Mkuu wa Wilaya mpya ya Buhigwe, Mary Tesha akiwasilisha taarifa kuhusu kero na changamoto mbalimbali kuhusu sekta ya nishati, zinazowakabili wananchi wake mbele ya Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani (wa pili kutoka kulia), alipofanya ziara wilayani humo hivi karibuni.
Na Veronica Simba - Buhigwe
Na Veronica Simba - Buhigwe
Naibu Waziri wa
Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani amekataa kupokea Taarifa ya utendaji kazi
kwa Wilaya mpya ya Buhigwe mkoani Kigoma, kutoka kwa Meneja wa Shirika la Umeme
Tanzania (Tanesco) wa Wilaya hiyo, Ntungwa Njegelo.
Dk Kalemani alikataa
kupokea taarifa hiyo juzi Februari 19, alipokutana na Uongozi wa Wilaya hiyo
mpya, kwenye Ofisi ya muda iliyopo wilayani humo, akiwa pamoja na watendaji
mbalimbali kutoka wizarani, Tanesco na Wakala wa Umeme Vijijini (REA)
Akizungumzia sababu
za kukataa kupokea taarifa hiyo, Naibu Waziri alisema haijitoshelezi kwani
haijaeleza kwa kina masuala mbalimbali muhimu ya kiutendaji katika wilaya hiyo.
“Kwa mfano, taarifa
hii inaeleza vijiji 12 vimepata umeme lakini haielezi idadi hiyo ni kati ya
vijiji vingapi. Pia, haielezi ni asilimia ngapi ya umeme imepatikana. Taarifa
hii haiwezi kunisaidia maana nataka kutatua kero hivyo ni lazima nijue ukubwa
wa tatizo.”
Kufuatia hatua hiyo,
Naibu Waziri Kalemani alimwagiza Meneja huyo aandae taarifa mpya, yenye maelezo
ya kina kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme hususani mradi wa REA (Umeme
Vijijini) Awamu ya pili na kuiwasilisha kwake Jumatatu, Februari 22 mwaka huu.
Aidha, Dk Kalemani
alimwagiza Meneja huyo kufuatilia na kufanyia kazi malalamiko ya wananchi
katika eneo lake, kuhusu kuwepo na mashimo yaliyochimbwa kwa ajili ya kusimika
nguzo za umeme katika mashamba yao lakini yameachwa wazi kwa muda mrefu pasipo
zoezi hilo kufanyika hivyo kuwazuia kuendelea na shughuli zao za kilimo.
Awali, akiwasilisha
taarifa kwa niaba ya wananchi wake kuhusu kero na changamoto mbalimbali
zinazowakabili kuhusiana na sekta ya nishati, Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Mary
Tesha alimwomba Naibu Waziri kusaidia ili mashimo yaliyochimbwa katika baadhi
ya vijiji kwa ahadi ya kusimika nguzo za umeme, yafanyiwe kazi mapema ili
wananchi waendelee na shughuli za kilimo katika mashamba yao.
Vilevile, Dk Kalemani
alisema pamoja na mapungufu kadhaa, Tanesco wamejitahidi kufanya kazi nzuri ya
kuwaunganishia wananchi wa vijijini umeme kwa kushirikiana na Wakala wa Nishati
Vijijini (REA).
Alimpongeza
Mkandarasi mzalendo anayeunganisha umeme wa REA Awamu ya pili mkoani Kigoma,
Wilbroad Mutabuzi kupitia kampuni yake ya JV State Grid Electrical and
Trchnical Works Ltd kwa kazi nzuri anayoifanya.
“Kuna baadhi ya
maeneo tumekutana na matatizo ya wakandarasi kufanya kazi chini ya kiwango
hivyo kuturudisha nyuma. Huyu Mkandarazi mzawa anayefanya kazi hiyo hapa Kigoma
anajitahidi sana na namtaka aendelee hivyo.”
Alisema ameagiza
zoezi la kuunganisha umeme wa REA Awamu ya pili likamilike ifikapo Mwezi Aprili
mwishoni, hivyo wale wote waliopangwa kuunganishiwa umeme katika awamu hiyo,
wanapaswa kuwa wamepatiwa huduma hiyo ndani wa kipindi hicho.
Naibu Waziri Kalemani
yupo katika ziara ya kikazi kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa chini ya
wizara yake. Alianza ziara hiyo mkoani Tabora, sasa yupo Kigoma na anatarajia
kumalizia ziara hiyo ya siku 10 mkoani Geita.
No comments:
Post a Comment