ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, March 12, 2016

Ukusanyaji wa kodi ya Serikali waikuna TPSF



Mwenyekiti wa TPSF, Reginald Mengi 
By Elizabeth Edward, Mwananchi eedward@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Umoja wa wafanyabiashara walio chini ya Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), umempongeza Rais John Magufuli na Serikali yake kwa juhudi ya ukusanyaji wa kodi na mapato na kuahidi kuwa watatimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria.

Wafanyabiashara hao pia wamepongeza mpango wa Serikali wa kudhibiti matumizi yasiyo na tija na badala yake, kuzielekeza fedha hizo katika maeneo yanayowagusa wananchi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa tovuti ya mawasiliano kwa ajili ya wafanyabiashara, Mwenyekiti wa TPSF, Reginald Mengi amesema jitihada hizo zimewatia moyo wafanyabiashara na kuwapa imani kwamba kodi wanazolipa zinatumika vizuri kwa kuelekezwa kwenye miradi ya maendeleo ya jamii na kiuchumi.

“Sekta Binafsi tumefarijika sana kuona dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kurudisha utawala wa sheria na haki; kurudisha uwajibikaji wa viongozi wa umma na juhudi zakukabiliana na urasimu hususan katika kufanya na kutekeleza uamuzi unaohusu biashara na uwekezaji.

“Tunaamini kwamba kasi hii italeta manufaa makubwa kwenye ukuaji wa pato la Taifa kutoka asilimia 6.9 ya mwaka 2015 na kufikia tarakimu mbili ndani ya miaka mitatu hadi mitano ijayo. Pia, ni mategemeo yetu kuwa mfumuko wa bei uliopo sasa wa asilimia 6.5 utadhibitiwa na kushuka chini ya asilimia tano,” amesema Mengi.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amesema Serikali inatambua mchango wa kundi hilo kwa maendeleo ya Taifa na kuahidi kuwa itaendelea kuweka mazingira mazuri ya kufanyia kazi wafanyabiashara.

“Amesisitiza kuwa wakati umefika kwa wafanyabiashara wa Tanzania kupanua wigo kwa kuwekeza nje ya mipaka ya nchi zinakopatikana fursa.

“Nimeambiwa Sudan kuna ardhi nzuri ya kilimo na wako tayari kuwaingiza wawekezaji katika sekta hiyo, kama mnaweza nendeni huko, hakuna sababu ya kulima mahindi huku na kusafirisha wakati shughuli zote zinaweza kufanyika huko,” amesema Mwijage.

No comments: