ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, February 25, 2016

Serikali yapokea vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi bilioni kumi.


Waziri mkuu Mhe Kassim Majaliwa amesema Tanzania itapiga hatua kubwa za maendeleo iwapo serikali na sekta binafsi zitafanya kazi pamoja katika kuwahudumia wananchi.
Waziri mkuu Mhe Kassim Majaliwa ameyasema hayo jijini dar es salaam wakati akipokea msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 10 kutoka kwa umoja wa wazalishaji wa vinywaji baridi nchini, na kutoa changamoto kwa wazalishaji wengine kuiga mfano huo.
Vifaa tiba hivyo vimetolewa na makampuni ya Cocacola kwanza, Bonite Bottlers, Nyanza Bottlers, Said Salum Bakhresa inayozalisha vinywaji vya Azam, na SBC Tanzania LTD wazalishaji wa soda aina ya Pepsi.

Waziri mkuu ambaye alikagua shehena ya vifaa tiba hivyo vya kisasa, alisema vifaa hivyo vimepokelewa wakati muafaka wakati serikali inajizatiti kuboresha huduma za afya, na kusisitiza kuwa vitasambazwa kwenye maeneo yote muhimu vinakohitajika sana.

Mapema mwakilishi wa umoja wa wazalishaji wa vinywaji baridi ambaye ni mkurugenzi mkuu wa Coca cola kwanza Bw. Basil Gadzios alisema pamoja na kukabidhi msaada wa vifaa tiba hivyo, watatoa wataalamu wa kutoa mafunzo ya matumizi na ukarabati wa vifaa tiba hivyo.

Akitoa shukrani mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya bohari ya madawa -MSD Prof. Idris Mtulia amewapongeza wazalishaji wa vinywaji baridi kwa kutoa vifaa tiba vyenye ubora wa kuweza kutumika katika hospitali zozote duniani.

Wakati huohuo kundi la wafanyakazi wa kampuni Tarmal wanaofanyakazi katika kampuni ya PSI walisimamisha msafara wa magari wa waziri mkuu Kassim Majaliwa uliokuwa ukitoka katika hafla ya kukabidhiwa vifaa tiba, na kumweleza manyanyaso wanayopata kutoka kwa mwajiri wao, huku waziri mkuu akiwataka waendelee na kazi zao na kuwaahidi waziri anayeshughulikia na ajira Mhe Jenister Mhagama atakwenda kukutana nao ili awasikilize kwa kina na kuzitafutia ufumbuzi kero zao. Source:ITV

No comments: