Mafuta ya taa lita 1,200 na kilo 98 za dawa za kulevya aina ya mirungi, vimekamatwa vikiwa katika harakati za kuingizwa nchini kwa njia za panya katika mpaka wa Tanzania na Kenya wa Horohoro.
Bidhaa hizo ambazo zilikuwa zikiingizwa kwa njia za magendo, zilikamatwa katika pori lililo karibu na mpaka huo.
Kukamatwa kwa mafuta na mirungi hiyo, kunatokana na kazi maalumu iliyofanywa na timu ya maofisa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Idara ya Uhamiaji, Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) kwalioko katika mpaka wa Horohoro.
Ofisa wa TRA, Edwin Iwato, alisema operesheni hiyo ilifanyika kwa lengo la kukabiliana na mitandao ya uhalifu kupitia mpakani, sambamba na kuwakamata na kuwachukulia hatua wafanyabishara wanaotumia njia za panya ili kukwepa kodi.
Iwato alisema kwa sasa watendaji kutoka idara mbalimbali zinazofanya kazi kwenye mpaka huo, wamejiwekea utaratibu wa kuhakikisha wanapambana na uhalifu huo, kutokana na kukithiri kwa vitendo vya uvunjaji wa sheria za nchi, ikiwamo uingizaji holela wa wahamiaji haramu, dawa za kulevya na bidhaa za magendo.
“Operesheni hii ni maalum katika kupambana na wahalifu hawa na huu ni mwanzo tu lakini itakuwa endelevu. Watakaobainika kuhusika na vitendo hivi, watafikishwa kwenye vyombo vya sheria,” alisema.
Kwa upande wake, Mrakibu Mwandamizi wa Idara ya Uhamiaji Kituo cha Horohoro, Mwesiga Lubalila, alisema bidhaa hizo zilikamatwa baada ya wahusika kubaini mtego uliokuwa umewekwa. Alisema wahusika walipobaini kuwa wanafuatiliwa, walipotupa pikipiki na kukimbia.
“Kundi la watu waliokuwa na pikipiki zilizobeba maboksi, walipobaini mtego wa kukamatwa walizitupa pikipiki na kisha kukimbia.
Tulipopekua tulikuta dawa za kulevya aina ya mirungi zenye uzito wa kilo 98 zilizokuwa zimefungwa katika vifurushi vyenye uzito wa kilo moja moja,” alisema.
CHANZO: NIPASHE
1 comment:
dam hivi mirungi ni dawa za kulevya?konyagi na Kilimanjaro larger tuziiteje?
Post a Comment