ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 22, 2016

CUF: Hatumtambui Shein

Wakati Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) ikimtangaza matokeo ya uchaguzi Mkuu wa marudio Zanzibar na kumtangaza mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Ali Mohamed Shein, kuwa mshindi, Chama cha Wananchi (CUF) kimesema hakiitambui Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) chini ya Dk. Shein.

Dk. Shein alitangazwa jana na Mwenyekiti wa Zec, Jecha Salim Jecha, kuwa ameshinda uchaguzi huo uliofanyika juzi kwa kupata asilimia 91.4 ya kura zote kisha kumkabidhi cheti cha ushindi.

Uchaguzi huo ulifanyika baada ya Jecha kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa rais, wawakilishi na madiwani uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana, kwa madai kuwa ulikuwa na kasoro kadhaa.

Msimamo wa kutomtambua Dk. Shein na serikali yake ulitolewa na Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Omar Ali Shehe, alipokuwa akizungumza na Nipashe kuhusu msimamo wa chama chake baada ya kufanyika kwa uchaguzi huo.


Alisema kuwa uchaguzi huo ni batili na haramu kwa sababu uchaguzi wa Zanzibar ulifanyika Oktoba 25, mwaka jana na ulikuwa huru na wa haki.

Alisema kuwa CUF kinajipanga kufanya tathmini juu ya hali ya kisiasa Zanzibar na mwelekeo wake pamoja na kuangalia njia za kisiasa za kukabiliana na CCM katika siasa za Zanzibar.

“Kitendo cha kutoshiriki uchaguzi kina maana kubwa sana kwa chama cha CUF kwa sababu sasa tunafanya tathmini ya kuangalia hali ya kisiasa ya Zanzibar na njia za kukabiliana na CCM katika siasa pamoja na mustakibali wa Zanzibar,” alisema Shehe.

Alisema kwa mujibu wa ripoti za waangalizi wa ndani na nje wakiwamo wa Jumuiya ya Ulaya (EU) na Jumuiya ya Madola, Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana ulikuwa huru na wa haki.

Alisema pamoja na kufanyika kwa uchaguzi wa Zanzibar, CUF haitaitambua serikali wala kushirikiana nayo kutokana na upatikanaji wake kuwa batili kupitia uchaguzi huo.

Aidha, alisema pamoja na waliokuwa wagombea wa CUF katika uchaguzi wa mwaka jana kupigiwa kura licha ya kususia, kura hizo hawazitambui pamoja na matokeo yake.

Alisema wagombea wote wa CUF akiwamo mgombea urais, Maalim Seif Sharif Hamad na wagombea wa uwakilishi na udiwani walitangaza kujitoa katika uchaguzi wa marudio na kwamba huo ndiyo msimamo Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho.

Hata hivyo, alisema kura walizopigiwa waliokuwa wagombea wa CUF katika uchaguzi wa juzi ni mpango wa kutaka kuidaganya dunia kuwa CUF ilishiriki katika uchaguzi wa marudio.

Alieleza kuwa CUF itaendelea kupigania haki ya wananchi iliyoporwa na Jecha kwa kufuta matokeo ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana kinyume cha matakwa ya Katiba na sheria ya uchaguzi ya Zanzibar.

Akizungumzia kukamatwa kwa viongozi wa CUF na kuendelea kubakia mahabusu bila kupewa dhamana wala kufikishwa katika vyombo vya sheria, mkurugenzi huyo alisema kitendo hicho ni kinyume cha misingi ya haki za binadamu na utawala wa sheria.

Viongozi waliokamatwa kwa nyakati tofauti Machi 15 na Machi 18, mwaka huu ni Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma, Hamad Masoud Hamad na Mshauri wa mikakati wa KatibuMkuu wa CUF, Mansoor Yussuf Himid.

Shehe alisema kitendo cha viongozi hao kuwekwa mahabusu na kunyimwa haki ya dhamna ni uvunjaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala wa sheria.

Alisema kwa mujibu wa wakili wao, viongozi hao wamekuwa wakishikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Mwembe Madema, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja wakituhumiwa kwa makosa ya uchochezi na milipuko ya mabomu.
SOURCE: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Strategists wa CUF inabidi wajitafakari, hizi siasa za kususia katika nchi zetu ambozo demokrasia bado niyakutia maji haitawasaidia sana.Nakusema kuwa sasa ni muda muafaka wa kupambana na CCM bila ya wawakilishi au kuwa sehemu ya serikali kuu vilex2 ni kujidanganya