Balozi Ombeni Sefue amekuwa kivutio kwenye televisheni kutokana na kutoa taarifa za kutenguliwa uteuzi kwa watumishi waandamizi wa umma, lakini jana hali ilikuwa tofauti baada ya kibao kugeuka.
Jana ilikuwa zamu ya Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa kumtangaza Balozi Sefue kuwa mtu wa kwanza kati ya wateule wa Rais Magufuli kuondolewa Ikulu.
Taarifa ya Ikulu haikuwa na maelezo mengi.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli amemteua Balozi Mhandisi John William Kijazi kuwa Katibu Mkuu Kiongozi,” inasema taarifa hiyo iliyotolewa na Msigwa.
“Kabla ya uteuzi huo, Mhandisi Kijazi alikuwa balozi wa Tanzania nchini India. Kufuatia uteuzi huo, aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue atapangiwa kazi nyingine.”
Injinia Kijazi anakuwa Katibu Mkuu Kiongozi wa tisa tangu nchi ipate uhuru mwaka 1961 na kabla ya kwenda India mwaka 2007, alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Miundombinu iliyokuwa inaongozwa na Dk Magufuli akiwa Waziri.
Katika mkanda wa video uliotumwa kwa vyombo vya habari jana, Rais Magufuli anamsifu Balozi Sefue kwa uchapakazi wake aliouonyesha kwa kipindi alichofanya naye kazi.
“Ni kwa sababu hiyo nimeamua kufanya mabadiliko kidogo,” anasema rais Magufuli katika mkanda huo kabla ya kueleza uteuzi huo.
Habari ambazo ziliibua mijadala jana ni za kuondolewa kwa Balozi Sefue, ambaye alionekana mtu anayekwenda na kasi ya Rais Magufuli, ambaye tangu aapishwe Novemba 5, 2015 amekuwa akifanya kazi ya kusimamisha na kutengua uteuzi wa watumishi wa umma wanaokabiliwa na tuhuma za uzembe, ubadhirifu, njama za kuhujumu mapato ya Serikali na wizi.
Sefue hakuonekana kuwa mmoja wa watu ambao wangeng’olewa kwa sababu yoyote ile, lakini amekuwa mtu wa kwanza kuondolewa kwenye nafasi yake ndani ya siku 123 tangu Magufuli aapishwe kuwa Rais, na siku 67 tangu balozi huyo atangazwe kuendelea na wadhifa wake Ikulu.
Mwanadiplomasia huyo wa muda mrefu alikuwa akipatikana kwa simu hadi jana alasiri alipojibu swali la Mwananchi kuhusu sakata la NSSF, lakini saa moja baadaye alipotafutwa kuzungumzia taarifa hiyo ya kuondolewa Ikulu, hakupokea simu kama ilivyo kawaida yake tangu aanze kufanya kazi chini ya Magufuli.
Katika siku za karibuni, Balozi Sefue amekuwa akihusishwa na sakata la uteuzi wa mkurugenzi mkuu wa Bohari ya Madawa (MSD) na uteuzi wa mkandarasi wa ujenzi wa daraja la Kigamboni, lakini Idara ya Habari (Maelezo) ilikanusha vikali habari hizo ikitaka walioandika wakanushe, jambo ambalo halijafanyika.
Sefue aliingia Ikulu Desemba 31, 2011 kuchukua nafasi ya Phillemon Luhanjo ambaye alikuwa amehitimisha mkataba wake wa utumishi wa umma.
Kabla ya hapo alifanya kazi Umoja wa Mataifa akiwakilisha Tanzania. Pia alifanya kazi Canada kabla ya kurejea nchini kuwa mwandishi wa hotuba wa Rais Ali Hassan mwinyi mwaka 1993 na baadaye Rais Benjamin Mkapa kuanzia 1995 hadi 2005.
Kwa upande mwingine, Injinia Kijazi amewahi kuwa Katibu Mkuu wa iliyokuwa Wizara ya Ujenzi na Miundombinu kwa miaka minne (2002-2006), wakati huo Waziri wa Ujenzi alikuwa Dk Magufuli.
Hata hivyo, mwaka 2007 aliondolewa kwenye wadhifa huo na kuteuliwa kuwa Balozi akiiwakilisha Tanzania katika nchi za India, Sri Lanka, Singapore na Nepal.
Tangu alipoondolewa Wizara ya Ujenzi na nafasi yake kuchukuliwa na Dk Ernos Bukuku, amekuwa akiishi New Delhi nchini India katika wadhifa wake wa ubalozi hadi jana alipoteuliwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi.
Akizungumzia uteuzi huo, Balozi Kijazi alisema anashukuru kwa uteuzi huo na anatumaini ni kwa sababu ya uchapakazi wake.
“Unajua nafasi kama hizi ni lazima uwe mtendaji,” alisema Balozi Kijazi.
“Nitaongea mengi nikishaapishwa.”
Wadau wazungumza
Alipoulizwa maoni yake kuhusu uteuzi huo, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu), Profesa Gaudence Mpangala alisema kuondolewa kwa Balozi Sefue katika nafasi hiyo ni mabadiliko ya kawaida kama alivyofanya kwa watendaji wengine.
Alisema kiongozi anapoingia madarakani anaweza kuunda safu yake mpya kwa kuwatumia watu wapya au akaendelea kufanya kazi na watu walewale. Alisema Rais ameamua kuunda safu yake mpya kwa kuwatumia watendaji wengine.
“Tumeona tangu alipoingia madarakani, Rais amebadilisha watendaji katika nafasi zao za juu kwenye utumishi wa umma. Kwa hiyo, nadhani Rais Magufuli ameona nafasi ya Sefue ichukuliwe na mtu mwingine ili kujenga safu mpya,” alisema Profesa Mpangala.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Emily Jonathan alisema Rais Magufuli hatabiriki katika utendaji wake. Alisema anaamini kwamba bado kuna watendaji wengine wataondolewa kwa sababu mbalimbali. “Sijashangaa kuondolewa kwa Sefue katika nafasi yake. Ninajua kuna sababu ya kufanya hivyo japo kuwa hajaweka wazi. Yeye ndiyo Rais wa nchi hii, hakuna mtu wa kuzuia mambo anayofanya,” alisema mhadhiri huyo.
No comments:
Post a Comment