Advertisements

Saturday, February 6, 2016

Lowassa ahofu Al-Qaeda kujipenyeza Zanzibar

Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana. PICHA:SELEMANI MPOCHI

ALIYEKUWA mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambaye alikuwa akiungwa mkono na vyama vinavyounga mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, ameonya kuwa ipo hatari Zanzibar ikatumiwa kuwa njia ya kuingia magaidi wa aina ya Al-Qaeda nchini endapo jitihada maalum hazitafanyika sasa katika kumaliza mkwamo wa kisiasa visiwani humo na kuzuia uwezekano wa kuvunjika kwa hali ya amani.

Akizungumza katika mahojiano maalum jana, Lowassa aliyetangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwa alishika nafasi ya pili katika Uchaguzi Mkuu uliopita kwa kupata asilimia 39.97 ya kura zote halali zilizopigwa, alisema hivi sasa hali ya Zanzibar ni tete na hivyo, hekima na busara ya hali ya juu inahitajika ili kuirejesha katika utulivu wa kisiasa.

Lowassa alitoa ufafanuzi huo wakati akijibu swali kuhusiana na hali ya Zanzibar katika kipindi hiki ambacho vyama vikuu viwili visiwani humo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) vimekuwa vikivutana kuhusiana na hatma ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2016 kabla ya kufutwa siku tatu baadaye na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha.

CUF wanaoamini kuwa mgombea wao, Maalim Seif Shariff Hamad alikuwa akiongoza kwa zaidi ya asilimia 50 dhidi ya mpinzani wake, Rais Ali Mohamed Shein, wanasisitiza kuwa uchaguzi ulikuwa huru na wa haki na hivyo ZEC iendelee na mchakato wa kujumuisha matokeo na kumtangaza mshindi. Hata hivyo, CCM wamekuwa wakiunga mkono uamuzi wa ZEC ambao ni kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi uliopita na kuandaliwa kwa uchaguzi mwingine utakaofanyika Machi 20. Tayari CUF wametangaza kutoshiriki uchaguzi huo na kutaka maamuzi ya wananchi waliyoyafanya Oktoba 25 kupitia sanduku la kura yaheshimiwe, huku CCM wakisisitiza kuwa watashiriki uchaguzi huo na kuwataka wanachama wake wajiandae kuibuka na ushindi.

Akizungumzia hali hiyo, Lowassa alisema siyo njema kwa mustakabali wa Zanzibar na Tanzania, hivyo akawataka Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete, Rais John Magufuli na viongozi wakuu wa Zanzibar kurejea kutafuta ufumbuzi wa suala hilo kupitia meza ya mazungumzo badala ya kuachia hali iliyopo sasa ambayo inaweza kuviingiza visiwa hivyo katika mgogoro mkubwa utakaotoa mwanya kwa vikundi vya kigaidi kujipenyeza.

“Nachukua fursa hii kumtaka Jakaya Kikwete kama Mwenyekiti wa CCM, Rais Magufuli na viongozi (wakuu) wa Zanzibar kuchukua hatua zinazostahili sasa. Wasisubiri hali iwe mbaya zaidi….naogopa tatizo la Zanzibar litasumbua pia Bara,” alisema Lowassa na kuongeza:

“Pili, (kama tatizo halitapatiwa ufumbuzi), makundi kama Al-Qaeda yanaweza kupata nafasi ya kujipenyeza. Sasa hivi (Al-Qaeda) wako katika nchi za jirani tu… kama CCM na CUF walikaa wakati ule na kukubaliana kuanzisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa, kwanini ishindikane sasa?”

Al-Qaeda ni kundi la kigaidi ambalo limekuwa tishio duniani baada ya kufanikisha mashambulizi mbalimbali duniani yakiwamo yaliyohusisha milipuko ya jengo la kituo cha biashara Marekani (WTC), makao makuu ya jeshi la Marekani, Pentagon na pia ofisi za ubalozi wa Marekani nchini Tanzania na Nairobi, Kenya.

Kadhalika, Lowassa alisema ni vyema majadiliano yoyote yenye lengo la kuitoa Zanzibar kutoka katika mkwamo wa kisiasa ni yakawashirikisha pia watu kutoka vyama vingine mbali na CCM na CUF, lengo likiwa ni kuona kuwa suluhu inapatikana katika namna ya kuhakikisha kuwa amani ya visiwa hivyo inadumishwa.

Kuhusiana na muungano, Lowassa alisema kwa mtazamo wake, jambo pekee linaloonekana kuwa kero kubwa kwa sasa ni uchaguzi tu, lakini mambo mengi ni madogo madogo na yanapaswa kuendelea kufanyiwa kazi kama ilivyokuwa kwa suala la mafuta.

“Maalim Seif aliwahi kuniambia kuwa hakuna anayetaka kuvunja muungano… bali anachotaka ni haki sawa kwa wote, wanataka nafasi ya Zanzibar itambulike zaidi, vitu vidogovidogo vifanyiwe kazi…kwa mfano, Kikwete alilifanyia kazi suala la mafuta. Hivi sasa hakuna mengi ya kutugawa (Zanzibar na Bara) ukiondoa uchaguzi. Nalo tusiruhusu litugawe,”

alisema Lowassa. Baada ya Uchaguzi Mkuu Zanzibar, Jecha alitangaza kufutwa kwa matokeo yote ya uchaguzi wa visiwa hivyo kwa maelezo kuwa uchaguzi haukuwa huru na wa haki. Hata hivyo, uamuzi wake huo ulipingana na taarifa za waangalizi wa uchaguzi wa ndani na wa kimataifa waliouelezea kuwa ulikuwa huru na wa haki, baadhi yao wakiwa ni waangalizi kutoka Umoja wa Ulaya (EU), Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Madola, Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na pia taasisi inayojihusisha na uangalizi wa uchaguzi nchini (TEMCO).

NEC SI LOLOTE, SI CHOCHOTE
Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva, alikaririwa akisema kuwa tume yake (NEC) iko huru. Hata hivyo, Lowassa alipinga madai hayo ya Lubuva kwa kusema kuwa hayana ukweli kwani NEC haikuwa huru na kwamba, yale yaliyojitokeza katika uchaguzi mkuu uliopita ni ushahidi tosha kuwa chombo hicho hakifanyi kazi kwa maslahi ya Watanzania bali kimekuwa kikitumika kwa ajili ya kuibeba serikali ya chama tawala.

“Kauli ya Lubuva kudai kuwa NEC iko huru siyo kweli… NEC siyo huru, si chochote, si lolote, ni chombo kinachotumika. Hawafai kabisa,” alisema Lowassa na kuongeza:

“Tume huru haiwezi kuambiwa kuna maboksi ya kura yamekamatwa halafu yenyewe ikabaki kimya, haiwezi kuambiwa watu wanatishwa halafu wao hawasemi lolote… ni tume iliyotumika kupora ushindi wangu.”

Awali, Lowassa alisisitiza kuwa ni yeye ndiye aliyeshinda katika uchaguzi huo ambao NEC ilimtangaza Magufuli kuwa mshindi kutokana na kupata asilimia 58.46 ya kura zote halali zilizopigwa.

“Kura zilichakachuliwa kwa kiasi kikubwa, mie ninajua, dunia inajua, itoshe kusema tu (NEC) walichakachua,” alisema.

Akieleza zaidi, Lowassa alisema anashukuru tuzo ya amani aliyotunukiwa hivi karibuni na taasisi moja kwani hiyo ni ishara ya kutambua mchango wake katika kuhakikisha kuwa hatoi kauli za kuchochea vurugu baada ya uchaguzi bali kudumisha amani katika nchi licha ya kila mmoja kujua kuwa kura zake zimechakachuliwa.

“Baada ya matokeo, watu wengi, hasa vijana, walitarajia niwaambie waingie barabarani, sikufanya hivyo, bali nikawaambia tulieni… ni kwa sababu tu ya kutunza amani. Lugha hiyo kwa wanasiasa wengi wa nchi za Afrika siyo ya kawaida. Nawashukuru zaidi Watanzania kwa kunielewa japo hawakukubaliana na matokeo,” alisema Lowassa.

NAFASI YAKE CHADEMA
Alipoulizwa kuhusiana na uwezekano wa kugombea uongozi ndani ya Chadema, Lowassa aliyeiwezesha Chadema kupata kura zaidi ya milioni 6, akiwakilisha pia muungano wa vyama rafiki vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, alisema ametosheka na nafasi yake ya sasa ya kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.
Aliongeza kuwa hivi sasa, anajiandaa kuzunguka nchi nzima kwa ajili ya kuwashukuru wananchi waliompa kura nyingi kwenye uchaguzi na pia kukitangaza zaidi chama chake. “Mimi ni mjumbe wa kamati kuu… kazi yangu kubwa (kwa sasa) ni kuimarisha chama. Nitazunguka nchi nzima kushukuru kwa kura walizotupa,” alisema Lowassa.

AZUNGUMZIA WABUNGE, POLISI KUINGIZWA BUNGENI
Akizungumzia mwenendo wa Bunge la sasa, Lowassa aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Monduli kwa miaka 20 mfululizo, alisema linatia moyo kwa vile lina vijana wengi wasomi, hasa kutoka kambi ya upinzani, na kwamba anaamini litafanya kazi nzuri kwa maslahi mapana ya taifa. Hata hivyo, alilaani hatua ya hivi karibuni ya polisi kuruhusiwa kuingia bungeni kwa ajili ya kuwadhibiti wabunge wa upinzani waliokuwa wakipinga kitendo cha kuzuia demokrasia kutokana na uamuzi wa serikali wa kusitisha urushaji wa matangazo ya moja kwa moja ya Bunge kwa kisingizio cha kuepuka gharama.
“Polisi kupelekewa bungeni ni jambo la aibu. Moja ya mambo alituachia Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ni kuheshimu maridhiano….siasa ni mabishano, kwa nini polisi watumike?” Alihoji. Aidha, alishangazwa na hatua ya serikali kuzuia urushaji matangazo ‘live’ ya bunge kupitia televisheni ya taifa (TBC) kwani maeneo mengi ambayo demokrasia hupewa nafasi yake jambo hilo hufanyika.
“Kwa nini matangazo ya Bunge yasirushwe moja kwa moja? Huku ni kuminya demokrasia,” alisema.

CCM IMSAHAU KABISA
Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kurudi CCM ikiwa Magufuli atashika madaraka na kurejesha misingi iliyoasisiwa na Mwalimu Nyerere, Lowassa alisema kamwe hatafanya jambo hilo.
“Sirudi CCM…sina mpango huo,” alisema Lowassa.

SIKU 100 ZA MAGUFULI
Wakati wiki ijayo Magufuli akitarajiwa kufikisha siku 100 tangu aapishwe kuwa Rais Novemba 5, 2015, mengi yamekuwa yakisemwa kuhusiana na utendaji wake. Alipotakiwa atoe maoni yake, Lowassa alisema wakati wa kufanya hivyo haujafika na kwamba, kufanya hivyo ni kutomtendea haki kwa vile duniani kote, mwelekeo wa utendaji wa marais wapya hupimwa baada ya siku 100. “Marais huhukumiwa baada ya siku 100…nitatoa tathmini baada ya siku hizo kutimia,” alisema Lowassa.

KATIBA MPYA, TUME HURU UCHAGUZI
Lowassa alisema hivi sasa, mara zote amekuwa akitumai na kuomba katiba ya sasa ibadilishwe na tume ya uchaguzi iwe huru ili mwishowe Watanzania wapate mabadiliko wanayotaka kupitia sanduku la kura kwani vinginevyo, kwa utaratibu wa sasa, ni vigumu kwa chama kingine kuiengua CCM.

“Bila katiba mpya, tume huru ya uchaguzi, itakuwa ngumu… mie najiuliza, tunajiondoa vipi katika hali hii? Jambo lolote huhitaji maamuzi ya wengi, na wengi (bungeni) wako CCM, je, tutajinasua vipi? Watanzania tufikirie, tena tufikirie sana, wasomi wafikirie,” alisema.
CHANZO: NIPASHE

11 comments:

Anonymous said...

SASA WEWE MZEE LOWASSA HIVI KWELI ZINAKUTOSHA? WEWE UNAOMBEA KUJA KWA ALQAIDA KWELI MTU MZIMA YAANI HATA UOGA HUONI KUTAMKA KITU HICHO NDIO MAANA WEWE NA CHAMA CHENU CHA CHADEMA MNAPENDA VURUGU KAMA CUF YA ZANZIBAR, MAAN NINYI KILA SIKU MNOMBEA FUJO TU ITOKEE,KWANINI? MBONA HUTUWAELEWI? WAAMBIE HAO ALQAIDA WAJE TU WATAKUMBANA NA JESHI LA MWAMUNYANGE, MTU MZIMA HUNA AKILI. KWA NINI UMEFIKIRIA HILO? AU WEWE UNAONA ALQAIDA NI SAWATU WAINGIE KWA ZSABABU UPINZANI MMEKOSA UONGOZI HIYO NI SAWA TU HATA ALQAIDA WAKIJA KUUA?

HAME ON YOU OLD MAN

Anonymous said...

Hee! Makubwa haya! Kwani CUF kushindwa ndo kuwa Al Queda?

Anonymous said...

Mapema kutambua na kuunga mkono jitihada za Magufuli? Really? Huyu Bwana kweli bankrupt. Watanzania sisi tunazitambua, tunamuunga mkono Magufuli na tunamuombea. Wanasiasa wachwala, wabinafsi na wanafiki hatuna muda nao tena. Lowassa Kama ukweli unakushinda kapumzike na fedha ya mafisadi wenzako.

Anonymous said...

nampenda sana lowassa anafikra nzuri sana lakini la hili la alqaeda sikubaliani nalo.japo kuwa huwa anatafakarii nzuri mzee huyu.ushauri wa bure usiwe kama waatu wa west kila kitu kuwasingizia alqaeda.

japo kuwa wanaweza kuja kweli wakasawazisha mambo poa visiwani na bara lakini si kila kitu kuwasingizia alqaeda kama wa west.

Anonymous said...

Lowassa is a sick man and irrelevant. Al-Qaida watakuja kule kijijini kwako, Moduli.

Anonymous said...

Nchi inahitaji kuwa na vyama vya upinzani ili viweze kuisimamia serikali itimize majukumu na ahadi zake na kamwe tusijidanganye kuwa "KUWANYANYASA WAPINZANI NDIYO UZALENDO" au "KUWANYIMA HAKI ZAO" ni kitu cha kujivunia, Huo ni ulimbukeni wa KISIASA na kamwe hautatufikisha popote.
Hongera sana mzee Lowasa kwa busara zako la sivyo leo TZ tungekuwa tunauwana wenyewe kwa wenyewe kwa tamaaa za viongozi wa CCM za kug'ag'ania madaraka hata pale waliposhindwa!!.

Anonymous said...

Siku zote huwa na question uwezo wa kufikiri wa huyu mzee..Kauli kama hizi zinafanya niendelee kumshukuru Mungu kwa kutuepushia huyu mzee kuwa raisi wetu..

Anonymous said...

Kweli Lowassa umekuwa mjinga to this level? Unaitishia nchi yetu kuwa Alqueda wataingia na kufanya vurugu kama CUF na Maalim hawapewi Ukubwa? Sasa mzee umeingia kambi ya Alqueda, na kuwa msemaji wao au wamekuahidi nafasi ya Uongozi (head representative) wao nchini Tanzania? Unakumbuka kilichompata Bin Laden? I hope this is not a joke, and if so, it is a very dangerous one. Kauli yako ni hatari sana kwa usalama wa Taifa letu, na hivyo Watanzania na serikali yetu lazima tuwe macho na wewe mzee. Wewe na Maalim Seif mnaweza kuwanunua na kuwaleta hao Alqueda wenu, lakini mjue mtakiona cha mtema kuni. Watanzania tupo tayari kuwasaka na kuwateketeza bila huruma. Bring it on!

Anonymous said...

Huyu lowassa yupo Kama clinton au Jeb bush .Wamelewa siasa mpaka hawajitambui .will say anything to get attention .unafikiri nyerere alikuwa mjinga kuwaweka huko zanzibar.Unguja peke Yao na Pemba peke Yao .watu wanaona mbali wewe .

Anonymous said...

Anakusudia kuwa CUF ndo ALQAEDA yani wakikosa ushindi watageuka kuwa ALQAEDA hii ni fikira potefu lowassa na nikuwapa wazo hili watu wasokuwa na msimamo mzuri waanzishe hichi kikundi, kosa kubwa sana kusema hivyo kama vile unasapoti na unataka yatokee hayo makundi znz, na pia kuonyesha kuwa ww haupo na hivyo vyama ila kimaslahi yako tu, mungu aepushe hiloa balaa kwa Tanzania yote na visiwani fikiria kabla hujasema neon..

Anonymous said...

Mbona Alqaeda washafika na video washatoa siku nyingi ?