NA VICTOR MASANGU, KISARAWE PWANI
NAIBU Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi Utumishi na Utawala bora, Seleman Jafo amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kisarawe kumtafutia kazi nyingine meneja wa Mamlaka ya Bodi ya Maji Kisarawe Listern Materu kutokana na kushindwa kutatua kero ya maji kwa muda mrefu.
Jafo ambae pia ni mbunge wa jimbo la Kisarawe alisema, hawawezi kuendelea kukaa na watumishi ambao hawaguswi na matatizo ya wananchi.
Alitoa agizo hilo juzi mjini Kisarawe, kwenye mkutano aliouandaa kwa ajili ya kuwashukuru wananchi kwa kumpa ridhaa ya kuendelea kuongoza jimbo hilo, na kusikiliza kero zinazowakabili wananchi hao.
Naibu Waziri huyo alimtaka Materu kuachia nafasi ya Meneja ili apangiwe kazi nyingine kwani ameshindwa kutatua changamoto ya maji katika mji wa Kisarawe.
“Mkurugenzi mtafutie kazi nyingine katika ofisi yako, hatuwezi kuwa na watu ambao hawaguswi na matatizo ya watu tafuta atakayekaimu nafasi yake katika kipindi hiki.
Hatufanyi mambo ya kuchekeana, na hatuwezi kuibadilisha Kisarawe yetu kama tutaendelea kuwavumili watumishi wanaochangia kudumaza maendeleo”alisema Jafo.
Inadaiwa kuwa, Materu amekua meneja wa Mamlaka hiyo kwa zaidi ya miaka kumi lakini hakuna njia mbadala iliyobuniwa na mamlaka hiyo kuondoa tatizo la maji kukosekana mara kwa mara.
Mji huo wa Kisarawe una chanzo cha maji cha kimani ambacho kinatoa lita 16000 kwa saa na chanzo kingine cha minaki kinachotoa zaid ya lita 10,000 kwa saa hali ambayo ni dhahiri kusingekuwepo na tatizo la maji.
Wananchi waliohudhuria katika mkutano huo walifurahishwa na kitendo kilichofanywa na mbunge wao huku wakiendelea kumuomba ahamie katika idara ya ardhi.
Mwajuma Yusuph, Salehe Ally na Said Issa walisema kitendo cha kuondolewa Meneja huyo kitaleta mabadiliko kwani baadhi ya watumishi wanafanya kazi kwa mazoea bila kujali adha inayowapata wananchi.
No comments:
Post a Comment