ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, February 23, 2016

WAKALA WA VIPIMO (WMA) KUFANYA MSAKO WA MIZANI FEKI YA MADUKANI MKOANI ARUSHA

Wakala wa Vipimo (WMA), Mkoa wa Arusha unatarajia kuanza kufanya msako wa mizani zisizokuwa na ubora katika maduka ya mkoani Arusha zinazodaiwa kutumika kuwapunja wananchi.
Meneja wa WMA wa mkoa huo, Dunford Manzi amesema leo kuwa mizani hizo zinadaiwa kutengenezwa nchini India na China.
Amesema kabla ya kuanza msako huo, watatoa elimu kwa wananchi na wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa kutumia mizani zenye ubora.
Pia, amewataka wafanyabiashara wabadilishe mizani hizo na kuweka halisi kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Sheria ya Vipimo Sura 340 (19) inatutaka tufanye ukaguzi wa mara moja kwa mwaka, katika kipindi cha mwezi mmoja tulikagua mizani na mashine kwenye vituo vya mafuta tumebaini mizani zilizopo sokoni hazina ubora zinapaswa kuondolewa.
“Kwa kawaida mizani ikifanyiwa kazi kwa muda wa mwaka mmoja zinahitaji kukaguliwa,” amesema.
Amewataka wafanyabiashara kuitumia ofisi ya WMA kupata ushauri wa vipimo sahihi ili kuepuka kuwapa hasara wateja wao.Pia, amewataka wateja kukagua mizani kabla ya kununua bidhaa ili kujiridhisha na kuepuka kuibiwa.
Mkazi wa Kwamrombo, Zaidi Jonathani amesema wafanyabiashara wengi wanatumia mizani iliyorekebishwa kwa lengo la kujipatia faida kubwa isivyo halali kwani unaweza kupima bidhaa moja kwenye mizani mbili na ikakupa vipimo tofauti. “Wafanyabiashara wanakuwa na mizani halisi na iliyofanyiwa ujanja, lengo lao wakija watu wa vipimo wanaonyesha iliyokaguliwa,” amesema.
Muuza nyama katika Soko la Kilombero, Loishiye Mollel amesema mizani yake hukaguliwa mara mara huku akiwaondoa hofu watu wanaodhani wanapunjwa.

MWANANCHI

No comments: