Mahakama ya Rushwa, ambayo iliahidiwa na Rais John Magufuli wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita, itaanza kufanya kazi Julai kwa kushughulikia kesi kumi ambazo uchunguzi wake umekamilika.
Mahakama hiyo imekuwa kwenye ilani ya CCM tangu mwaka 2010, lakini ilizungumzwa zaidi kwenye uchaguzi uliopita na Magufuli akaibeba kwenye kampeni zake wakati Taifa likipigia kelele ufisadi uliokithiri nchini.
“Napenda kulitaarifu Bunge lako kwamba, Serikali imeanzisha Divisheni ya Rushwa na Ufisadi ya Mahakama Kuu itakayoanza kufanya kazi Julai mwaka 2016,” alisema Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akiwasilisha hotuba Makadirio na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu bungeni jana.
Majaliwa alisema katika mwaka wa fedha wa 2016/17 Serikali itaendelea kuchunguza tuhuma 3,444 zilizopo na mpya zitakazojitokeza na kukamilisha uchunguzi wa tuhuma 10 za rushwa kubwa.
Waziri Mkuu Majaliwa alisema kuanzishwa kwa mahakama hiyo ni ahadi iliyotolewa na Magufuli wakati akilihutubia Bunge Novemba mwaka jana baada ya kuapishwa.
Januari mwaka huu, Rais Magufuli alimtaka Jaji Mkuu, Othman Chande kutosubiri Bunge kupitisha Sheria ya Uanzishwaji wa Mahakama ya Mafisadi, badala yake waanze maandalizi ya kuiendesha mahakama hiyo.
Alisema kuchelewesha kuanza kwa mahakama hiyo, kunatoa mwanya kwa mafisadi kuendelea kuangamiza nchi na kuifanya kuwa maskini wakati ina rasilimali za kutosha ambazo zinaweza kuiendesha nchi bila kutegemea fedha za wafadhili.
Tangu aapishwe Novemba 5, 2015, Rais Magufuli amekuwa akipambana na wakwepaji kodi, wazembe, watumishi wanaoshindwa kusimamia fedha za umma, wezi na wabadhirifu.
Rushwa kwenye miradi ya maendeleo
Kwa upande wa rushwa kwenye miradi ya maendeleo, Majaliwa alisema miradi 284 yenye thamani ya Sh41.63 bilioni ilikaguliwa kupitia ufuatiliaji wa miradi hiyo katika Serikali za mitaa.
“Miradi 69 yenye thamani ya Sh8.32 bilioni ilibainika kuwa na kasoro na miradi 10 wahusika walishauriwa namna ya kurekebisha kasoro,” alisema.
Hata hivyo, alisema uchunguzi wa kina wa miradi 59 umeanzishwa ili wahusika wachukuliwe hatua.
Pia, Majaliwa alisema ufuatiliaji maalumu wa miradi ya afya inayofadhiliwa na Benki ya Dunia (WB), unaendelea kufanyika na tayari hatua zimechukuliwa kwenye maeneo yaliyobainika kuwa na kasoro.
Alisema hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuanzisha uchunguzi wa awali ambao umefanikisha majalada 85 kufunguliwa.
Akizungumzia mwaka uliopita wa fedha wa 2014/2015, Majaliwa alisema Serikali imeshughulikia tuhuma 3,911 na tayari uchunguzi wa tuhuma 324 ulikamilika. Alisema kati ya tuhuma hizo, majalada 252 yaliombewa kibali kwa Mkurugenzi wa Mashtaka na 156 yamepata kibali cha kuwafikisha watuhumiwa mahakamani. “Majalada 329 yaliyotokana na taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali yalichunguzwa. Majalada 19 yalikamilika na kuombewa kibali kwa Mkurugenzi wa Mashtaka na 12 yalipata kibali cha kuwafikisha watuhumiwa mahakamani,” alisema.
Alisema katika kipindi hicho majalada manane yanayohusu rushwa kubwa yalifikishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka.
“Kati ya hayo majalada mawili yamepata kibali na watuhumiwa wamefikishwa mahakamani,” alisema Majaliwa.
Aidha, alisema Serikali katika mwaka ujao wa fedha, itaimarisha ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ili kwa pamoja ziweze kuharakisha utoaji wa haki.
Migogoro ya ardhi
Majaliwa alisema tayari Serikali imechukua hatua kali dhidi ya maofisa ardhi waliokiuka sheria na taratibu za usimamizi wa ardhi nchini.
Alisema hiyo ni pamoja na kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi. Alitoa mfano wa maofisa ardhi waliochukuliwa hatua kuwa ni wa halmashauri za majiji ya Mwanza, Arusha, Manispaa za Bukoba na Kahama na kutengua uteuzi kwa maofisa ardhi.
Mifuko ya hifadhi ya jamii
Majaliwa alisema Serikali imefanya tathimini kwa mifuko ya GEPF, LAPF, NHIF, NSSF, PPF na PSPF kwa lengo la kupima uendelevu wake na kubainisha bado ni endelevu ikiwa na raslimali za thamani ya Sh8.8 trilioni. Alisema Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii imetoa miongozo ya kupunguza gharama za uendeshaji wa mifuko ya jamii itakayoanza kutumika Julai 2016.
Kuhusu deni la PSPF, alisema Serikali inakamilisha uhakiki wa madeni ya mfuko huo kabla ya kuanzishwa mwaka 1999 yenye thamani ya Sh2.9 trilioni.
“Hadi sasa Serikali imelipa sehemu ya deni la PSPF kiasi cha Sh180 bilioni ili kuhakikisha kwamba mafao ya wastaafu wa mfuko wanalipwa kwa wakati,” alisema.
Pia, alisema Serikali inaendelea kulipa deni la Sh840.4 bilioni iliyogharamiwa na mifuko ya GEPF, LAPF, NHIF, NSSF na PPF.
Uchaguzi Mkuu 2015
Kuhusu Uchaguzi Mkuu uliopita, Majaliwa aliiagiza Tume ya Uchaguzi (NEC), kufanya tathmini ya kina kubaini sababu zilizowafanya wapigakura zaidi ya milioni saba waliojiandikisha kutotumia haki yao ya kikatiba.
“Hii itasaidia kuboresha chaguzi zijazo kwani wananchi wana wajibu wa kutumia haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi wanaowataka,” alisema.
Alisema tathmini hiyo itasaidia kubaini iwapo kuna vikwazo vinavyozuia baadhi ya watu kupiga kura ili waviondoe.
Ofisi ya Waziri Mkuu imeomba kuidhinishiwa Sh236.75 bilioni, kati ya hizo Sh71.56 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh165.19 bilioni kwa maendeleo
1 comment:
What is this a.. hole think he is doing?
Post a Comment