Konseli Mkuu wa Ubalozi
Mdogo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliopo Jeddah, Saudi Arabia, Bw.
Suleiman Saleh, Jumanne Machi 29, 2016, amekaribishwa rasmi katika Wizara ya
Mambo ya Nje ya Saudi Arabia alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi
Muhammad A. Tayeb, Mkurugenzi Mkuu wa Wizara hiyo.
Balozi Tayeb alimpokea
Bw. Saleh Ofisini kwake Jeddah na kuahidi kutoa ushirikiano unaohitajika katika
kuimarisha mahusiano baina ya Saudi Arabia na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kufuatia kusainiwa hivi karibuni Ikulu, Dar-es-Salaam, makubaliano ya mashirikiano
baina ya nchi hizo mbili. Makubaliano hayo ambayo yalisainiwa na Mhe. Adil Jubeir, Waziri wa Mambo ya Nje wa
Saudi Arabia na Mhe. Balozi Augustine Mahiga, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Kikanda na Kimataifa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
yalishuhudiwa pia na Mhe. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Kwa mujibu wa Balozi
Tayeb, kusainiwa kwa makubaliano hayo kumefungua ukurasa mpya wa mahusiano
baina ya Saudi Arabia na Tanzania na hakusita kuonyesha furaha yake kutokana na kuainishwa maeneo mahususi ya
mashirikiano katika sekta za uchumi,
uwekezaji na biashara.
Pichani Balozi Muhammad Tayeb, Mkurugenzi Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia akimkaribisha Bw. Suleiman Saleh, Konseli Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jeddah, na kufanya nae mazungmzo kuhusu mahusiano baina ya Saudi Arabia na Tanzania.
No comments:
Post a Comment