JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
TAMKO KUHUSU MWENENDO WA UGONJWA WA KIPINDUPINDU NCHINI LILILOTOLEWA NA MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGWALLA (MB); NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, TAREHE 29 FEBRUARI 2016
Ndugu Waandishi wa Habari,
Taarifa hii ni mwendelezo wa utaratibu ambao Wizara yangu imejiwekea kila wiki wa kutoa taarifa kwa umma kuhusu hali ya kipindupindu nchini pamoja na kueleza juhudi mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa ili kukabiliana na hali hii. Hadi kufikia tarehe 28 Februari 2016,jumla ya wagonjwa 16,825 wametolewa taarifa, na kati ya hao watu 258 wamepoteza maisha.
Takwimu za wiki iliyopita zinaonyesha kuwa kuanzia tarehe 22 hadi 28 Februari 2016, idadi yawagonjwa wapya walioripotiwa ni 473, na kati yao watu 9 walipoteza maisha yao. Takwimu hizi za idadi ya wagonjwa katika wiki hii, zinaonyesha kuwa idadi ya wagonjwa imepungua japo kwa kiasi kidogo sana (5%) ukilinganisha na wiki iliyopita ambapo wagonjwa 499 waliripotiwa. Katika wiki iliyoishia tarehe 21 Februari, Mkoa wa Iringa ndio uliokuwa ukiongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi zaidi. Kwa wiki hii idadi ya wagonjwa kwa mkoa huo imepungua kwa kiasi kikubwa sana japo idadi ya wagonjwa nchini kwa ujumla imeendelea kubakia kuwa juu.
Jumla ya Mikoa 12 nchini iliripoti wagonjwa katika kipindi cha juma moja lililopita ambapo mkoa wa Mara uliripoti idadi kubwa zaidi ya wagonjwa ambayo ni 125 (Rorya 47, Musoma Mjini 40, Tarime Vijijini 26, Musoma Vijijini 10, Butiama 2) ukifuatiwa na Dodoma 87(Chamwino 64, Mpwapwa 17 na Dodoma mjini 6), Iringa 64 (Iringa Vijijini 63, Mjini 1 ),Mwanza 59 (Ilemela 32, Ukerewe 19, Nyamagana 8) na Morogoro 44 (Morogoro Mjini 21, Kilosa 13, Ulanga 10). Wagonjwa waliripotiwa pia kutoka mikoa ya Mbeya 29, Dar Es Salaam 25, Arusha 18, Kigoma 8, Rukwa 6, Simiyu 6, na Singida 2.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Wizara bado inaendelea kukumbana na changamoto mbalimbali katika kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu. Vikosi kazi vya wataalamu kutoka wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wanaoendelea kuzuru maeneo mbalimbali wameendelea kuibua changamoto hizo na kuhakikisha zinafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo ili kuzuia ueneaji wa vimelea vya ugonjwa huu na kisha kuutokomeza kabisa.
Moja ya changamoto kubwa inayoendelea kujitokeza ni pale ambapo baadhi ya wataalamu wa afya wa ngazi mbalimbali pamoja na wanajamii wanapowaficha wagonjwa na hivyo kutoa taarifa ya wagonjwa wachache kuliko uhalisia. Madhara yanayoambatana na hili ni kutokuwepo kwa taarifa za kutosha zitakazoongoza juhudi za kuzuia ugonjwa kutoka katika maeneo ambayo wagonjwa hawakutolewa taarifa, na hivyo kuongeza hatari ya ugonjwa kuendelea kusambaa kimya kimya na baadae kusababisha wagonjwa wengi kujitokeza katika maeneo hayo kwa mara moja.
Wizara inaendelea kuzitaka mamlaka zinazohusika na jukumu la kutambua wagonjwa kushirikiana na kutoa taarifa sahihi kama inavyoelekezwa katika miongozo mbalimbali ya Wizara ikiwamo muongozo wa udhibiti wa magonjwa ya milipuko Tanzania wa mwaka 2011 “IDSR” na muongozo wa udhibiti wa ugonjwa wa kipindupindu toleo la tatu la mwaka 2015. Pia natoa wito kwa jamii kuwa pale wapatapo wagonjwa wawapeleke mapema katika vituo vyetu vya kutolea huduma ili wapatiwe matibabu sahihi na kutolewa taarifa.
Kwa kufanya hivyo taarifa za kutosha na sahihi zitakazosaidia kupambana na ugonjwa huu zitapatikana kwa wakati na hivyo kuwezesha kuutokomeza ugonjwa huu mapema. Tunatoa rai kwa viongozi hususani ngazi ya Mikoa na Wilaya kutokutoa kauli za kutaka kuwaadhibu watendaji na viongozi wa ngazi za chini kwa kigezo cha wagonjwa wa kipindupindu kuwepo katika maeneo yao kwani kwa kufanya hivyo wataongeza kasi ya kuficha wagonjwa na hivyo kukwamisha juhudi za kupambana na ugonjwa huu.
Aidha tunatoa wito kwa mikoa yote nchini kuhakikisha kuwa wanaimarisha vikao vya Kamati za Afya ya Msingi (PHC meetings) na kutumia taarifa zinazotokana na tathmini ya mwenendo wa ugonjwa huu katika maeneo yao ili ziwasaidie kupanga mbinu sahihi za kuudhibiti ugonjwa wa kipindupindu.
Ndugu waandishi wa habari,
Wizara ilituma timu ya wataalamu kwenda Mkoani Iringa ili kufanya tathmini na kuongeza nguvu ya kupambana na kuzuia ueneaji wa ugonjwa huu kwa wahanga wa mafuriko. Taarifa ya tathmini hiyo imeonyesha jinsi ambavyo jitihada mbalimbali zilizochukuliwa zinavyosaidia kuepusha madhara zaidi kwa binadamu walioathiriwa na mafuriko katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa na kuepusha ongezeko la wagonjwa wa kipindupindu katika Wilaya hiyo na maeneo jirani. Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na wadau mbali mbali itaendelea kutoa msaada wa kitaalamu kwa Mikoa na Halmashauri zote ili kusaidia juhudi zilizopo za kupambana na ugonjwa huu nchini.
Tunaendelea kuisihi jamii kuungana na halmashauri, mikoa pamoja na wizara katika juhudi za kupambana na kuenea kwa ugonjwa wa kipindupindu kwa kuzingatia yafuatayo:
kunywa maji yaliyo safi na salama
kuepuka kula chakula kilichoandaliwa katika mazingira yasiyo safi na salama
kunawa mikono kwa sabuni na maji safi
kutumia vyoo wakati wote na kutokujisaidia ovyo katika vyanzo vya maji vya mito, maziwa na mabwawa. Tunaelewa kwamba jambo hili lina changamoto kubwa, lakini tunaisihi Mikoa na Halmashauri kuhimiza na kusimamia ujenzi na matumizi ya vyoo bora katika maeneo yao kwa kuwashirikisha wananchi.
Kutotiririsha maji taka na vinyesi ili kuepuka uchafuzi wa vyanzo vya maji.
Pia wananchi wanahimizwa kuwahi mapema katika vituo vya kutolea huduma za afya mara waonapo dalili kuu za ugonjwa wa kipindupindu ambazo ni pamoja na kuanza ghafla kuharisha mfululizo kinyesi cha majimaji na kunako weza kuambatana na kutapika, kulegea, kusikia kiu, midomo kukauka, na kuishiwa nguvu. Mgonjwa anaweza kupoteza maisha endapo hatapata huduma yoyote ya tiba katika muda mfupi na hasa kutokana na kuishiwa maji.
Hitimisho
Wizara inaendelea kutoa rai kwa jamii, wataalamu na viongozi katika ngazi zote kwamba kila mmoja wetu atimize wajibu wake katika harakati za kuudhibiti ugonjwa wa Kipindupindu.
Aidha, kwa mara nyingine tena tunaendelea kuwashukuru wadau wote, yakiwemo Mashirika ya Kimataifa kwa mchango wao mkubwa katika jitihada za kupambana na magonjwa mbalimbali ikiwemo mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu. Aidha tunawashukuru na kuwapongeza watumishi wa afya katika ngazi mbali mbali kwa juhudi zao katika kupambana na ugonjwa huu. Pia tunawapongeza waandishi wa habari kwa kuendelea kuisaidia Serikali kuielimisha jamii jinsi ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa kipindupindu kwa kusambaza taarifa mbalimbali zinazotolewa na Wizara kwa ngazi zote zinazohusika na mapambano ya Kipindupindu.
Asanteni sana
No comments:
Post a Comment