ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 30, 2016

Zanzibar: Hatutishiki na pesa za MCC

Licha ya Bodi ya Shirika la Changamoto za Milenia (MCC), kukutana juzi na kupiga kura kusitisha mchakato wa maandalizi ya mkataba wa pili na Serikali ya Tanzania, Zanzibar imesema haitishiki na uamuzi huo, na kwamba itatumia inachokipata kwa masilahi ya wananchi wake.

Moja ya vigezo vya msingi, ambavyo MCC hutumia kuingia ubia na nchi yoyote, ni dhamira ya dhati ya nchi husika kuimarisha demokrasia na kuendesha uchaguzi ulio huru na haki.

Kutokana na sababu hiyo, mchakato wa uchaguzi visiwani Zanzibar ambao waangalizi wa kimataifa walieleza kuwa ulikuwa huru na haki na haukuwa na dosari yoyote, pamoja na matumizi ya Sheria ya Mtandao, imeelezwa ndicho kilichoifanya Tanzania kuenguliwa, hivyo kukosa fungu la miradi ya maendeleo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, aliliambia Nipashe jana kuwa: “Wao wana hiari yao, lakini sisi kama Serikali wala hatutishiki na hilo. Tunachokipata tutatumia kwa maslahi ya wananchi wetu wa Zanzibar."

Balozi Seif alisema nchi wahisani zimekuwa na utamaduni wa kutoa misaada yenye masharti ya kuzitaka nchi zinazoendelea kufanya mambo zinavyotaka wakati Zanzibar ina haki ya kusimamia mambo yake ya ndani bila kuingiliwa.

“Uchaguzi huru na wa haki hatujui tafsiri yake kwa wao ni ipi. Uchaguzi ulioharibika hatujui tafsiri yao ni ipi, lakini sisi tunajua kuwa uchaguzi uliofutwa ni uchaguzi uliovurugwa ndiyo maana Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (Jecha Salim Jecha), akaamua kuufuta na kuitisha uchaguzi wa marudio,” alisema.

Aliongeza kuwa: “Hii si mara ya kwanza kwa hawa wahisani kutufanyia kitendo hicho. Mwaka 1995 walifanya hivyo hivyo baada ya wenzetu kupita huko na kuwaambia nchi za Ulaya kwamba wasitoe misaada kwa Zanzibar kwa sababu za kisiasa, lakini hatukushughulika, tumekwenda miaka mitano mfululizo.”

Hata hivyo, alisema serikali itahakikisha inapunguza matumizi yasiyokuwa ya lazima ili kukabiliana na mazingira yoyote yatakayojitokeza na kuona bajeti ya serikali inakidhi mahitaji ya wananchi wake kulingana na kile kitakachokuwa kinapatikana.
CHANZO: NIPASHE

2 comments:

Anonymous said...

Hawa MCC ni Moja ya Majambazi sasa wameona kugumu ndio wanaleta longolongo.

Anonymous said...

same shit different days, this always happen only if you cannot bring food on your table. dawa ni kujitegemea hawa jamaa wanaitumia sana misaada kuwanyanyasa wanaopewa misaada. uharibifu walioufanya kule Iraq sijui nani anawahukumu, sasa hawataishia hapo tu watatulazimisha tuzikubali ndoa za mashoga tujiandae na hilo linakuja, they know our weakest points they know how to get us to do things on their ways.