ANGALIA LIVE NEWS

Friday, April 8, 2016

PPRA wamjaribu Magufuli


Hali hiyo imejitokeza baada ya Mkuu wa Kitengo cha Sheria wa PPRA, Bertha Soka, kuendelea na shughuli za utumishi wa umma wakati amejumuishwa katika kesi inayowakabiliwa wakurugenzi wa zamani wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), David Mattaka na wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi ya Umma, Dk. Ramadhan Mlinga wanaokabiliwa na shtaka la uhujumu uchumi na kuisababishia serikali hasara.

Katika kesi hiyo, shtaka la sita ndilo linalowatia matatani kutokana na kudaiwa kuwa Machi 19, 2008 katika Ofisi za PPRA zilizopo Wilaya ya Ilala, Dk. Mlinga na Soka, walighushi mwenendo wa kikao wa tarehe hiyo, wakionyesha kwamba mamlaka hiyo ilikaa kikao na kujadili maombi ya kuidhinisha ATCL kukodisha ndege.

Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Dk. Laurent Shirima, alikiri ni kweli Soka anatuhumiwa na ameshafikishwa mahakamani, lakini bado anaendelea na utumishi kutokana na bodi kumruhusu.

Akizungumza kwa njia ya simu na Nipashe, Dk. Shirima alisema kwa mujibu wa taratibu za utumishi wa umma mwajiri ni bodi ambayo ilikaa hivi karibuni na kuangalia sheria na kanuni za utumishi.

"Bodi ilikaa, sikumbuki tarehe, lakini pamoja na mambo mengine iliangalia na kupitia sheria na kanuni za utumishi wa umma ikaona hakuna sababu ya kumsimamisha kazi Soka... pia, iliona kumsimamisha kazi wakati anaendelea kulipwa, serikali inaingia hasara kubwa," alisema na kuongeza:

"Bodi imeona yale yanayomkabili yalitokana na kuwajibika kupitia nafasi yake na kwamba haitaathiri utendaji wala maslahi ya taifa wakati akiendelea na kesi yake," alisema Dk. Shirima.

Akifafanua zaidi, alisema yeye kama mkurugenzi hana makali zaidi ya bodi, na kwamba imeamua hivyo hana sababu ya kupingana nayo.

Mahojiano kwa njia ya simu kati ya Nipashe na Dk. Shirima;
Nipashe: Mheshimiwa vipi kuhusu suala la Mkuu wa Kitengo cha Sheria kuendelea na kazi wakati anatuhumiwa, na kesi iko mahakamani?

Dk. Shirima: Taratibu za mtumishi anapokuwa na tuhuma zinakuwa chini ya mwajiri wake ambaye ni bodi, na imeshakutana.

Nipashe: Uamuzi wa bodi unasemaje?

Dk. Shirima: Bodi imepitia yale yanayomkabili, imeona yanatokana na kuwajibika kupitia nafasi yake ya kazi, hivyo imeona haina sababu ya kumsimamisha kazi kwa kuwa wanaendelea kumlipa mshahara.

Nipashe: Lakini mheshimiwa sheria za utumishi wa umma zinaruhusu hayo yaliyofanywa na bodi?

Dk. Shirima: Bodi ndiyo ina mamlaka na imejiridhisha, mimi kama mkurugenzi sina uwezo wa kupingana na uamuzi wake.

Nipashe: Unaweza kunisadia hivyo vifungu vya sheria na kanuni vilivyotumika kumruhusu kigogo huyo kuendelea na kazi wakati akiwa mtuhumiwa?

Dk. Shirima: Siwezi kukumbuka sheria na kanuni hizo, lakini nenda kwenye ofisi yoyote ya uombe sheria za utumishi wa umma utazisoma, sisi watumishi tunalindwa na taratibu za utumishi wa umma.

Kwa upande wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angela Kairuki, alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa suala hilo, alisema hausiki nalo kwa kuwa PPRA iko chini ya Wizara ya Fedha.

"Mimi sihusiki na suala hilo kwa kuwa PPRA iko chini ya Wizara ya Fedha ndiyo wenye kujua..." alisema Waziri Kairuki.
Alipoulizwa kuhusu wizara yake kuwa na dhamana na masuala ya utumishi wa umma, bado alisisitiza kuwa suala la mtumishi wa PPRA kuendelea na kazi wakati ni mtuhumiwa halina mahusiano na wizara yake.

Hata hivyo, gazeti hili lilipokwenda Wizara ya Fedha kwa ajili ya kupata ufafanuazi wa suala hilo, halikufanikiwa kumpata waziri, naibu wake, katibu mkuu wala mkurugenzi wa utawala kwa madai kuwa walikuwa na vikao kwa ajili ya bajeti.

"Kwa sasa waheshimiwa wako kwenye vikao labda uache maswali na tutayawasilisha kwa mabosi ..." alisema Ofisa Habari wa wizara hiyo, Eva Valeriani, ambaye hajatoa majibu ya maswali hayo mpaka habari hii inakwenda mtamboni.
Juhudi za kupata ufafanuzi wa wizara hazikuishia hapo, kwani Nipashe lilimtumia ujumbe mfupi Katibu Mkuu Dk. Servacius Likwelile, ambaye alijibu 'nimeambiwa uliwauliza PPRA na walikupatia maelezo.

Kwa mujibu wa Kanuni za kudumu za utumishi wa umma ya mwaka 2009 kifungu cha F34 na 35 vinaeleza:

F34, Mtuhumiwa anaweza kuondolewa kwenye majukumu yake kiutawala. Kama inafikiriwa kumuacha mtuhumiwa aendelee na majukumu yake, hasa jukumu maalum alilokabidhiwa kutapelekea kutendeka kwa kosa au vinginevyo kwa maslahi ya umma, anapaswa kuondolewa mara moja kwenye majukumu hayo ama jukumu hilo maalum likisubiriwa matokeo ya uchunguzi wa polisi ama mamlaka ya kinidhamu.

Hatua hii inapobidi kuchukuliwa kiutawala, yaani bila mkondo wa kisheria, hautaathiri mshahara wake.

F35, Kusimamishwa (1) Pale mtumishi wa umma anapohukumiwa kwa kosa la jinai, mamlaka ya kinidhamu inaweza kumsimamisha kutekeleza mamlaka na majukumu ya ofisi yake, ikisubiriwa matokeo ya mashtaka ya kinidhamu dhidi yake.

(2)Mtumishi wa umma aliyesimamishwa hatastahili kulipwa mshahara kutokea tarehe aliposimamishwa, ila atalipwa na mwajiri wake malipo sawa na moja ya tatu ya jumla ya malipo yote ya mwezi.

CHANZO:NIPASHE

No comments: