ANGALIA LIVE NEWS

Friday, April 8, 2016

Chunga namba hizi hatari, Yanga yaambiwa

23: Idadi ya wachezaji wa Al Ahly waliotarajiwa
By Oliver Albert, Mwananchi ;oalbert@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati Al Ahly ilitarajiwa kutua nchini jana usiku kuikabili Yanga Jumamosi kwenye mchezo wa raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, timu hiyo ikiwa na jeshi kamili la wachezaji 23, chini ya kocha wa zamani wa Tottenham ya England, Martin Jol inaipa nafasi kubwa mechi hiyo ambayo kwao inaonekana kama vita.

Hata hivyo, itakuwa vita ya mbinu sahihi za makocha Wadachi, Hans Pluijm (Yanga) na Martin Jol (Ahly), wenye ubora na rekodi tofauti.

Vyombo mbalimbali vya habari vya Misri, juzi na jana vilifichua siri nzito ambazo kocha Pluijm hana budi kuzifanyia kazi mapema kabla ya mchezo huo.

Siri hizo ni pamoja na falsafa ya Mdachi huyo aliyetua Ahly miezi miwili iliyopita, alivyoibadili timu na kurejeshea soka la kumiliki mpira kwa muda mrefu, pasi nyingi pia kuangalia makosa ya mpinzani na kuyatumia kupata mabao.

Pia, ina baadhi ya wachezaji hatari kwenye kikosi chake walioteuliwa na kocha Jol kwa safari ya kuikabili Yanga wakipewa kazi maalumu.

Nyota hao ni; viungo, Abdalla El-Said, Moemen Zakareya, mwenye jezi namba nane, ambao ni wazuri kwenye ufungaji wa mabao.

Gazeti la Al Ahram lilimtaja kiungo El-Said, jezi namba 19 kuwa ni mjuzi wa mabao ya faulo, ambaye Al Ahly inamtegemea kwenye mipira iliyokufa, ambayo katika mechi zilizopita imeipa timu yake mabao muhimu. Mbali ya hao, yupo mshambuliaji raia wa Gabon, Malick Evouna, anayevaa jezi namba 15 mgongoni. Yeye, ndiye kinara wa mabao wa klabu hiyo ambayo ina rekodi ya kutwaa mataji kwa ngazi ya klabu Afrika.

Evouna, kulingana na gazeti hilo alisajiliwa na Ahly katika dirisha dogo, amecheza mechi 15 na kufunga mabao saba kwa klabu hiyo.

Kikosi kamili Al- Ahly

Makipa: Sherif Ekramy, Ahmed Adel, Mosad Awad.

Walinzi: Ahmed Fathi, Bassem Ali, Mohamed Hani, Saad Samir, Rami Rabia, Ahmed Hagazy, Sabri Rahil.

Viungo: Hossam Ghaly, Hossam Ashour, Amr El-Sulaya, Ahmed El-Sheikh, Walid Soliman, Moemen Zakareya, Ramadan Sobhi, Abdalla El-Said.

Washambuliaji: Malick Evouna, Amr Gamal, Emad Meteb.

Kauli ya Mwambusi

Wakati hayo yakiendelea ndani ya Ahly, kocha msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi alisema wataitumia kambi ya Pemba kumaliza tatizo la kukosa nafasi kabla ya kuikabili Al Ahly, Jumamosi.

Yanga iko kisiwani Pemba ilikoweka kambi ya takriban wiki ili kujiandaa na mchezo huo dhidi ya Al Ahly ya Misri utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaaam. Kutokana na timu hiyo kutengeneza nafasi nyingi na kushindwa kuzitumia kikamilifu katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu dhidi ya Kagera, Mwambusi alisema sasa ni wakati sahihi wa kulifanyia kazi hilo kabla ya kupambana na Waarabu hao.

Alisema wanacheza nyumbani, hivyo lazima wahakikishe wanatumia nafasi wanazopata kwa kupata mabao mengi ili iwe kazi rahisi watakapokwenda ugenini nchini Misri wiki mbili zijazo.

Alisema tatizo la kushindwa kutumia nafasi nyingi za kufunga wanazopata uwanjani limekuwa sugu ndani ya timu yake. Hivyo watahakikisha wanakazania mazoezini na kulimaliza ili kuhakikisha Al Ahly inafungwa mabao mengi.

“Tumeweka kambi Pemba kwa sababu ni eneo tulivu na litatusaidia kujipanga vizuri kwa ajili ya mchezo ujao ambao ni mgumu.

“Katika mazoezi yetu ya huku, tutarekebisha kasoro ndogondogo tulizoziona kwenye kikosi chetu, lakini kubwa ni wachezaji kushindwa kutumia nafasi, kwani hata katika mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar tulistahili kushinda mabao mengi,” alisema Mwambusi.

No comments: