
Dar es Salaam. Kamishna mkuu wa zamani wa TRA, Harry Kitilya pamoja na maofisa wawili waandamizi wa zamani wa Benki ya Stanbic tawi la Tanzania, Shose Sinare na Sioi Solomon wamepandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa makosa manane likiwamo la kutakatisha fedha.
Washtakiwa wote walisomewa mashtaka manne likiwamo la utakatishaji wa fedha kiasi cha Dola za Marekani 6 milioni, lakini Sinare aliyekuwa mrembo wa Tanzania mwaka 1996 anakabiliwa na mashtaka mengine mawili ya kughushi na mawili mengine ya kuwasilisha nyaraka za uongo Serikali ya Tanzania ilipokopa Dola za Marekani 550 milioni kutoka Benki ya Standard ya Uingereza kati ya mwaka 2012 na 2013.
Kuwapo kwa shtaka la kutakatisha fedha kuliibua mvutano wa kisheria mahakamani hapo na mawakili wa utetezi wakiongozwa na Dk Ringo Tenga walidai washtakiwa wana haki ya kupata dhamana, huku mawakili wa Serikali wakiongozwa na Oswald Tibabyekomya wakidai shtaka hilo halina dhamana.
Kutokana na mvutano huo wa hoja, Hakimu Emilius Mchauru anayesikiliza kesi hiyo aliamuru washtakiwa wapelekwe mahabusu hadi Aprili 8, mwaka huu atakapotoa uamuzi kama washtakiwa wana haki ya kupewa dhamana au la. Uamuzi wa mahakama wa kuamuru washtakiwa wapelekwe mahabusu ulipokewa kwa simanzi na ndugu wa washtakiwa walijikuta wakilia wakati washtakiwa hao walipoongozwa na askari kuelekea mahabusu ya mahakama hiyo kabla ya kupelekwa gerezani. Magari mawili ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) aina ya Toyota Land Cruiser yaliyowafikisha mahakamani hapo huku wakisindikizwa na maofisa wa taasisi hiyo, ndiyo yaliwachukua saa 11.15 jioni kuwapeleka mahabusu gerezani.
Wakati wakiondoka kwenda kupanda magari hayo tayari kwa safari ya kuelekea gerezani, washtakiwa hao walikuwa wamebeba ndoo ndogo aina ya plastiki, huku Kitilya na Sinare wakiagana na ndugu zao kwa kuwapungia mikono.
Awali, washtakiwa wote walikana kuhusika na makosa hayo. Wakili wa Serikali, Tibabyekomya aliieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika hivyo aliiomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kesi hiyo kutajwa.
Mashtaka
Mashtaka waliyosomewa ni pamoja na kula njama ili kutenda kosa la kujipatia fedha, linalowakabili washtakiwa wote; mashtaka matatu ya kughushi ambapo moja linawakibili wote, na mawili yanamkabili Sinare peke yake.
Mashtaka mengine ni mawili ya kuwasilisha nyaraka za uongo yanayomkabili Sinare peke yake, shtaka la kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu linalowakabili washtakiwa wote na moja la kutakatisha fedha ambalo pia linawakabili wote.
Wakili wa Serikali Christopher Msigwa alidai kuwa washtakiwa hao pamoja na wengine ambao hawako mahakamani walitenda makosa hayo kwa nyakati tofauti kati ya Agosti 2012 na Septemba 2015.
Katika shtaka la kwanza washtakiwa hao na wenzao ambao hawajafikishwa mahakamani wanadaiwa kutenda kosa la kula njama za kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kati ya Agosti 2012 na Machi 2013 katika Jiji la Dar es Salaam.
Msigwa alidai shtaka la pili ambalo linamkabili Sinare ni la kughushi alipokuwa makao Makuu ya Benki ya Stanbic iliyopo Kinondoni Agosti 2, 2012. Pia, Msigwa alidai Sinare akiwa na nia ya kudanganya aliandaa nyaraka za mapendekezo kuonyesha kuwa Benki ya Standard ya Uingereza ikishirikiana na Benki ya Stanbic ya Tanzania kuwa watatoa mkopo wa Dola za Marekani 550 milioni kwa Serikali ya Tanzania kwa ada ya uwezeshaji ya asilimia 2.4 ya kiasi cha mkopo huo wakati akijua kuwa siyo kweli.
Shtaka la tatu linalomkabili pia Sinare pekee ni kwamba anadaiwa Agosti 2, 2012 alitoa nyaraka za uongo za mapendekezo ya kuonyesha kuwa Benki ya Standard ya nchini Uingereza ikishirikiana na Benki ya Stanbic ya Tanzania, watatoa mkopo wa Dola za Marekani 550milioni na kuziwasilisha katika ofisi za Wizara ya Fedha wakati akijua kuwa siyo kweli.
Shtaka nne ambalo pia linamkabili Sinare ni kwamba inadaiwa kuwa Septemba 20, 2012 akiwa benki ya Stanbic eneo la Kinondoni, alighushi barua ya mapendekezo ikionyesha benki ya Standard ikishirikiana na benki ya Stanbic ya Tanzania watatoa mkopo wa Dola za Marekani 550milioni kwa Serikali ya Tanzania kwa ada ya uwezeshaji ya asilimia 2.4 ya kiasi cha mkopo huo wakati akijua kuwa sio kweli.
Katika shtaka la tano ilidaiwa kwamba Agosti 21, 2012 Sinare kwa lengo la kulaghai aliwasilisha nyaraka za uongo Wizara ya fedha kuonyesha kuwa benki ya Standard ya UingEreza ikishirikiana na benki ya Stanbic ya Tanzania watatoa mkopo wa Dola za Marekani 550 milioni kwa Serikali ya Tanzania kwa ada ya uwezeshaji ya asilimia 2.4 ya kiasi cha mkopo huo wakati akijua kuwa siyo kweli.
Katika shtaka la sita, Wakili Tibabyekomya alidai kuwa wakiwa makao makuu ya Benki ya Stanbic Kinondoni, washtakiwa wote kwa nia ya kudanganya walighushi waraka wa makubaliano Novemba 5, 2012 kuonesha kuwa Stanbic Tanzania imeingia makubaliano ya ushirikiano na kampuni ya Enterprise Growth Market Advisors (Egma) Limited kuwezesha upatikanaji wa mkopo wa Dola za Marekani 550 milioni kwa ajili Serikali ya Tanzania. Shtaka la saba, linawakabili washtakiwa hao kwamba Machi 2013 jijini Dar es Salaam, washtakiwa kwa pamoja walijipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kiasi cha Dola za Marekani 6 milioni kutoka serikalini, zikionyesha kuwa fedha hizo zilikuwa malipo ya ada ya uwezeshaji wa upatikanaji wa mkopo ambazo zililipwa kupitia Egma T Ltd.
Katika shtaka la nane, Wakili Tibabyekomya alidai kuwa kati ya Machi 2013 na Septemba 2015 washtakiwa wote walitenda kosa la kutakatisha fedha kwa kuhamisha, kuchukua na kuweka kiasi cha Dola za Marekani 6 milioni katika akaunti tofauti tofauti za benki.
Wakili Tibabyekomya alidai kuwa washtakiwa waliweka fedha hizo katika akaunti mbalimbali zilizomilikiwa na Kampuni ya Egma wakati walipaswa kufahamu kuwa fedha hizo ni mazao ya uhalifu wa kughushi.
Imeandaliwa na James Magai na Hadija Jumanne
2 comments:
wapumbavu hawa walikuwa wanajua nchi ni yao.. mcheki huyo mama anavyoangalia kwa dharau ngoja akanyee ndoo sasa.
Oh jamani sioi NILISOMA nae forodhani rafiki yangu mnoo.yaani wazazi wakiafrica na arranged marriage .sioi walim force kuoa mtoto wa Lowasa sasa jamani mbona hivi .sioi ebu achana Lowasa
Post a Comment