ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, February 20, 2016

SIMULIZI YA BINTI WA KICHINA, WA PILI KITAIFA MITIHANI YA KIDATO CHA NNE


Saa 6.40 mchana wa Februari 18, saa chache baada ya matokeo ya mitihani ya kidato cha nne kutangazwa, nakutana na mwanafunzi aliyeshika namba mbili kitaifa Congcong Wang.
Ni binti wa Kichina ambaye hakuficha kunionyesha tabasamu, bashasha baada ya kutambulishwa na walimu wake kuwa mimi ni mwandishi wa habari na nimefika shuleni (Feza Girls) kwa lengo la kuzungumza naye.
Nilishangaa baada ya mwanafunzi huyu kunisalimia kwa Kiswahili kisha kunipa pole ya kazi na safari ndefu ya kumfuata shuleni hapo.
“Shikamoo mama. Naitwa Congcong Wang,” alisema binti huyu mcheshi. Salamu hiyo ilinipa hamu ya kutaka kujua alijifunzia wapi Kiswahili, ilhali kwa mwonekano ni Mchina halisi.
Congcong alifika nchini mwaka 2006 akiwa na wazazi wake ambao wanafanya hapa nchini na alianza masomo katika shule hiyo akiwa darasa la kwanza.
Anasema mwanzoni alipata wakati mgumu hasa baada ya kufahamishwa kuwa anatakiwa aifahamu vyema lugha ya Kiswahili kwa sababu endapo atafeli somo hilo, atalazimika kurudia mwaka.
Anaeleza kuwa wakati huo hakuwa akifahamu lugha yoyote zaidi ya lugha yake ya asili, Kichina, hivyo alilazimika kusoma lugha tatu kwa wakati mmoja; Kiswahili, Kiingereza na Kituruki.
Anasema matokeo yake ya kumaliza elimu ya msingi shuleni hapo hayakuwa mazuri, kwa sababu wakati huo lugha zote zilizokuwa zinatumika kufundishia hakuwa anazielewa vizuri.
“Wanafunzi, walimu ni nguzo kuu katika kutambua lugha hizi kwa sababu kila niliyekuwa namtizama usoni alikuwa ananichekea, wakati mwingine nilitamani kuwauliza mnacheka nini, lakini sikuwa nafahamu, kizuri zaidi walipobaini napata tabu kuzungumza Kiswahili walitumia muda mwingi kunitajia maneno kwa lugha ya Kiingereza ambayo niliyaelewa haraka.
“Na kubadili katika Kiswahili, nilikuwa na marafiki wengi kwa sababu nilikuwa nakosea sana na wao wanacheka nikikosea, lakini walitumia muda mwingi kunifundisha kwa sababu ya utulivu uliopo shuleni hapa, ”anasema.

Kuhusu Tanzania
Congcong anasema kitu anachokumbuka na kukifurahia maishani mwake ni kufika Tanzania na kujionea kitu tofauti na kile alichokuwa anakisikia na kuona katika mitandao akiwa kwao.
Binti huyo aliyetokea katika Mkoa wa Jilin, uliopo katika Jiji la Chang Chun anasema akiwa kwao alisikia na kuona katika mitandao hali duni ya nchi za Afrika ikiwamo Tanzania.
Anakumbuka sifa kuu ya nchi za Afrika ilikuwa ni ubaya wa barabara, viwanja vya ndege, hakuna maduka makubwa, kwa ujumla ilijengeka picha kwamba maisha ni ya kuhangaika sana.
“Siku ya kwanza kufika Tanzania mwaka 2006, nilishangaa sana, baada ya kuona uwanja wa ndege mkubwa na wa kuvutia, majumba ya kifahari na maghorofa, maduka makubwa, hoteli zinazopika vyakula vya kila aina hadi vya kwetu, barabara nzuri hasa katikati ya mji, nilishangaa na kufurahi, ”anasema.
Anasema aliposikia anaongozana na wazazi wake kuja nchini alijiandaa kukutana hali mbaya ya watu watakaokuwa wamewazunguka, lakini badala yake kila alipopita alikutana na watu wenye furaha na wengi wao wakimwambia “Mambo”.

Anapenda kuishi wapi nchini?
Congcong anasema furaha yake ni kuishi popote nchini, lakini anafurahi zaidi akiwa Jijini Arusha kutokana na hali ya hewa ya baridi inayofanana na ya kwao China.
Anasema licha ya kufurahishwa na hali ha hewa, akiwa huko anakumbuka alipoanzia safari yake ya kwenda kuuona mlima aliokuwa ana hamu ya kuuona tangu akiwa mdogo wa Kilimanjaro.
“Tukiwa na wazazi wangu Arusha ndipo tulipoanza safari ya kwenda kuuona Mlima Kilimanjaro.
Nilipofika, nilitaka kulia kwa furaha ni kitu nilichokuwa natamani kiwe cha kwanza nilipofika tu hapa nchini, ” anasema Congcong.
Anasema anaipenda Tanzania kuliko nchi nyingi alizokwenda, kwa sababu ya watu wake ni wakarimu, wapo karibu nao, wanajali tamaduni zao, ikiwamo mavazi yao kama ushungi, vilemba, vitenge na nguo ndefu hadi miguuni.

Mama yake anamzungumziaje?
Ukiwaona wakiwa wameongozana na mama yake aitwae Wanhong Wang, utapata tabu kumfahamu nani ni mama na nani mtoto kati yao kutokana na kulingana, unaweza kubabaika zaidi kwani Congcong anaonekana kuwa ni mkubwa. Wanhong hawezi kuzungumza Kiswahili wala Kiingereza, hivyo binti aligeuka mkalimani pale nilipotaka kupata maoni yake.
Mama yake anasema binti yake ana nidhamu ya shule tangu akiwa mdogo, hakupenda kukaa kimya kwa kila alichokisikia au kukiona na wakati mwingine hufanya juhudi binafsi kujua kitu ambacho anaamini wakubwa au walio karibu naye wameshindwa kumuelewesha.
Anasema mara nyingi binti yake amekuwa mwalimu kwao, hasa hapa nchini kutokana na kufahamu vitu vingi kuwashinda.
“Najivunia kuwa naye, ni kiongozi wetu, hasa hapa Tanzania. Anafahamu vitu vingi, ni mdadisi, anapenda kusoma vitu vingi kwa wakati mmoja,” anasema Wanhong.
Congcong huku akicheka anaeleza ni kwa nini mama yake anaonekana mdogo kuliko yeye: “Baba yangu Wang Dacheng, ambaye ni mhandisi katika kampuni ya Spring City Auto Glass ni mkubwa kama mimi ndiyo maana natofautiana na mama hata kwa kimo,” anasema.

No comments: