ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, April 24, 2016

UKWAA HURU LA WAZALENDO TANZANIA LATOA TAMKO KUHUSU BUNGE LA BAJETI

Katibu wa Jukwaa Huru la Wazalendo Tanzania, Mtela Mwampamba akizungumza na waandishi wa habari leo, Ubungo mjini Dar es Salaam, kuhusu mwenendo wa Bunge la Bajeti na hatua ya Wabunge wa baadhi ya Vyama Vya upinzani kutoka nje ya ukumbi na kutotoa bajeti mbadala ya Kambi ya Upinzani. Kulia ni Mwanachama wa Jukwaa hilo, Simon Simalenga (Picha na Bashir Nkoromo).
 TAARIFA KAMILI NI IFUATAYO KAMA ILIVYOTOLEWA NA MWAMPAMBA
JUKWAA HURU LA WAZALENDO TANZANIA (JUHWATA)
TAMKO JUU YA MWENENDO WA SHUGHULI ZA BUNGE
Ndugu wanahabari poleni na majukumu ya kulihabarisha Taifa, ndugu wanahabari tulio mbele yenu ni wajumbe wa jukwaa huru la Wazalendo Tanzania ( JuhwaTa). Kama mnavyojua jukwaa huru la WAzalendo ni taasisi huru inashughulikia mambo mbalimbali ya kitaifa ikiwepo, Mijadala, Makongamano,Matamko na Elimu kwa umma kuhusiana na mambo mbalimbali ya kijamii,kisiasa na kiuchumi kwa maslahi mapana ya Taifa.

Leo tumewaita, Jukwaa likiwa na masikitiko makubwa kuhusu mwenendo wa shughuli za bunge, hususan bunge linaloendelea sasa pale Dodoma, bunge la bajeti, Kwa mujibu
wa Ibara ya 63 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inalitaja bunge kuwa ndio chombo kikuu ambacho kitakuwa na madaraka , kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri serikali na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake. Kumekuwepo na tabia kwa baadhi ya wabunge kususia mijadala,vikao na shughuli nyingine za bunge kwahiyo wamekuwa wakivunja katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara 63 (2) na kutupelekea wananchi kukosa fursa ya uwakilishi kutoka wa wale tuliwachagua huku wao wakiendela kupata stahiki zao kwa maslahi yao. Kwa mfano, Watanzania tunatambua kwamba kuna baadhi ya wabunge walisusia bunge maalum la katiba matokeo yake wananchi tukakosa mawazo mbadala kutoka kwao na walioumia ni wananchi wanyonge na sio wao.

Jukwaa linasikitika sana, Mnamo 22/04/2016, Kambi Rasmi ya Upinzani  Bungeni, ilishindwa kuwasilisha Mapendekezo Mbadala wa Bajeti Ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mujibu wa kanuni za bunge kwa visingizio vya kwamba serikali haina Mwongozo wa kuiongoza nchi, Serikali kubana sana Matumizi bila kuwashirikisha wao kama Wabunge na Hatua mbalimbali ambazo mh Rais John P Magufuli za  Kutumbua majibu hadharani bila kutoa mchakato  wa watumbuliwa wa ufisadi kujitetea kwanza. Wananchi tunaamini kabisa kuwa, Kambi Rasmi imeshindwa kuwasilisha na kutoka nje kwa sababu mosi, Mpango Uliowasilishwa Bungeni na serikali kupitia Waziri wa Fedha na Mapendekezo ya Bajeti Ya Ofisi Ya Waziri Mkuu, umepokelewa vema na wananchi  na wasomi  huku wakiupongeza kwani Mpango umejikita katika, Ujenzi wa reli ya kati kwa standard gauge, Kuboresha Makusanyo ya Kodi, Vita Vya Ufisadi na Ubadhirifu, n.k. Pili Kambi Rasmi inawezekana kabisa hawakuwa na Hoja ya kupinga na njia pekee ni kutoka nje kuunga mkono Mapendekezo ya serikali.

Ndugu wanahabari ikumbukwe, Utaratibu, michakato na kuonea haya dhidi ya Mafisadi kimekuwa ni kilio cha wananchi wengi na tunashukuru mh Rais kusikia kilio chetu na kuweza kutufuta machozi yetu kwa vitendo. Pia ikumbukwe nchi hii imeliwa na Mafisadi kwa kuendekeza Michakato na Utaratibu, na sisi kama wananchi hatutakubali michakato na taratibu katika kushughulikia mafisadi wa Taifa iendelee. Na katika kumuunga mkono mh Rais, siku ya hotuba ya uzinduzi wa bunge la 11,Mh Rais alituomba Wananchi wazalendo tumuunge mkono katika vita aliyoianzisha ya kupambana na Mafisadi, Kubana matumizi, Kurudisha nidhamu ya Utumishi wa Umma, Uchapakazi na Uzalendo na sisi kama wananchi wanyonge tunauunga mkono jitihada hizo na tunamwambia na kumtia moyo kwamba tupo nyuma yake katika vita hii ijapokuwa wapo wachache wanaojaribu kuirudisha na kuhujumu jitahada zako kwa maslahi yao binafsi na Mafisadi wanaowatumia.

Ndugu wanahabari, sote tunajua mh Rais alipokuwa akiomba ridhaa ya kuwatumikia wananchi alikuwa akitoa ahadi na viapombele mbalimbali na sasa mh rais amezidi kutekeleza ahadi zake kwa vitendo kwa wananchi aliowaahidi, mfano Kuwa na baraza dogo la Mawaziri, Elimu bure, Kubana Matumizi yasiyo ya lazima na kuelekeza fedha zitakazo okolewa kwenda kutatua kero sugu za wananchi wake, kupambana na Mafisadi nk. Sasa tunashangaa kuwekuwepo na baadhi ya watu wakiwemo wabunge kupinga na kuhujumu waziwazi juhudi na jitahada za utekelezaji wa ahadi za mh Rais. Kama vile Kubana matumizi ya fedha za bunge kwa wabunge kutosafiri kwenda nje ya nchi kwa kisingizio cha kwenda kukagua ujenzi wa balozi zetu ilihali tunajua wao sio mainjinia wa majengo na pesa hizo kuelekezwa katika kutengeneza madawati ya wanafunzi na kila mbunge wa jimbo atapewa madawati 600 kwa ajili ya jimbo lake. Hivyo tunaamini wabunge nao walitoa ahadi zao kwa wananchi wao kwahiyo tunaomba na tunawashauri wajikite katika kutekeleza ahadi walizowaahadi wananchi wao kuliko kufanya malumbano,hujuma dhidi ya jitihada za utekelezaji wa ahadi za mh Rais.

Sote tunajua kauli mbiu ya mh Rais ni “Hapa Kazi Tu”  anataka awamu ya tano watu wafanye kazi, lakini bunge  lilipokulinaoneshwa moja kwa moja kwenye television tulikuwa tukishuhudia mijadala isiyo na tija kwa taifa, na zaidi Bunge lilikuwa uwanja wa kampeni za kisiasa,Vijembe, Kejeli, Mipasho na Vitimbi mpaka kufikia wao wenyewe kuliita bunge, “ Silly Season” na wengine wakiliita Bunge Comedy hivyo bunge kukosa Tija kwa Taifa na kupoteza kabisa maadili na kusudio la wananchi kufuatilia mijadala ya bunge letu hadi wengine hususan vijana kuacha kufanya kazi na kutumia muda mwingi kuangalia bunge kujifunza yasiyokuwa na tija kwa Taifa letu. Sisi kama Jukwaa tunawashauri wabunge wasijikite kwenye bunge kuoneshwa live bali wapige kazi kwa mustakali wa maendeleo ya Watanzania, na Wananchi watajua tu. Imefikia hatua Wabunge wanagoma kuchangia hoja bungeni kwa sababu tu familia , marafiki, ndugu na jamaa zao hawatawaona live. Sababu nyingine ni kuwa serikali haina Mwongozo na inatumia inatumia mwongozo wa awamu ya nne, sheria sio vacuum ndio maana Mawaziri hata kama bado hawajapewa mwongozo bado wanaendelea kutumia instruments za mwongozo iliyopita na kupata mwongozo mpya na bora ni mpaka serikali ifanye utafiti.

Pia Ukawa wameendelea kuhujumu shughuli za bunge kwa kuwazuia wabunge wao wasiende kwenye kamati mbili za bunge za PAC na LAAT na kusabisha kamati hizo kukosa uongozi. Tunaishauri serikali nayo shughuli zake zote zitakazokuwa zinaenda moja kwa moja (live) zifanyike jioni au siku za mapumziko ya kitaifa.

Kwa kuhitimisha ndugu wana habari, tukirejea kauli ya Mh Mbowe na Ukawa wakijinadi kuwa mh Rais anatekeleza Ilani yao,sasa tunashangazwa na vitendo vyao vya ghafla vya kuanza kupinga na kujihujumu wao wenyewe kwa kutekelezwa kwa Ilani yao, tunapatwa na mashaka na nia yao katika Taifa hili na uenda wakawa wanatumika na Mafisadi na watu wasiokuwa na nia njema na taifa hili maana hata ile agenda ya ufisadi hatuisikii tena, Pia waache tabia ya kususa hata kama kasi ya Mh Rais ni kali ili tusiendelee kuwakosesha wananchi haki zao kama tulivyoona pale Zanzibar baada ya Chadema kuwashawishi Viongozi wa CUF kususia na  kuwazuia wana CUF  kushiriki uchaguzi  wa marudio na kuwapelekea kukosa uwakilishi ilihali wao wana wawakilishi ndani ya bunge.

Jukwaa tunaomba na tunatoa ushauri kwa Uongozi wa Bunge, kuchukua posho na ikiwezekana kukata mishahara ya wabunge wote wasioshiriki vikao na shughuli za bunge na fedha hizo zipelekwe kwenye matumizi mengine ya kutatua kero za wananchi ikiwemo upatikanaji wa chaki mashuleni.

Ndugu wana habari, Kuna baadhi ya watu pamoja na Wabunge wa Ukawa wakiongozwa na mh Mbowe, wamekuwa wakilalama kwamba Rais anakiuka katiba na sheria za kwa kubadili matumizi ya fedha. Sheria ya Usimamizi wa Bajeti {Appropriation Act ya 2015 (6) Waziri wa Fedha anapewa mamlaka ( Baada ya Maagizo au Mashauriano ya ndani ya serikali) Lakini pia Katiba inamruhusu Rais ndani ya miezi baada ya kuchaguliwa kuweza kubadili matumizi ya fedha . Bajeti ikishapitishwa inakuwa ya serikali na endapo itakuwa imezidi , fedha zile Waziri anaweza kuzipangia matumizi mengine au akasaini na Rais akatangaza maana ndiye anayewateua.

Jukwaa linaiomba serikali itusaidie maana wao wana mkono mrefu ili tujue dhamira zao ni nini? Ikiwa kama Mpango wa serikali ni Kutoa elimu bure, ikiwa Mpango ni kufufua Viwanda,Ikiwa Mpango ni Kubana Matumizi, Ikiwa Mpango ni Kupambambana na rushwa, ikiwa Mpango ni kujenga barabara, Ikiwa 41% ya Bajeti ni kwa ajili ya Maendeleo nk kama hawayataki haya kwa Watanzania, Je hawa wana Agenda gani nyuma?
Mwisho Mh Rais alitoa Rai, “Atakayejaribu kumkwamisha Atakwama Yeye

Imetolewa 24/04/2016 na :-
MTELA MWAMPAMBA 0755 17 89 27­, 0627 94 95 15
KATIBU JUKWAA HURU LA WAZALENDO TANZANIA 

1 comment:

Anonymous said...

Asante kada. Naona zile fujo za skuli unaziendeleza. Nafasi za ukuu wa Wilay zimebakia ngapi? Au kuna za halmashauri? Kwa mtizamo sioni kikubwa zaidi ya kutafuta kusikika nawe umetoa tamko, kwani maelezo yako yote pamoja na kuchafua hali ya hewa, mheshimiwa Rais anafanya kazi yake na hata kama kwa pupa yote haya aliyakuta huko Iksuslu na ilikuwa ni uharibifu mkubwa wa wale wale ndani ya CCM! Mheshimiwa hafanyi tu bila kujua na kwa ujumla kama angeliingia ndfani zaidi utakuta uongozi mkubwa ndani ya awamu aliyoopokea ina husika kwa asilimia 80 bila ubishi. Ni wale waleeh.

mpita njia