ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 17, 2016

Kiama cha mafisadi.

Sasa ni dhahiri kiama cha mafisadi kimetimia baada ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuwasilisha bungeni mapendekezo mbalimbali ili kuipa meno zaidi ya kuchunguza na kufuatilia mali zinazomilikiwa na watumishi wa umma isivyo halali.

Hatua hii imelenga katika kuhakikisha kwamba Serikali ya Rais Dk. John Magufuli, inawashughulikia mafisadi kikamilifu.

Aidha, mapendekezo hayo yanalenga kufanya marekebisho ya vifungu 16 ambavyo vipo kwenye vipengele vitatu vya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Namba 13 ya mwaka 1995, ambayo kwa kiasi kikubwa haikutoa nguvu za kisheria kwa Sekretarieti kutekeleza majukumu yake kwa uhuru.


Akijibu swali la mwandishi wa Nipashe aliyetaka kujua jinsi gani sekretarieti hiyo inatafuta kuwa na meno katika utekelezaji wa majukumu yake, Ofisa Sheria Mkuu wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Filotheus Manula, alisema tayari mapendekezo ya mabadiliko ya sheria hiyo yamewasilishwa bungeni.

“Mapendekezo yetu tayari yapo bungeni tangu mwaka jana, tunachosubiri ni mjadala,” alisema.

Alifafanua kuwa baadhi ya vifungu ambavyo moja kwa moja vinawabana watumishi wa umma na kutoa mamlaka kwa sekretarieti hiyo kutekeleza majukumu yake kuwa ni pamoja na Kamishna kumuita na kumhoji mtumishi ambaye wana taarifa zake.

Alitaja baadhi ya maeneo ambayo wamependekeza kufanyike maboresho kuwa ni kuwapa mamlaka zaidi kisheria kuchunguza malalamiko dhidi ya viongozi wa umma yanayowasilishwa kwa njia mbalimbali.

Lingine ni kutoa kinga kwa watumishi wa Sekretarieti wanaofanya kazi za uchunguzi, jambo ambalo halikuwa limetajwa kisheria na kuwa kikwazo katika utekelezaji wa majukumu yao.

Eneo lingine ni muda wa baraza kutoa uamuzi na kuwasilisha kwa Rais, awali haikuwa na muda maalum, lakini mapendekezo waliyowasilisha ni baraza kufanya kazi kwa kipindi cha miaka mitatu mitatu.

Manula aliongeza kuwa eneo lingine ni kufanya uhakiki, ambao ni baada ya kupokea fomu ya tamko la mali na madeni kwa watumishi wa umma, awali hawakufuatilia kwa karibu kilichojazwa kwenye fomu husika, lakini kwa mapendekezo hayo wanataka kuwa na meno ya kufuatilia ukweli wa kilichojazwa.

“Kwa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995, ufuatiliaji ulifanyika kwa agizo la Rais, lakini kwa mapendekezo haya tunataka tuwe tunafuatilia wenyewe kwa mujibu wa sheria,” alifafanua.

Aidha, alisema mapendekezo mengine ni nguvu ya kisheria kumuita kiongozi yeyote wa umma kwa hati ya wito kwa ajili ya kumhoji, kwani kwa sheria ya sasa walitumia Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma linapokutana ndiyo limuandikie barua ya wito mhusika.

“Mapendekezo yetu kuwe na mamlaka kisheria kwa Kamishna kumuita mto yeyote na kumhoji,” alisema.

Manula alisema kipengele cha pili ni kuimarisha mfumo wa mawasiliano baina ya mamlaka mbalimbali za serikali kama Polisi na Takukuru, ambayo awali yalikuwa ya kawaida.

Mawasiliano mengine ni baina ya Sekretarieti na wananchi wenye taarifa mbalimbali na wanaokwenda kutoa ushahidi kwenye Baraza kuhakikishiwa usalama wao ikiwa ni pamoja na kulipwa stahiki zao.

Kuhusu Baraza kutoa uamuzi baada ya kusikiliza shauri lililofikishwa mbele yao na kuamua, alisema itabaki kama ilivyo kwenye sheria ya sasa kuwa Rais atapelekewa mapendekezo ya Baraza na hawawezi kutoa hukumu kwa kuwa siyo chombo cha kuhukumu bali kazi hiyo imepewa mahakama.

Mwanasheria huyo alisema kipengele kingine ni kutungwa kwa sheria maalum ya kudhibiti mgongano wa maslahi kwa watumishi wa umma hasa inapotokea kiongozi husika ana maslahi binafsi katika eneo lake la kazi ili visigongane na majukumu yake kazini.

Alisma mathalani, Kamishana wa Madini awe ni mmiliki wa mgodi, ni lazima sheria itaje wazi namna gani ataepuka kushughulikia mgodi wake kwa nafasi aliyonayo ili afanye kazi za umma.

Kwa muda mrefu Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kupitia Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma, limeendesha mashauri mbalimbali kuhusiana na matumizi mabaya ya mali ya umma.

Baadhi ya viongozi waliowahi kuhojiwa na baraza hilo ni pamoja na Mwenyekiti wa sasa wa Bunge, Andrew Chenge, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka, aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufilisi na Udhamini (Rita), Philip Saliboko.

Wote hao walifikishwa mbele ya baraza hilo kwa madai ya kutumia ofisi na mamlaka ya umma kujipatia mgawo wa fedha za Tegeta Escrow.
 
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Na wote waliofikishwa mbele ya baraza hilo bado wanafanya kazi serikalini. Wengine bado wanapigiwa kura majimboni mwao. Mh Raisi aliuliza ni shetani gani huyu katuloga ? Tunajiloga sisi wenyewe