ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 17, 2016

Dk Mahiga ajibu kwa nini Rais JPM hakuonekana sherehe ya mabalozi

By Raymond Kaminyoge, Mwananchi; rkaminyoge@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk Augustine Mahiga amemtetea Rais John Magufuli kwa kutohudhuria hafla ya mwaka ya mabalozi akisema alikuwa Singida kwenye maadhimisho ya miaka 39 ya CCM.

Balozi Mahiga alikuwa mgeni rasmi kwenye hafla hiyo iliyofanyika Ikulu ya kukaribisha mwaka mpya wa mabalozi ambayo kwa kawaida mwenyeji huwa ni Rais.

Dk Mahiga alitoa ufafanuzi huo kwa waandishi wa habari jana baada ya kuulizwa sababu za Rais kushindwa kuhudhuria hafla hiyo, lakini maelezo hayo yalichanganya zaidi, kwa kuwa hafla hiyo ya mabalozi ilifanyika Februari 8 wakati kilele cha sherehe za CCM kilikuwa Februari 6.

Kuhusu tofauti hiyo ya siku, Dk Mahiga alisema baada ya sherehe ya Singida, Rais alipitia kwenye ziara ambayo hata hivyo hakuifafanua.

Wakati huohuo, Waziri Mahiga alisema licha ya Dk Magufuli kuwakilishwa kwenye mikutano katika nchi mbalimbali, nchi hizo zinafahamu anachokifanya na bado nchi inaheshimika.

Akitoa mfano, katika mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika ulioandaliwa na China ambao ulifanyika Afrika Kusini, alisema licha ya Tanzania kuwakilishwa na makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ilikuwa miongoni mwa nchi nne kati ya 54 za Afrika zilizopewa kipaumbele na kuwekeza katika sekta ya viwanda. Nchi nyingine zilizopewa kipaumbele ni Kenya, Ethiopia na Afrika Kusini.

“Utaona namna tunavyokubalika kimataifa kati ya nchi 54 za Afrika tunakuwa miongoni wa nchi nne zitakazopewa kipaumbele,” alisema.

Alisema wizara yake itaendelea kubana matumizi kwa kuziwezesha balozi za nje ili ziwe na uwakilishi imara.

Akitoa mfano, Dk Mahiga alisema juzi alirejea kutoka Angola ambako alimwakilisha Rais Magufuli kwenye mkutano wa Maziwa Makuu, akiongozana na watu watatu tofauti na zamani ambako angekuwa na msururu wa watu.

Alisema hata Makamu wa Rais alipokwenda Ethiopia kwenye mkutano wa Umoja wa Afrika (AU) alisafiri na watu 14 wakati zamani angesafiri na zaidi ya watu 30.

No comments: