Konseli Mkuu wa Ubalozi Mdogo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliopo Jeddah, Saudi Arabia, Bw. Suleiman Saleh, Jumatatu Machi 28, 2016, amekutana na Bw. Oumarou Issa, Konseli Mkuu wa Jamhuri ya Cameroon, ambaye pia ni kiongozi wa Makonseli Wakuu wa Afrika wanaoziwakilisha nchi zao Jeddah, Saudi Arabia. Bw. Issa alimkaribisha Bw. Saleh ofisini kwake na kumweleza kwa urefu na undani utendaji kazi wake pamoja namna sahihi ya kuweza kutekeleza majukumu yake mapya katika mazingira mapya.
Bw. Issa Issa ambaye anaongoza Makonseli Wakuu 25 kutoka nchi za Afrika alibadilisha mawazo na Bw. Saleh katika maeneo mbali mbali kuanzia mahusiano yaliyopo na Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia kimawasiliano pamoja na katika kufuatilia masuala mbali mbali ya kikazi. Aidha Bw. Issa alimfahamisha Bw. Saleh uwepo wa Konseli 98 kutoka nchi mbali mbali duniani ambazo nazo kadri ya mahusiano yalivyo na nchi zetu zinatoa fursa ya kuimarisha mahusiano zaidi ya kiuchumi na kijamii. Bw. Issa aliongeza kwamba Jeddah ni kitovu cha biashara cha Saudi Arabia ambapo kuna fursa nyingi ambazo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaweza kufaidika nazo.
Kwa upande wake Bw. Suleiman Saleh alimshukuru Bw. Oumarou Issa kwa nasaha zake nzuri ambazo zitamsaidia katika utendaji wake na kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Kwa upande mwingine Bw. Saleh anatarajia kukutana Mtendaji Mkuu wa Shirika la Ndege la Saudia, Saudi Airlines, ikiwa ni katika juhudi za kuimarisha mahusiano baina ya nchi hizo mbili kwa kulishawishi shirika hilo kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka Jeddah kwenda Dar-es-Salaam. Uwepo wa kiunganisho cha mawasilano ya namna hiyo kitakuwa ni chachu kubwa ya kukuza biashara, uwekezaji, utalii pamoja na kuondoa kero sugu ya usafiri wa mahujaji wanaokuja nchini humu kwa ibada ya Hijjah. Kwa sasa Mashirika ya Emirates na Etihad ya Falme za Kiarabu, Qatar Airways la Qatar, Oman Air la Oman yanafanya safari za moja kwa moja kila siku kutoka nchi hizo kuja Tanzania. Ni Saudi Arabia pekee ambayo hadi sasa Shirika lake la Ndege la Saudi Airlines halijaanza safari za kuja nchini Tanzania.
Pichani Bw. Issa Oumarou, Konseli Mkuu wa Jamhuri ya Cameroon na Kiongozi wa Makonseli Wakuu wa Afrika waliopo Jeddah, Saudi Arabia akimkaribisha Bw. Suleiman Saleh ofisini kwake pamoja na kufanya nae mazungumzo.
No comments:
Post a Comment