumu kwenda jela miaka 30, Mwalimu wa Sekondari ya Makurugusi, Idd Gerald (21) baada ya kupatikana na kosa la kumbaka mwanafunzi wa kidato cha pili.
Hukumu hiyo ilitolewa jana kwenye kilele cha siku ya sheria iliyofanyika katika viwanja vya Mahakama hiyo na kuhudhuriwa na umati wa watu.
Hakimu wa Mahakama hiyo, Jovith Kato alimtia hatiani mshtakiwa kutokana na upande wa mashtaka kuwasilisha ushahidi uliojitosheleza pasipo kuacha shaka yoyote.
Akisoma huku, hakimu huyo alisema mshtakiwa alitenda kosa hilo Machi 23, mwaka jana saa saba usiku akiwa ndani ya chumba chake kilicho karibu na shule hiyo.
Alisema siku hiyo alimshawishi mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 16 na wakati anatekeleza kitendo hicho alipiga kelele za kuomba msaada kutokana na maumivu aliyokuwa akiyapata.
Hakimu alisema baada ya mwanafunzi huyo kupiga kelele, walijitokeza wanafunzi wenzake na mwalimu mmoja waliomdhibiti mshtakiwa kisha wakamkabidhi kwa ofisa mtendaji wa kijiji usiku huo.
Alisema ushahidi wa watu saba uliowasilishwa mahakamani hapo na upande wa mashtaka, kielelezo cha fomu namba 3 ya polisi (PF3) na maelezo ya daktari vilithibitisha kwamba mlalamikaji alibakwa.
Hakimu Kato alisema mwanafunzi huyo alikutwa na mbegu za kiume na michubuko kwenye sehemu zake za siri.
Awali, mshtakiwa alijitetea kuwa hakutenda kosa na kuwa siku ya tukio aliacha mlango wazi kwa lengo la kumruhusu rafiki yake aingie ndani kwa urahisi, lakini alikiri mwanafunzi huyo kuingia chumbani kwake.
Hakimu huyo alisema mwanafunzi huyo anaweza kuwa aliridhia kufanya mapenzi na mwalimu wake, lakini sheria inazuia mtu yeyote kufanya mapenzi na mtu mwenye chini ya miaka 18.
No comments:
Post a Comment