Raia wa Uganda wakiwa kwenye mkutano wa kampeni za Uchaguzi Mkuu utakaofanyika kesho . Picha na AFP
Ingawa Rais Yoweri Museveni anapewa nafasi kubwa ya kuendelea kusalia madarakani, anakabiliwa na kibarua kigumu cha kuibuka kidedea kwa mara nyingine.
Katika majukwaa ya kampeni, Rais Museveni amekuwa akisisitiza kudumisha umoja nchini humo, mshikamano na azma ya chama chake cha NRA kuendelea kuwapigania wanyonge.
Kibarua ambacho kinamkabili Museveni ni kukabiliana na upinzani kutoka kwa wagombea wa urais akiwamo aliyekuwa waziri wake mkuu, Amama Mbabazi na kiongozi wa kambi ya upinzani, Dk Kiiza Besigye.
Rais Museveni ametoa ahadi nyingi kwenye mikutano yake ya kampeni ikiwamo ya kuimarisha miundombinu ya barabara kwa kuweka lami.
Kiongozi huyo aliyeingia madarakani tangu 1986 akitokea msituni ana matumaini kufanya vizuri katika uchaguzi huo.
Akiwa na umri wa miaka 71 na kati ya viongozi waliokaa madarakani kwa muda mrefu zaidi Afrika, Museveni anashutumiwa kwa kuendelea kukandamiza wapinzani wake kwa kutumia vyombo vya dola.
Museveni alipaswa awe amemaliza muhula wake wa utawala mwaka 2006, lakini mwaka 2005 Katiba ya Uganda ilibadilishwa na kuondoa ukomo wa mihula ya rais.
Rais Museveni alikabiliwa na tuhuma kutoka nchi za Magharibi kwa ukiukaji wa haki za binadamu. Hata hivyo, kiongozi huyo aliyajibu mataifa hayo akiyaambia yasidiriki kuingilia masuala ya ndani ya nchi yake.
Kizza Besigye, ambaye wakati mmoja alikuwa rafiki mkuu wa Rais Museveni, alipambana naye kwenye Uchaguzi Mkuu mara tatu kwa tiketi ya chama cha Forum for Democratic Change (FDC) bila mafanikio.
Besigye anasema uchaguzi wa mwaka huu ni karata muhimu kwa raia wa Uganda kuchagua mabadiliko ya kweli.
Anajivunia zaidi huruma ya wapigakura kutokana na kuandamwa mara kwa mara na vyombo vya dola.
Amama Mbabazi, pia alikuwa rafiki wa karibu wa Rais Museveni kabla ya kutangaza kuwania urais.
Alikuwa waziri mkuu wa Uganda kuanzia 2011-2014. Katika uchaguzi huo, anawania kama mgombea huru kupitia vuguvugu la Go Forward. Kuna wagombea wengine wanne ingawa hawatarajiwi kutoa ushindani mkubwa katika kinyang’anyiro hicho.
Kwa mujibu wa sheria za Uganda, rais huchaguliwa kuongoza nchi kwa muhula wa miaka mitano.
Mgombea huhitajika kupata asilimia 50 + 1 ya kura zilizopigwa ndipo atangazwe mshindi. Iwapo hilo halitatokea basi italazimika kuingia katika duru ya pili kati ya aliyeongoza na mgombea wa pili katika kipindi cha siku 30.
Bunge la nchi hiyo lina viti 418, kufuatia kuundwa kwa maeneo 43 mapya mwaka 2015.
Kampeni hizo kwa wagombea hao, zimekuwa zikitawaliwa kwa kutoa ahadi za kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira, ufisadi na kuboresha huduma za Serikali kwa wananchi.
Suala ya mafuta pia limeangaziwa kwenye mikutano ya kampeni. Taifa hilo liligundua mafuta mwaka 2006.
Simu marufuku
Tume ya Taifa ya Uchaguzi Uganda imepiga marufuku wapiga kura, wasimamizi wa uchaguzi na waangalizi wa ndani na nje kutumia simu kwenye vituo vya kupigia kura.
Amri hiyo ya tume ilipingwa vikali na wanaharakati na wanasiasa wakisema siyo yake bali ni ya chama tawala na ina maana nyingine tofauti.
Mabomu
Juzi mabomu yalirindima wakati mgombea urais wa chama cha upinzani cha FDC nchini Uganda, Kizza Besigye alipokamatwa na kuzuiliwa kwa muda na maofisa wa polisi mjini Kampala.
Polisi walitoa sababu za kumkamata kiongozi huyo kwamba ni kushindwa kuwazuia wafuasi wake wasizibe barabara kutokana na uwingi wao.
Tuhuma nzito
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lilisema vitisho vya Serikali ya Uganda dhidi ya vyombo vya habari na wanaharakati vimeathiri uhuru wa kujieleza nchini humo.
Ripoti ya Human Rights Watch ilisema waandishi kadhaa walisimamishwa kazi kutokana na shinikizo la Serikali na kwamba vituo vya redio vilivyowahoji wanasiasa wa upinzani na kutoa maoni yanayokipinga chama tawala, navyo vimetishwa.
Katika ripoti hiyo iliyopewa jina, ‘Wanyime watu taarifa’’ Human Rights Watch ilisema, uchaguzi wa haki unahitaji nafasi sawa kwa wagombea wote kunadi sera zao kwa wapigakura.
Mdahalo
Ilifanyika midahalo miwili ya wazi nchini ikiwakutanisha wagombea wa urais, lakini mdahalo wa kwanza Museveni alishindwa kutokea akisema ulikuwa ni mdahalo wa kitoto na pia alikuwa kwenye kampeni.
Akijibu maswali kwenye mjadala wa urais Kampala, alisema: “Tunapinga ukiukaji wa sheria, ndipo tuliunga mkono ICC, lakini haina maana ina ubaguzi
Rais huyo ambaye zamani alikuwa akiunga mkono Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu amekuwa katika mstari wa mbele kuikashifu na kutaka viongozi wa Afrika wajiondoe kushirikiana nayo.
Maoni ya Museveni yaliungwa mkono na mgombea urais kwa chama cha People’s Progressive Party, Abed Bwanika akisema Uganda ilitakiwa iwe imeshajiondoa ICC kitambo.
Kwa upande wake, Dk Besigye alisema anashangazwa na hatua ya Museveni kuchaguliwa kuwa msuluhishi wa mgogoro wa nchiniBurundi.
Besigye alitamba kuwa ana uhakika kumshinda Museveni kwenye uchaguzi huo na kusisitiza kuwa yeye hawezi kutawala kimila.
Mapambano ya vitisho
“Tunachoshughulika nacho siyo uchaguzi,” alisema Profesa wa sheria Oloka Onyango kutoka Chuo Kikuu cha Makerere, na kuongeza kuwa mapambano ya kisiasa yanafanyika kupitia vitisho kuliko kwenye sanduku la kupigia kura.
Alisema kinachotakiwa ni uwapo wa demokrasia kwa wananchi kuchagua kiongozi wanayemtaka.
Imeandaliwa na Hussein Issa kwa msaada wa mitandao mbalimbali ya habari
MWANANCHI
1 comment:
Fake elections washapanga Museveni anashinda kwa kura ngapi
Post a Comment