ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, February 25, 2016

Magufuli awalaza njaa 'wapiga dili'

Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli, imeamua kutumia mfumo wa ‘Cash Budget (kutumia kilichokusanywa), huku baadhi ya wachumi wakisema utaleta nidhamu ya matumizi ya serikali na kubana watumishi ambao walizoea kutumia vibaya fedha za umma kwa kuzipangia matumizi yasiyo na tija.

Wizara ya Fedha na Mipango imeieleza Nipashe jana kuwa, mfumo wa kupanga na kutumia kinachokusanywa na Mamlaka ya Mapato (TRA), ndiyo ulioamuliwa kutumiwa na serikali ya awamu ya tano.

Itakumbukwa kuwa, tangu Novemba mwaka jana, mapato ya TRA yalipanda kutoka wastani wa Sh. bilioni 800 na Sh. bilioni 900 kwa mwezi mpaka Sh. trilioni 1.3, Desemba, mwaka jana Sh. trilioni 1.4, Januari, mwaka huu Sh. trilioni 1.06 na malengo ya Februari ni kukusanya Sh. 1.03.

Jana Ofisa Habari wa Wizara ya Fedha na Mipango, Ingiaheddi Mduma, alisema utaratibu wa kutumia kilichokusanywa utaendelea kutumika kila mwezi.

Alisema kila makusanyo yatakayopatikana kwa mwezi husika, yatatumika kulingana na mahitaji husika ya mwezi huo.

“ Mahitaji yakiwa mengi katika mwezi husika, basi hata fedha itakayokusanywa kwa mwezi huo itatumika kulingana na mahitaji hayo, tutakuwa tunafanya hivyo kila mwezi,” alisema Mduma.

WASOMI WAZUNGUMZA
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Wilhelm Ngasamiaku, alisema mfumo ambao unatumiwa na serikali ya awamu ya tano unajulikana zaidi kama ‘Cash Budget,’ ambapo mipango na matumizi ya serikali inabidi ipangwe kutokana na kile
kinachokusanywa.

“Kutumia kile unachokipata hiyo ndiyo ‘Cash Budget’, siyo mara ya kwanza mfumo huu kutumiwa hapa nchini hata miezi ya mwisho ya serikali ya awamu ya nne baada ya wahisani kuacha kutoa misaada, ulitumika.

Huu mfumo faida yake unaleta nidhamu ya matumizi ya serikali kwa hiyo inaifanya itumie na kupanga kutokana na makusanyo yake ya ndani, ndiyo sifa pekee ya mfumo huo.

“Hasara yake ni kwamba unaposhindwa kukusanya mapato ya kutosha, matumizi yako mengi uliyopanga kuyafanya utashindwa kuyagharimia na kwa sababu unatumia unachokusanya ni lazima nguvu nyingi zielekezwe kwenye kukusanya,” alisema Dk. Ngasamiaku.

Alisema kwa muda mfupi ambao Rais Magufuli ameanza uongozi wake, suala la makusanyo limeongezeka kuanzia Novemba, Desemba na Januari, ingawa fedha za nyuma ambazo hazikukusanywa zimesaidia ongezeko hilo.

Alisema kuongeza zaidi mapato kutawezekana endapo biashara nyingi za wajasiariamali wadogo na wa kati zitatozwa kodi, jambo ambalo sasa hivi halifanywi kwa ufasaha.

Kuhusu matumizi kadhaa aliyofayanya ikiwa ni pamoja na kukata fedha za sherehe za uhuru na za wabunge, alisema hatua hiyo ilichukuliwa kwa kuwa aliingia madarakani bajeti ya mwaka 2015/16 ikiwa imeshapita.

“Ikumbukwe alipoingia madarakani bajeti ilishasomwa, kwa hiyo hivi vitu ambavyo siyo lazima kama hizo sherehe za uhuru, za wabunge, semina elekezi fedha zilikuwa zimeshatengwa kwa shughuli hiyo, akaona ni vyema kupeleka kwenye masuala muhimu zaidi,” alisema na kuongeza:

“Hiyo ilikuwa ni re-allocation tu ya kawaida na kwa sababu makusanyo ni makubwa anayatumia kutekeleza baadhi ya ahadi zake ambazo hazikuwa kwenye bajeti,” alisema.

Mhadhiri wa UDSM na mtaalam wa uchumi, Dk. Haji Semboja, alisema anachofanya Rais Magufuli sasa kiliwahi kufanywa na marais waliomtangulia.

Alisema tofauti yake na marais hao ni kuwa, Rais Magufuli anatumia kutokana na kile alichokikusanya, tofauti na watangulizi wake waliokuwa wanatumia kutoka katika kile walichokopa.

“Unashona nguo kulingana na ukubwa wa kitambaa chako, mfumo huu ni mzuri kwa kuwa anatumia kutoka kile alichokusanya na nchi haitakuwa na deni kubwa miaka ya mbele,” alisema.

Dk. Semboja alisema mfumo wa kutumia fedha katika sekta mbalimbali ni mzuri kwa sababu, mtu anatakiwa kutumia kulingana na kile alichonacho na siyo asichonacho.

Naye Mkuu wa Idara ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Jehovaness Aikaeli, alisema ni utaratibu mzuri ulionzishwa kwa kuwa unasaidia kuziba mashimo yaliyokuwapo tangu awali.

Alisema haina haja kwa serikali kuweka akiba wakati wananchi bado wanahitaji kupata mahitaji muhimu kama vile dawa hospitalini na madawati katika shule.

“Haina haja ya kuweka akiba, kama vile alivyofanya fedha za sherehe za uhuru zielekezwe katika ujenzi wa barabara ni sahihi, utaratibu huu uendelee na usiishie njiani,” alisema.

Dk. Aikaeli alisema katika nchi yoyote duniani kanuni kubwa ni kutegemea kodi katika kuendeshea nchi, hivyo Rais Magufuli anatakiwa kuendelea kuziba mianya ya upotevu wa kodi.

Mhadhiri wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) cha Dar es Salaam, Dk. Bill Kiwia, alisema ni mfumo mzuri aliouanzisha Rais John Magufuli katika kuinua uchumi wa nchi.

Hata hivyo, alisema serikali inapaswa kutotegemea makusanyo ya kodi pekee katika bajeti yake, bali iangalie vyanzo vingine vya mapato, kwani kwa kutokufanya hivyo kutaua sekta binafsi.

Alisema serikali pia inapaswa kuangalia makusanyo katika vitalu vya madini na gesi, ushuru na tozo.

Alisema pia serikali inaweza kutumia njia ya kukopa fedha kutoka mataifa ya nje na kuzielekeza katika sekta za maendeleo.

“Serikali isitegemee sana makusanyo ya kodi katika kutekelezea bajeti yake, inaweza kuangalia vyanzo vingine vya mapato, lakini ni mfumo mzuri aliouanzisha Rais, utasaidia kukuza uchumi wa nchi,” alisema Dk. Kiwia.

Aliongeza kuwa, kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia (WB) ya Julai, 2015, uwiano wa wigo wa kodi ni asilimia 12.

Alisema Tanzania inahitaji kukusanya kodi zaidi ili iweze kulipia gharama mbalimbali za uendeshaji serikali na kwamba kupungua kwa misaada na vikwazo katika mikopo ndio kunapelekea umuhimu wa kukusanya kodi zaidi.

Alisemal akini ni muhimu ukusanyaji huo wa kodi usidhoofishe sekta binafsi.

Akizungumzia operesheni ya kukusanya kodi inayoendeshwa na TRA, Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Umma wa mamlaka hiyo, Richard Kayombo, alisema lengo lake ni kusajili wafanyabiashara ambao hawajasajiliwa na kukagua ambao wanapaswa kutumia mashine za EFDs lakini hawazitumii.

Alisema operesheni hiyo ni ya kawaida na inafanyika nchi nzima na kuwa wale ambao watakutwa wanafanyabiashara bila kusajiliwa watawashauri kufanya hivyo ili kukidhi matakwa ya sheria.

MAKUSANYO YA SERIKALI
Desemba mwaka jana, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilikusanya Sh. trilioni 1.3 Novemba na Desemba makusanyo hayo yalipanda na kufikia Sh. trilioni 1.4, huku sehemu ya fedha za miezi hiyo pamoja na mambo mengine zikitumika kuanzisha mpango wa elimu bure.

Januari kiasi hicho kilishuka mpaka Sh. trilioni 1.06 na malngo ya Februari ni Sh. 1.03.

MATUMIZI YA FEBRUARI
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile, alieleza kuwa kwa Februari, mwaka huu, serikali imeweza kutumia zaidi ya Sh. trilioni moja katika miradi na sekta mbalimbali.

Baadhi ya sehemu ya fedha hizo, Sh. bilioni 18.7 zimepekwa kutekeleza mpango wa elimu bure, Sh.bilioni 1.65 mafunzo kwa vitendo katika vyuo 35, Sh. milioni 29.1 kununulia vifaa, Sh. milioni 1.49 zilitumika kulipa posho, Sh. milioni 402.1 zilitumika kulipia posho kwa wanafunzi.

Pia Sh. bilioni 573.2 zilitumika kulipa mishahara kwa watumishi wa umma, Sh. bilioni 842.1 zililipa deni la taifa, Sh. bilioni 81.23 kulipa deni la mifuko ya hifadhi ya jamii, Sh. bilioni 166.1 zilitumika katika miradi ya maendeleo, Sh. bilioni 2.078 zilipelekwa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).

Sh. bilioni 7.115 katika sekta ya maji na Sh. bilioni 58.168 sekta ya barabara, Sh. bilioni 40.73 sekta ya ujenzi na Sh. bilioni 16.46 zilipelekwa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Sh. bilioni 20.1 sekta ya umeme, Sh. bilioni 2.034 sekta ya reli na Sh. bilioni 12.3 sekta ya mahakama.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Hivi kama toka huko nyuma mambo yangekuwa hivi uwazi na ukweli na mikakati na mipangilio. Si tungendelea. Na kodi ingekuswanywa vizuri kama sasa. Tungendelea kama nchi zilizoendelea zinajiendesha kwa kukusanya kodi tu. Na uchumi wa maliasilia pato lake wanalifadhi hapo hapo. Sasa hawa wengine waliopita wao kazi kuwafwata wale wakina kajamba nani kama mama ntilie eti ndio walipe kodi. Kutwa asikali wa jiji kufukuzana na mama ntilie na machinga. Wale mapapa hahahaaa hawawagusi kwa kodi. Wale wanawawakilishia mijihela kwenye mufuko yao na zikija za misaada hapo hapo ufisadi mifukoni. Da hawa viongozi waliopita ni shidaaaa tupu tu. Tena michoshooo