Thursday, March 3, 2016

Mbunge wa Kinondoni aponda nauli ya Makonda

By Tumaini Msowoya, Mwananchi tmsowoya@mwananchi.co.tz
Dar es Salaam. Mbunge wa Kinondoni, (CUF), Maulid Mtulia amepinga mpango wa walimu wa Mkoa wa Dar es Salaam kusafiri bure kwenye daladala akisema utawashushia heshima.

Badala yake, alitaka Manispaa ya Kinondoni iweke utaratibu wa kuwaongezea walimu fedha za usafiri kwenye mishahara yao ili wajilipie wenyewe.

Kauli ya mbunge huyo imekuja baada ya Mkuu wa Wilaya ya hiyo, Paul Makonda kutangaza kuwa walimu wa shule za Serikali za Dar es Salaam watasafiri bila kulipa nauli kwenye daladala.

Katika mpango huo ambao umepangwa kuanza Jumatatu ijayo unaozigusa pia manispaa za Temeke na Ilala, walimu watapatiwa vitambulisho maalumu vyenye saini ya Makonda.

Akizungumza katika mahojiano maalumu juzi, Mtulia alisema licha ya kuwa wazo lililenga kuwasaidia walimu, lakini litawasababishia dhihaka.

Alisema kinachopaswa kufanyika ni kutafuta suluhisho la kudumu la kero zinazowakabili walimu ambazo zinachangia kushuka kwa kiwango cha elimu nchini.

“Itafika hatua kondakta atamsimamisha mwalimu kwenye kiti kama ilivyo kwa wanafunzi kwa sababu tu halipi nauli… Wazo hili ni zuri lakini lilipaswa kuboreshwa kama kweli nia ni kumsaidia mwalimu,” alisema.

Alisema ikiwa kweli nia ni kuwasaidia walimu, basi halmashauri zina wajibu wa kuhesabu siku za kazi na kiasi ambacho mwalimu atalipia nauli ili fedha hizo ziongezwe kwenye mshahara wake.

Alisema njia hiyo itakuwa ya heshima zaidi kuliko walimu kusafiri bure kwa kutumia vitambulisho kama walivyo wanafunzi wao. Hata hivyo, alisema ipo haja kwa viongozi wa manispaa hiyo kukaa meza moja na walimu ili kujua changamoto zinazohitaji suluhu ya haraka, akisema huenda nauli ikawa si ya msingi kwao.

Bomoabomoa

Mbunge huyo amepinga hoja ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, January Makamba kuhusu wananchi waliobomolewa nyumba zilizokuwa zimejengwa kwenye Bonde la Mto Msimbazi kuwa wenye kibali ndiyo watakaolipwa.

“Kama watu walipelekewa umeme, maji na wakawa wanalipa kodi ya majengo kwa Serikali halafu wanaondolewa bila taarifa wala kuwapa eneo jipya kwa ajili ya makazi yao, huo ni uonevu. Nani mwenye kosa hapo? Bomoabomoa haikuwatendea haki wananchi maskini,” alisema.

Alisema aliamua kufungua kesi ya kuwatetea wananchi hao mahakamani akiamini kuwa ndiyo njia pekee inayoweza kuwapatia haki. Alibainisha kuwa kabla ya kuwabomolea, wananchi hao wangepewa taarifa, muda wa kujiandaa na mahali pa kuhamia tofauti na hali ilivyotokea.

Hata hivyo, alisema njia pekee ya kuwasaidia wananchi hao kwa sasa ni kuwapatia eneo la kuhamia.“Mabwepande walipelekwa wananchi wasiozidi 200 kutoka kwenye jimbo langu wakati waliobomolewa wanazidi 800, Serikali itenge maeneo mengi ili haki za binadamu ziendelee kulindwa,” alisema.

Alisema Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lingeweza kuwa msaada kwa wananchi wasio na makazi, lakini jambo hilo limeshindikana. Alisema yupo kwenye harakati za kuandaa mradi wa kuwatafuta wafadhili watakaojenga maghorofa kwa ajili ya watu wasio na uwezo wa kuwa na makazi, wakiwamo waliovunjia nyumba.

“Ninafikiria kutengeneza makazi kwa watu maskini kama ilivyo Michenzani, Zanzibar. Yale maghorofa yalijengwa kwa watu maskini. Sasa nina mpango huo kwa Dar es Salaam,” alisema.

Alisema ameandaa pendekezo la mradi wa ujenzi wa nyumba na kwamba wakati wowote atapata wafadhili.

Alisema Manispaa ya Kinondoni itatakiwa kutoa maeneo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba hizo.    

No comments: