Obasanjo ambaye aliongoza ujumbe wa Jumuiya ya Madola uliokuwa ukiangalia vigezo vya kidemokrasia katika uchaguzi uliokamilika nchini Uganda wiki iliyopita, amewashauri viongozi waUganda kujiepusha na makabiliano na migongano baina yao.
Obasanjo alikemea jinsi Serikali inavyotumia nguvu kuwadhibiti wapinzani na kutaka uhuru wa kujieleza uheshimiwe.
‘’Dosari zilizotokea katika Uchaguzi Mkuu zimeathiri matokeo na kutilia shaka ukweli, haki na uwazi wa uchaguzi huo,’’ alisema kiongozi huyo wa zamani wa Nigeria.
Pia, alisisitiza tofauti kati ya Serikali na upinzani zinahitajika kusuluhiswa kupitia mazugumzo na siyo vinginevyo.
‘’Vyombo vya usalama vinatakiwa kuacha tabia ya kukamata viongozi wa siasa na badala yake walinde usalama kwani wanasababisha uhasama,’’ alisema.
Alisema uhuru wa kujieleza na kuwasiliana na umma, kila kiongozi sharti ulindwe na kama kuna vizuizi dhidi ya kiongozi yeyote lazima viondolewe.
Kiongozi wa kambi ya upinzani, Dk Kiiza Besigye ambaye aligombea urais kwa mara ya nne bila mafanikio, alikamatwa juzi na polisi alipokuwa akielekea ofisi za Tume ya Uchaguzi ya Uganda kuulizia matokeo rasmi.
Besigye alikuwa kwenye kizuizi cha nyumbani tangu wiki iliyopita baada ya polisi kumtuhumu kupanga kujitangazia matokeo.
Pia, wawakilishi wa Umoja wa Ulaya (EU) ambao walikuwapo nchini humo kusimamia uchaguzi huo, walisema hakukuwapo na uwazi katika utendaji wa tume hiyo.
Walisema, kucheleweshwa ufikishaji wa karatasi za kupigia kura katika vituo vya uchaguzi hususan Kampala na vitongoji vyake, ni dosari iliyojitokeza. Jambo hilo lilisababisha uchaguzi huo kwa kiwango kikubwa kutokuwa huru. Vilevile wawakilishi hao walisema polisi walitumia nguvu kuwakamata wapinzani.
Museveni kuapishwa Mei
Naibu Msemaji wa Polisi, Polly Namaye amesema idadi ya polisi waliopelekwa kulinda usalama mjini Kampala haitapunguzwa mpaka Mei rais mteule atakapoapishwa.
Museveni alishinda uchaguzi huo baada ya kuongoza kwa asilimia 62.8 ya kura zilizohesabiwa, akifuatiwa Dk Besigye kwa asilimia 32.7.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment