ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, March 31, 2016

YANGA, AZAM ZAANZA RATIBA NGUMU LEO

Robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho inafanyika leo kwa mechi mbili kali - Yanga wakiikaribisha Uwanja wa Taifa Ndanda FC ya Mtwara, huku Azam FC wakiwa Chamazi kukipiga dhidi ya Tanzania Prisons ya Mbeya.

Yanga na Azam zinazoshiriki michuano ya klabu Afrika, zimepangiwa ratiba ngumu inayojumuisha mechi za Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho, huku pia ikikabiliwa na michuano ya kimataifa.

Yanga inashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na inatarajia kuikaribisha Al Ahly ya Misri Aprili 9 kwenye Uwanja wa Taifa, wakati Azam atakuwa mwenyeki wa Esperance ya Tunisia kwenye Uwanja wa Chamazi.

Yanga yenye matumaini ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo, itashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao 1-0 iliyoupata Januari 17 dhidi ya Ndanda.

Kwa upande wa Azam FC, watakuwa wakijaribu kusaka ushindi nyumbani baada ya mchezo wa kwanza dhidi ya maafande hao kumalizika bila kufungana Februari 24 kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm, alisema kwenye mchezo huo atashusha kikosi kamili na lengo likiwa ni kusonga mbele.

Pluijm alisema tofauti na wengi wanavyotarajia kwamba atashusha 'jeshi jepesi', amepanga kuchezesha kikosi cha kwanza.

"Mechi za mtoano ni ngumu na ili usonge mbele lazima kujiandaa kikamilifu. Hatutaidharau Ndanda, tunaifahamu vizuri na tunajua uwezo wao," alisema Pluijm.

Kocha huyo aliongeza kwamba ushindi katika mechi hiyo utakisaidia kikosi chake kufanya vizuri mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar itakayofanyika Jumapili na Jumatano watakapoikaribisha Mtibwa Sugar.

Msemaji wa Azam FC, Jaffer Iddi aliliambia gazeti hili jana kuwa timu yao imejipanga kufanya vizuri dhidi ya Prisons na wanashukuru wamefahamu uzuri wa kikosi hicho ulipo baada ya kutoka nao suluhu.

Iddi alimtaja mshambuliaji wao wa kimataifa, Kipre Tchetche kuwa hatacheza mechi hiyo baada ya kuanza mazoezi mepesi juzi.

Michuano hiyo itaendelea tena Aprili 11 kwa Simba kuikaribisha Coastal Union.
Mwadui FC ya Shinyanga ndiyo timu pekee hadi leo iliyotangulia hatua ya nusu fainali.
CHANZO: NIPASHE

No comments: