
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa maofisa watendaji wakuu wa kampuni binafsi nchini (CEOrt), Ali Mufuruki ameteuliwa kuwa mwenyekiti nwenza wa kamati maalumu ya Bunge la Uingereza ya kuchunguza manufaa ya misaada ya Taifa hilo kwa nchi za Afrika.
Uchunguzi huo unafanyika ikiwa ni sehemu ya kupanua wigo wa biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kimataifa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Mufuruki (56) alithibitisha taarifa hiyo na kueleza kuwa, kamati hiyo ilianza kazi jana katika ukumbi wa mikutano wa Bunge la Uingereza jijini London. Alisema baada ya kufanya uchunguzi kamati itawasilisha ripoti na ushauri kwa Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, Juni 23.
Kwa uteuzi huo, Mufuruki anafanya kazi na Mwenyekiti Mwenza Lord Stephen Green ambaye ni mwakilishi wa Bunge la Makabwela (House of Lords) na wajumbe wengine ambao ni Profesa Myles Wickstead na Lord Paul Boateng wa Uingereza na Balozi Darlington Mwape wa Zambia.
Katika mkutano wa jana wa kamati hiyo, uliwakutanisha wadau 17 kutoka mashirika na makampuni mbalimbali ikiwamo Benki ya Dunia (WB), Shirika la Misaada ya Nje la Uingereza (DFID), UNCTAD/WTO, Trademark East Africa, ITC na mengineyo.
Pia, walikuwapo wawakilishi wa kampuni binafsi zinazofanya biashara Afrika, mashirika mbalimbali ya utafiti wa biashara za kimataifa na wanasheria wa kimataifa.
No comments:
Post a Comment