ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 29, 2016

Naibu Spika akaangwa kwa mafuta yake

By Godfrey Kahango na Raymond Kaminyoge, Mwananchi

Mbeya/Dar. Naibu Spika, Dk Tulia Ackson amesema kazi za mbunge si kupiga kelele bungeni ili aonekane kwenye luninga, bali ni ushiriki wake katika kazi za maendeleo kwenye jimbo lake.

Lakini kauli hiyo imepingwa vikali na baadhi ya wabunge wa upinzani ambao wamesema ukosefu wa uzoefu ndiyo uliomfanya atamke hayo.

Dk Ackson ambaye ameingia kwa mara ya kwanza kwenye chombo hicho kwa kuteuliwa na rais na baadaye kushinda uchaguzi wa naibu spika baada ya kupitishwa na CCM, alitoa kauli hiyo juzi usiku jijini Mbeya wakati wa hafla ya kumpongeza kwa kuchaguliwa kushika nafasi hiyo iliyoandaliwa na wadau wa maendeleo wa mikoa ya Mbeya na Songwe.

Aliwataka wananchi kuacha kuwafurahia wabunge wanaozungumza kwenye Bunge bila kuonyesha vitendo kwenye majimbo yao.

Alisema hata kama mbunge hapati fursa ya kuzungumza chochote bungeni, hilo lisiwape shida badala yake, waangalie anavyofanya kazi kwenye jimbo.

“Angalieni wabunge wenu wanafanya nini majimboni ukilinganisha na kuonekana kwenye TV, na pia pimeni mambo anayozungumza kama yana faida kwa jamii au la,” alisema.

Wabunge wamjibu

Lakini kauli yake ilijibiwa vikali na wabunge. Mbunge wa Kaliua (CUF), Magdalena Sakaya alisema kauli ya Naibu Spika imemkera na ni hatari kutolewa na kiongozi kama yeye.

Sakaya, ambaye pia Naibu Katibu Mkuu wa CUF, alisema Dk Ackson anafahamu kwamba kazi za mbunge ni kuisimamia na kuishauri Serikali na kutunga sheria na wanatakiwa kuisimamia Serikali ili kuhakikisha bajeti iliyopitishwa inatekelezwa.

“Utafanyaje kazi hizo bila kuzungumza bungeni. Anataka kutueleza kwamba tunauza sura kwenye televisheni? Tunamsubiri huyo amenikasirisha sana,” alisema.

Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa alisema: “Naibu Spika ni mbunge wa kuteuliwa. Hajawahi kuchaguliwa kuwakilisha wananchi ndiyo maana anatoa ujumbe unaopotosha wananchi.”

Mbunge wa viti maalumu (Chadema), Suzan Lyimo alisema wabunge wanatakiwa kuzungumza wakati wowote ili kuibana Serikali, lakini vikao vikiisha wanakwenda majimboni.

Mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Suleiman Said Bungara alisema moja ya kazi za wabunge ni kuisimamia na kuishauri Serikali.

3 comments:

Anonymous said...

Huyu dada yupo sahihi kabisa na ndio maana wahusika wamekasirika kwa kuambiwa ukweli. Kuna tofauti kati ya kuzungumnza na kupiga kelele . Wabunge wengi wa upizani Tanzania ni watu wasiojua wajibu wao kama wabunge wanapokuwepo pale bungeni.Hata hivyo ni wabunge wachache mno kutoka upizani na chama tawala waliotafuta ubunge wapo kwenye nyazifa hizo kwa maslai ya wananchi waliyowaweka madarakani. Wengi wao wapo pale kwa maslai yao binafsi zaidi na vyama vyao vya siasa.

Anonymous said...

Hapo juu unashindwa jua nini maana ya vyombo vya habari. Bila wabunge kupiga kelele na kuonekana kwenye luninga ungeona au kusikia wapi wizi mkubwa wa pesa zilizoibwa na viongozi. Ungejua vipi kwamba magufuli ni mchapa kazi. Kazi kwa vitendo ni muhimu lakini usipoangalia wabunge watajenga barabara na kuwapa pesa za wizi watu ili waingie bungeni. Huyo mama atajifunza tu, taratibu ndio mwendo mwache alopoke wabishane nae atajirekebisha na kujua umuhimu wa vyombo vya habari. Hata yeye tumemjua habari zake kwa kelele zilizopigwa na wapinzani na si vinginevyo. Aseme ameifanyia nini CCm mpaka apewe nafasi kubwa kama hiyo maaana kila mtu anajua alipewa. Maana JPM mwenyewe yuko hoi kwa madudu yalioachwa na CCM. Hatutaki kufika walikofika Zimbabwe. Utawala wa kifalme ulishaingia bila kelele bungeni tungeendelea kuwa na wabunge wanaolala bungeni.

Anonymous said...

Mtoa mada hapo naona kuna tatizo ndani yako! nasema hivyo kwanini? Huo ukweli unaousema uko wapi hapo. Tunachojua wabunge wote sio CCM wala yeyote upinzani!
Wako wanaendekeza kukaa Dododm na maskani yaoe wengi ni Dar sasa ni saa ngapi wanachukua data na habari za wapiga kura wao hilo ni kitendawili na ndio maana mara nyingi kwenye vikao vya bunge imekuwa ni malumbano kwa kuwa wabunge hawapeleki taarifa kamili toka kwa majimbo yao bali kuletewa au kubuni wakati kinaelewe3ka kule kwa wananchi wanja tatizo kadha bwa kadha!