Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, amesema ikiwa ni miezi mitatu tu tangu aingie ofisini baada ya kuteuliwa Desemba 10, mwaka jana na kuapishwa siku mbili baadaye, mpaka sasa tayari watu 3,000 wamekamatwa kwa tuhuma za kuhusika na biashara ya dawa za kulevya.
Kauli hiyo ya Waziri Kitwanga inakuja ikiwa ni siku chache tangu Ofisi ya Hazina inayoshughulikia udhibiti wa mali za nje ya Marekani (Ofac), kutangaza kushikilia mali za raia wa Tanzania, Ali Khatib Haji Hassan maarufu kama ‘Shkuba’, zilizo nchi mbalimbali, kutokana na kumtuhumu kuwa ndiye msambazaji mkubwa wa dawa hizo kutoka Afghanistan kwenda barani Asia, Marekani na eneo kubwa la Afrika.
Wakati Marekani ambayo pia imepeleka suala hilo kwenye Bunge la Congress tangu ilipotoa taarifa hiyo, Bodi ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya (International Narcotic Control Board – ICBC), nayo ilitoa ripoti ya mwaka 2015 iliyolenga Afrika na Tanzania, ikionyesha kuwa Tanzania ni kichochoro cha kupitisha dawa za kulevya zinazosambazwa karibu nusu ya dunia.
Akizungumza na Nipashe katika mahojiano maalum, Kitwanga alisema:
“Kama utakumbuka mara tu nilivyoteuliwa, nilisema suala la dawa za kulevya tutapambana nalo na siogopi kufa, nilisema na narudia tena siogopi kufa, hili ni suala la kufa au kopona.
“Hatutakubali tena Tanzania iingize dawa za kuleva au iwe njia ya kupitishia kwenda sehemu nyingine, au hata kama soko, kikubwa tunachokifanya sasa ni kujenga mifumo itakayozuia kabisa dawa kuingia nchini kwetu na zile zilizopo zitafutwe na zikamatwe, ndiyo sababu tunasema tumekamata watu wengi sana kwa muda mfupi sana ili kuhakikisha dawa za kulevya hazipitishwi hapa Tanzania.”
Alipoulizwa idadi ya watu waliokamatwa, Kitwanga alisema: “Kwa muda niliokaa hapa, zaidi ya watu 3,000 wamekamatwa, kuna wakubwa sana, wakubwa wa kati, wale wanaopokea tumewakamata zaidi ya 20, wanaosambaza tumekamata zaidi ya 100 na wale wanaouza kidogo kidogo ndiyo wengi zaidi." na kuongeza:
“Lakini bado tunaendelea na sasa hivi siyo suala tu la kwamba tukukamate na dawa za kulevya, tunakwenda mbali zaidi kwamba ukitajwa au tukikuhisi, tuone na utuhakikishie kwamba wewe kweli siyo muuza dawa za kulevya.
“Kuhisiwa tu ni kwamba lazima tufanye uchunguzi wetu utuhakikishie kuwa wewe siyo muuza dawa za kulevya.”
Akizungumzia mkanganyiko wa kauli aliyonukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa ana orodha ya majina ya wauza dawa za kulevya, Kitwanga alisema alinukuliwa vibaya.
“Watu walininukuu vibaya, ile ya kwamba nayajua (majina ya wauza dawa), huwezi ukawajua wote, hata ukijua, utajua kidogo tu, kinachotakiwa ni kuweka mfumo wa kufumua kila kitu, na huo ndiyo tumeuweka na tunaendelea kuuimarisha,” alisema na kuongeza:
“Nilisema jamani mimi sijapewa orodha, na siijui orodha, mimi ninachotaka kutengeneza ni kujenga mfumo utakaohakikisha kwamba dawa za kulevya haziingii na zilizopo ndani zinakamatwa na wahusika wote wanakamatwa wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.”
Alipoulizwa kama alipoingia ofisini alikuta orodha ya wauza dawa za kulevya na majangili ambayo kiongozi mmoja wa serikali ya awamu ya nne alisema anayo, Kitwanga alisema yeye haangalii orodha, kazi yake ni kuwasaka wauza dawa hizo tu.
“Mimi nadhani sikumbuki sana, lakini nakwambia sasa hivi, sisi siyo suala la orodha, sisi ni suala la kuwasaka, kuwakamata na tutaendelea na hii siyo ya siku moja, siyo ya siku mbili ni endelevu, niwapo wizarani mimi, nisiwapo wizarani, kwa sababu tunajenga mfumo,” alifafanua Kitwanga.
Alisema kazi yake ni kujenga mfumo utakaohakikisha dawa za kulevya haziingia nchini na kwamba mfumo uliokuwapo awali ulikuwa dhaifu kidogo.
Kutokana na hali hiyo, alisema katika miezi sita mataifa ya nje yatakuwa na imani kwamba Tanzania hakuna tena suala la dawa za kulevya, jambo litakalopunguza kero ambazo Watanzania wanakutana nazo wanaposafiri nje ya nchi kwa kupekuliwa sana kutokana na kuhisiwa wanafanya biashara hiyo.
“Katika miezi sita, watu watakuwa na imani na Tanzania kuwa hakuna dawa za kulevya, sasa hivi tunaimarisha zaidi doria baharini, kwenye mipaka yetu ili tuhakikishe hakuna mwanya wa kuingiza,” alisema na kuendelea:
“Sasa hivi hakuna sukari (za magendo) wala dawa za kulevya, kwa sasa bado tuna tatizo huku Kusini kidogo, lakini tunafikiria kuanzisha mkoa wa kipolisi mwingine wa hapa baada ya Dar es Salaam, ukienda Kibiti, hususan katika eneo la bahari sana sana.”
MABADILIKO UHAMIAJI
Kwa upande wa mabadiliko yaliyofanywa kwenye Idara ya Uhamiaji na Polisi hivi karibuni, alisema pamoja na mambo mengine, lilichangiwa na kushamiri kwa biashara ya dawa za kulevya.
“Lakini hatuiishi Uhamiaji tu na Uhamiaji kwenyewe siyo kwamba tutaishia hapo, Uhamiaji tutaendelea, Polisi tutaendelea, kwenye Magereza tutafanya na Zimamoto. Suala ni kuhakikisha kwamba wizara yote inabadilisha utendaji na unakuwa wa hali ya juu kwa ajili ya kuhakikisha kwanza wananchi wetu wanaendelea kuwa salama, wageni au watu wote wanaoingia, wanafanya hivyo kihalali,” alisema Kitwanga.
UHALIFU WA SILAHA
Akizungumzia suala la uhalifu wa kutumia silaha kuongezeka kwa siku za karibuni, alisema serikali imeliona na sasa hivi wanaangalia namna ya kuweka alama katika aina zote za bunduki.
“Silaha nyingi bado hutoka Burundi kutokana na hali ilivyo kule, lakini sasa hivi tunautaratibu wa kuziwekea alama bunduki kuanzia SMG mpaka bastola ili zitambulike ni za nchi gani.
“Mara chache majambazi wakiua, askari huwa tunatafuta sana bunduki zile tunazoshindwa kuzipata mapema, zinaweza kufanya uhalifu pindi wanapoziiba,” alisema.
Alisema wanaangalia namna ya kuwatambua waendesha bodaboda wote ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakitumiwa kwenye uhalifu wa silaha unaoendelea.
“Sasa hivi wizara kama tatu tunashirikiana, Wizara ya Uchukuzi na Mawasialiano ambayo Sumatra wapo chini yao, wizara yangu na Tamisemi wanaotoa maeneo ya maegesho, tunafikiria kuwapa hata sare ili kujua kila bodaboda anatoka sehemu fulani, wilaya fulani na kituo fulani ili kudhibiti uhalifu huu,” alisema Kitwanga.
POLISI KUSHIRIKIANA NA WAHALIFU
Kuhusu baadhi ya polisi kulalamikiwa na wananchi kushirikiana na wahalifu hali ambayo inachochea uhalifu kuongezeka, alisema kwa hatua ya kwanza wamehamisha Ma-RPC na RCO mbalimbali.
“Tumefanya hivyo ili tuhakiki ni RPC yupi au RCO yupi anashirkiana na wahalifu. Kama ukiondoa mmoja hapa ukimpeleka kwingine, uhalifu ukapanda, utajua anashirikiana na wahalifu. Hi ni kwa sababu bado hatujapata ushahidi wa moja kwa moja, lakini kama hapa kulikuwa hakuna uhalifu, halafu ukamhamishia mwingine na uhalifu ukaanza, tutajua kwamba wewe siyo mwenzetu," alisema Kitwanga na kuongeza:
“Sasa hivi tumehamisha wengi sana, kinachofuata siyo kuhamisha tena ni kufukuza, kama hapa kulikuwa hakuna uhalifu huyu kaja ukaanza tutajua huyu siyo mwenzetu,” alisema Kitwanga.
UGAIDI
Akizungumzia tishio la ugaidi nchini ambao kwa siku za hivi karibuni vikundi vya uhalifu vimekuwa vikisajili watoto wadogo kwa njia mbalimbali ikiwamo mtandao, Kitwanga alisema ushirikiano wa Watanzania wote na kuondoa tofauti zao za kisiasa, ni muhimu ili kuhakikisha nchi inabaki salama.
“Lazima ujue mtoto wako yuko wapi, kama husemi kwamba kapotea, hayupo, itakuwa ngumu kukabiliana na suala hili.
Kama likizo imefika mtoto hajaja, mzazi hujiulizi kwa nini mtoto hajafika, itakuwa vigumu. Watanzania tujue watoto wetu, ndugu zetu, wako wapi, kwenye serikali za mitaa kama kuna vikundi vinajifunza ugaidi, kwanini tusiseme? Na kila kiongozi ajue kuna nini kwenye mtaa wake, lakini kila mmoja kama hajali ni tatizo.
“Kuondoa tofauti za kisiasa ni muhimu, kama mabalozi wa nyumba 10 wanaonekana ni wa CCM, hawa wengine wanaacha kushirikiana nao, ni tatizo kubwa, ikibidi na wao waanzishe wakwao, hawa viongozi wa ngazi za chini ni wazuri zaidi kutusaidia,” alisema.
SOURCE: NIPASHE
No comments:
Post a Comment