ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, February 25, 2016

Spika Kificho apata wapinzani Zanzibar.

Hatimaye Spika Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW), Pandu Ameir Kificho, amepata wapinzani katika nafasi hiyo aliyoiongoza kwa takriban miaka 25 mfululizo.

Uchunguzi wa Nipashe visiwani humu umebaini kuwa, harakati za chini kwa chini zimeanza kufanyika kuhusiana na nafasi hiyo kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa marudio Zanzibar Machi 20, mwaka huu.

Miongoni mwa watu wanaotajwa kujipanga kuwania nafasi hiyo baada ya kukamilika kwa uchaguzi mkuu wa marudio ni Mrajisi Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Abdallah Waziri, Wakili wa Mahakama Kuu Zanzibar, Omar Mmadi Mwarabu na aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mohamoud Mohamed Mussa.

Kwa upande wake, Waziri alisema kuwa ameombwa na watu mbalimbali kuwania wadhifa huo wakiwamo Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Zanzibar.

Hata hivyo, alisema baada ya kupokea maombi hayo, bado anatafakari kabla ya kuamua kugombea nafasi hiyo nyeti.

“Nimepokea maombi kutoka kwa wanasiasa wazito na UVCCM wakinitaka kugombea nafasi ya Spika, Bado natafakari na wakati ukifika nitatoa msimamo wangu,” alisisitiza Waziri ambaye ameibua mjadala mkubwa katika siasa za Zanzibar.

Mwanasheria Mwarabu alisema tangu kuvunjwa kwa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Agosti 13, mwaka jana, kumekuwapo na wimbi la kumtaka kuwania wadhifa huo kutoka kwa watu mbalimbali wakiwamo wanataaluma wezake visiwani humu.

“Nimepokea maombi yao na ninaendelea kuyafanyia kazi kabla ya kuamua baada ya wakati kufika najua Spika nafasi nyeti katika mihimili mitatu ya dola,” alisema.

Lakini Mahamoud kwa upande wake, alisema atagombea wadhifa huo iwapo Spika Kificho atasema hatogombea nafasi hiyo mwaka huu.

Alisema hawezi kushindana na kiongozi aliyemfundisha kazi akiwa Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi katika kipindi kilichopita.

“Maji hayapandi mlima, kama Spika Kificho atasema anagombea tena, siwezi kujitokeza kumpinga kutokana na mila na desturi na si ungwana mwanafuzi kupingana na mwalimu wake,” alisisitiza Mahamoud.

Hata hivyo, alisema uwezo wa kuliongoza Baraza la Wawakilishi, anao kutokana na uzoefu alioupata akiwa Mwenyekiti wa Baraza hilo na Mwakilishi wa Jimbo la Kikwajuni.

Akizungumzia suala hilo, Spika Kificho alisema hajawahi kuomba wadhifa huo bali amekuwa akiombwa na Wajumbe wa Baraza na wanasiasa kugombea.

“Siku zote mie naombwa kugombea sijawahi kuomba mwenyewe bila ya kuombwa na wenzangu katika kipindi chote cha uongozi wangu,” alisisitiza Spika Kificho.

Hata hivyo, alisema kama yatatokea maombi ya kumtaka kugombea tena wadhifa huo kutoka kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, atatafakari kabla ya kuamua kuwania nafasi hiyo.

Alisema kazi ya kuongoza BLW ni nzito na inahitaji busara na hekima kutokana na kukua kwa demokrasia tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi Zanzibar mwaka 1995.

Aidha, alisema kitendo cha Chama cha Wananchi (CUF) kususia uchaguzi wa marudio Zanzibar, ni pigo kwa sababu kitarudisha nyuma mafanikio yaliyokuwa yamepatikana katika kuimarisha demokrasia.
CHANZO: NIPASHE

No comments: