Mkutano na wanahabari ukiendelea.
Na Dotto Mwaibale
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza kushuka kwa bei ya mafuta nchini kuanzia kesho Machi 2, 2016.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam leo mchana, Mkurugenzi Mkuu wa (EWURA), Felix Ngamlagosi alisema bei ya Petroli imeshuka sh. 31 kwa lita sawa na asilimia 1.70, Dizeli sh. 114
kwa lita sawa na asilimia 7.10 na mafuta ya taa kwa sh. 234 kwa lita sawa na asilimia 13.75 ikilinganishwa na mwezi uliopita.
Alisema hapa nchini kwa sasa Petroli itauzwa Sh.
1,811, Dizeli sh. 1,486 na mafuta ya taa sh. 1,465.
Alisema kupungua kwa bei hizo kwa soko la
ndani kumetokana na kuendelea kushuka
kwa bei za mafuta katika soko la dunia.
Hata hivyo alisema hakutakuwa na mabadiliko yeyote
ya bei ya petroli na dizeli kwa mkoa wa Tanga kwa mwezi huu na kwamba hiyo imetokana
na kutopokea mafuta mapya kupitia Bandari ya mkoa huo katika kipindi cha
Februari mwaka huu.
"Mamlaka inapenda kuujulisha umma kuwa bei
hizi kikomo za mafuta kwa eneo husika zinapatikana vilevile kupitia upigaji wa simu ya mkononi kwa mitandao yote kwenda namba *152*00# na
kisha kufuata maelekezo.
Aliongeza kuwa kwa mujibu wa sheria ya mafuta ya
mwaka 2015, bei za bidhaa za mafuta zitaendelea kupangwa na soko hivyo Ewura
itaendelea kutoa taarifa za bei kikomi lengo likiwa ni kuwasaidia wadau kufanya maamuzi stahiki kuhusu manunuzi ya bidhaa hiyo.
Aidha amevitaka vituo vyote vya mafuta nchini na
kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayonekana bayana na
yakionesha bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni
zinazotolewa na kituo husika.
Alisema wateja wanashauriwa kununua bidhaa za
mafuta kutoka kwenye vituo vinavyouza mafuta kwa bei ndogo zaidi ili kushamirisha
ushindani. Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri
kwa wateja na adhabu itatolewa kwa kituo husika.
Alibainisha kuwa wanunuzi wanashauriwa kuhakikisha
kuwa wanapata stakabadhi ya malipo inayoonesha jina la kituo, tarehe, aina ya
mafuta kwa lita na kwamba stakabadhi ya malipo itatumika kama kidhibiti cha
mnunuzi wa mafuta endapo kutajitokeza malalamiko ya ama kuuziwa mafuta kwa bei
ya juu kuliko bei kikomo, au yenye kiwango cha ubora kisichofaa.
(Imeandaliwa na mtandao wa www. habari za jamii.com)
No comments:
Post a Comment