ANGALIA LIVE NEWS

Monday, April 25, 2016

RIPOTI YA CAG KUWASILISHWA DODOMA LEO

Hali ya hewa katika Bunge la kwanza la Bajeti ya Serikali ya Awamu ya Tano huenda ikachafuka kuanzia leo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) atakapowasilisha ripoti yake ya ukaguzi mwaka 2014/15 huku ikielezwa kwamba imebainisha madudu mengi.
Taarifa hiyo inatarajiwa kujadiliwa katika mkutano wa Bunge unaoendelea sambamba na majibu ya awali ya Serikali kuhusu kasoro katika matumizi ya fedha za umma zitakazobainishwa na CAG huku Kamati za Bunge; ya Hesabu za Serikali (PAC) na ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), zikitarajiwa kutoa taarifa ambazo zitakuwa mwongozo wa mjadala bungeni.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya kamati hizo mbili, zinasema ripoti hiyo ya CAG imeibua madudu mazito katika mashirika ya umma, taasisi za Serikali na wizara jambo ambalo linaweza kusababisha baadhi ya watendaji kukumbana na panga la Rais John Magufuli.
Imeelezwa kwamba ripoti hiyo imeibua suala la watumishi hewa ambao mpaka sasa Serikali imewabaini zaidi ya 7,700 sambamba na ufisadi katika mamlaka za Serikali za Mitaa.
Hata hivyo, Naibu Katibu wa Bunge, John Joel alisema jana kuwa CAG anapotoa ripoti hiyo haina maana kuwa kila alichokisema ni sahihi.
“Yeye (CAG) anakuwa na shaka tu ambayo ni lazima ithibitishwe katika majibu ya Serikali. Serikali itatoa majibu yake bungeni kuhusu hoja mbalimbali na majibu hayo yatathibitishwa na kamati za PAC, LAAC na Msajili wa Hazina ambao nao watatoa maelezo yao,” alisema Joel.
Tangu Rais mstaafu, Jakaya Kikwete aliporidhia taarifa ya CAG kuwasilishwa bungeni kisha kujadiliwa na wabunge, baadhi ya vigogo wa Serikali wakiwamo mawaziri na watendaji wakuu ambao wizara na idara wanazoziongoza zilibainika kuhusika na upotevu mkubwa wa fedha za umma waling’olewa katika nafasi zao.
Katika mjadala wa mwaka 2012, mawaziri sita na naibu mawaziri wawili walitimuliwa kazi yakiwa ni matokeo ya mjadala mkali bungeni wa ripoti ya CAG ya 2010/2011.
Mawaziri waliotoswa wakati huo na wizara zao katika mabano ni Mustafa Mkulo (Fedha), William Ngeleja (Nishati na Madini), Dk Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), Omary Nundu (Uchukuzi), Dk Cyril Chami (Viwanda na Biashara), Athuman Mfutakamba (Naibu, Uchukuzi) na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Lucy Nkya.
Mbali na vigogo hao, pia fagio hilo liliwakumba wakurugenzi wakuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).

Kishindo cha ripoti
‘‘Ripoti imeanika masuala mengi ambayo si ajabu kuona yakiibua mjadala mzito ndani na nje ya Bunge. Ukizingatia utumbuaji wa majipu, bila shaka hali itakuwa mbaya sana kwa watumishi na watendaji wa Serikali,” alieleza mtoa taarifa kutoka PAC.

Ripoti ya 2013/14
Ripoti ya CAG ya mwaka 2013/14 ya ukaguzi uliofanywa katika taasisi 176 za Serikali Kuu, halmashauri 163 na mashirika ya umma 109, iliibua ufisadi mkubwa.
Katika ripoti hiyo CAG, Profesa Mussa Assad alisema ulibainika ukiukwaji wa matumizi ya utoaji wa misamaha ya kodi, kuendelea kwa mishahara hewa, usimamizi mbovu wa mipango miji, madeni ya Serikali katika mifuko ya hifadhi za jamii na Bohari Kuu ya Dawa (MSD), ukiwamo misamaha wa kodi iliyotolewa kwa mafuta yanayotumika migodini iliyotajwa kufikia Sh22.33 bilioni.
Ripoti hiyo iliyataja mashirika yanayosuasua kwa usimamizi wa uwekezaji wa Serikali kuwa ni Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) na Shirika la Reli Tanzania (TRL) ambayo yote yanahitaji ruzuku kutoka serikalini.
Katika ukaguzi wa mapato ya ndani, ripoti hiyo ilibaini kuwa taasisi zilizo katika mpango wa kubakiza maduhuli na hazikurejesha zilikuwa Sh32.74 bilioni, hivyo kuathiri utekelezaji wa kazi zilizokuwa zimepangwa na taasisi husika.
Katika mishahara hewa, taasisi hiyo ilieleza kuwa wafanyakazi walioacha kazi na kustaafu wameendelea kulipwa mishahara kupitia akaunti zao, licha ya Serikali kuwekeza katika mfumo wa Lawson kama njia ya kudhibiti hali hiyo.

No comments: