Mkuu wa Mkoa wa Rukwa,
Zelothe Steven amemwagiza Kamanda wa Polisi mkoa huo, Jacob Mwaruanda kuwasaka
na kuwakamata watumishi hewa 18 waliobainika katika uhakiki uliofanyika katika
halmashauri zote mkoani humo hivi karibuni.
Pia ameagiza fedha hizo zilizolipwa kwa watumishi hao hewa na kuiingizia hasara
kubwa Serikali zirudishwe mara moja. Akifafanua alisema katika uhakiki huo, watumishi hewa tisa walibainika katika
wilaya ya Nkasi, wanane katika Manispaa ya Sumbawanga na mmoja wilaya ya
Sumbawanga wakati Kalambo ikiwa haina mtumishi hewa.
Uhakiki huo unatokana na maagizo aliyotoa Rais John Magufuli baada ya
kuwaapisha wakuu wa mikoa aliowateua, aliwaambia wakafanye kazi ya kutatua kero
za wananchi na sio kwenda kufanya siasa. Pia Rais Magufuli aliwapa wakurugenzi wa halmashauri siku 15 wawatoe katika
orodha ya malipo ya mshahara wafanyakazi hewa wote katika halmashauri zote
nchini.
Zelothe alitoa agizo hilo jana katika kikao maalumu cha kufahamiana
kilichojumuisha wazee, viongozi wa dini , watendaji wa umma na wajumbe wa
kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo kilichofanyika mjini hapa. Alisisitiza kuwa hajaridhishwa na uhakiki huo, hivyo akaagiza halmashuri zote
kurudia upya uhakiki wa watumishi.
“Siku ile ile nilipoapishwa kabla sijavuka geti kutoka nje ya Ikulu nilipiga
simu na kuagiza halmashauri zote (Manispaa, Nkasi, Kalambo na Sumbawanga)
kuanza uhakiki mara moja wasinisubiri hadi niripoti mkoani hapa,” alieleza.
Aliongeza kuwa aliporudi mkoani humo na kuripoti kazini katika siku yake ya
kwanza ofisini alikabidhiwa kitabu chenye orodha ya watumishi wa umma wa
halmashauri zote akielezwa kuwa hakuna mtumishi hewa katika mkoa wa Rukwa.
“Sikukubaliana nao nilikataa, nikaagiza ufanyike uhakiki mara moja ndipo wamepatikana
watumishi hewa 18 na watumishi wengine 137 wapowapo tu wakiwa na taarifa
zinazotia mashaka. Wote wamebainika kwenye hicho kitabu nilichokabidhiwa
kikionesha hakuna mtumishi hewa,” alisisitiza.
Chanzo: Habari Leo
2 comments:
Mwanzo mzuri,Je waliokuletea report ya Kwanza wachukuliwe hatua kwa report ya uongo.
Mwanzo mzuri,Je waliokuletea report ya Kwanza wachukuliwe hatua kwa report ya uongo.
Post a Comment