ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, April 27, 2016

MBWA HUUA WATU 1,600 KILA MWAKA

Watu 1,600 hususan watoto hufa nchini kila mwaka kutokana na ugonjwa wa kichaa cha mbwa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Mary Mashingo alisema vifo hivyo hutokana na watoto kukosa chanjo kwa wakati dhidi ya ugonjwa huo.
“Tuna vituo saba pekee hapa nchini vinavyotoa huduma hizo,” alisema Dk Mashingo.
Alitaja mikoa ambayo vituo hivyo vipo kuwa ni Dar es Salaam, Tabora, Mwanza na ile ya kusini mwa Tanzania.
Hata hivyo, alisema baadhi ya watu huzembea kwenda kwenye vituo vya afya kupata chanjo hiyo na kwamba wizara imepanga kutumia maadhimisho ya Siku ya Vetenari Duniani yatakayofanyika Aprili 30, kutoa elimu kuhusu suala hilo.
Alisema katika kuadhimisha siku hiyo wataongeza kasi ya kujiendeleza kitaaluma kwa lengo la kukabiliana na ugonjwa huo.
Dk Mashingo alisema taaluma ya tiba ya mifugo (vetenari) inazidi kubadilika, hivyo wataalamu wanapaswa kujiendeleza ili wawe na maarifa ya kutosha, ujuzi na weledi wa kutumia teknolojia ya kisasa.
Katibu mkuu huyo aliongeza kuwa taaluma hiyo ina nafasi muhimu katika kulinda afya ya binadamu na wanyama nchini.
Alisema wataalamu hao wanapaswa kushughulika na udhibiti wa magonjwa yanayoambukiza wanyama na binadamu.
Dk Mashingo alisema katika maadhimisho hayo yatakayofanyika Jumamosi wiki hii, wizara itatoa chanjo kwa mbwa ili kuwakinga na kichaa cha mbwa.
Akizungumzia ugonjwa huo, mkazi wa Ilala, Dar es Saalam, Juma Hamdun aliiomba Serikali kujikita kutoa elimu kwa wananchi ya namna ugonjwa ulivyo na dalili zake.

No comments: