Dar es Salaam. Ubalozi wa Norway nchini umetoa ufafanuzi kuwa balozi wake, Hanne-Marie Kaarstad hakutembelea wala kuzungumza na viongozi wa CUF Zanzibar, bali aliyefanya hivyo ni ofisa mmoja wa ubalozi ambaye alitembelea visiwa hivyo na kuwajulia hali viongozi wa vyama vya CUF na CCM.
Taarifa iliyotolewa jana na ofisa mwambata wa ubalozi huo anayeshughulikia masuala ya utawala na siasa, Victor Mlunde ilisema ofisa huyo ambaye hakutajwa jina, alitembelea Zanzibar mapema wiki hii na kuwajulia hali Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Vuai Ali Vuai pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Mazrui akiongozana na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano wa chama hicho cha upinzani, Ismail Jussa Ladhu.
Mlunde alisema katika taarifa hiyo kuwa mikutano ya namna hii ni sehemu ya shughuli za kawaida za kidiplomasia.
Alifafanua kuwa, “Balozi Kaarstad hajatembelea Zanzibar wala viongozi wa chama chochote wiki hii wala iliyopita. Ubalozi wa Ufalme wa Norway unapenda kukanusha hiyo habari kwa kuwa si sahihi.”
Taarifa hiyo ilikuwa inafafanua habari iliyochapishwa na gazeti hili jana ikisema balozi huyo ndiye aliyetembelea Zanzibar juzi na kufanya mazungumzo na viongozi hao wa CUF.
Kutokana na kujiridhisha kuwa balozi huyo hakutembelea CUF ila ni ofisa wake ambaye alikwenda katika vyama vyote viwili, Mwananchi linaomba radhi kwa usumbufu wowote uliojitokeza kutokana na upungufu wa habari hiyo.
No comments:
Post a Comment