Hali hiyo ilitokea baada ya mawakili wa serikali wakiongozwa na Vincent Tangoh na wale wa Mabula, kupinga mahakama kupokea fomu namba 21B, ambacho kinaonyesha idadi ya kura katika vituo 693.
Wenje alitoa kielelezo hicho kama ushahidi, baada ya kumaliza kutoa ushahidi alipokuwa akihojiwa na wakili wake, Elias Hezron, hatua iliyozusha ubishaji wa kisheria kwa takriban saa mbili huku mawakili wa mlalamikiwa wakivikataa.
Ubishani huo wa kisheria, ulitokana na jopo la mawakili wa serikali, liliongozwa Wakili Tangoh pamoja na mawakili wa Mabula, Constantine Mutalemwa na Faustine Malongo, kugoma kupokea vielelezo hivyo kwa madai kuwa kisheria shahidi hatakiwi kuviwasilisha mahakamani hapo.
Hali hiyo ilisababisha, mawakili wa Wenje, Daya Outa na Hezron, kusimama kidete kutetea sababu za mteja wao kuwasilisha ushaidi wa fomu hizo No. 21B mahakamani.
Kutokana na ubishani mkubwa wa kisheria, Jaji Kasukulo Sambo, aliamuru kesi hiyo iahirishwe hadi Jumanne ijayo, atakapotoa uamuzi iwapo shahidi huyo aendelee kutoa ushahidi wake mahakamani au la.
Awali, Jaji Sambo, alianza kutoa uamuzi ya pingamizi dogo la kupinga aya ya vipengele vilivyokuwamo kwenye utetezi wa Wenje, huku akikubaliana na wakili Tangoh, kuondoa aya tatu zilizokuwamo kwenye ushahidi huo lakini akipinga kuondoa aya zingine tatu zilizopingwa na Mutalemwa.
Wakati hayo yakiendelea, Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani Mwanza, jana kililituliza jiji la Mwanza kwa muda, baada ya kusambaratisha makundi ya wafuasi na wanachama wa Chadema, waliokusanyika kwa ajili ya kusikiliza kesi hiyo.
FFU hao, waliotanda katika mitaa mbalimbali ya jiji la Mwanza, walikuwa na lengo la kutibua vikundi vya wafuasi hao waliokuwa wamesimama makundi makundi.
Hata hivyo, FFU hao ambao mara nyingi hutumia mabomu ya kutoa machozi, jana waliamua kutumia fimbo na virungu, licha ya gari la maji ya kuwasha (washawasha) kurandaranda mitaani.
Ulinzi huo mkali uliowekwa mitaani, pia ulionekana katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, baada ya watu waliotakiwa kuingia mahakamani hapo kuulizwa maswali na askari.
SOURCE: NIPASHE
No comments:
Post a Comment