Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mkoa wa Dar es Salaam
kimelaani kauli iliyotolewa na Mbunge wa CCM, Goodluck Mlinga kuwa ili
wanawake wapate nafasi ndani ya chama hicho lazima waitwe ‘baby’ neno
linalomaanisha kutumiwa kimapenzi.
Hivi karibuni akichangia
mjadala wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mlinga ambaye ni Mbunge wa Ulanga
Mashariki alitoa kauli hiyo iliyoibua mtafaruku bungeni na kusababisha
wabunge wanawake wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutoka nje ya
ukumbi huo baada ya kunyimwa mwongozo na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson.
Akizungumza
jana nje ya eneo la Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), akiwa na
viongozi wenzake walipokwenda kuchangia damu, Katibu wa Chadema Dar es
Salaam, Henry Kileo alisema wamesikitishwa na kauli hiyo ya mbunge
aliyepewa dhamana na kuaminiwa wananchi.
Alisema ili uwe mbunge
wa viti maalumu ndani ya Chadema, kuna hatua nne za kupitia ikiwamo
wanawake wenyewe kuchaguana ngazi ya wilaya kupitia Baraza la Wanawake
la Chadema (Bawacha), hivyo siyo rahisi kuwa na kitu kama hicho cha
uhusiano wa kimapenzi.
Kileo alisema: ‘‘Lakini cha ajabu nimeshangaa hata wenzetu upande wa pili CCM wamekaa kimya bila kutoa kauli ya kukaripia.’’
Alisema Chadema Mkoa wa Dar es Salaam, inaungana na wabunge wanawake wa Ukawa kupinga kauli hizo za kihuni.
Kuhusu
suala la damu, Kileo aliwataka Watanzania kujenga tabia ya kuchangia
damu ili kuokoa maisha ya wengine waliolazwa katika hospitali na vituo
vya afya nchini.
“Chadema Dar es Salaam, tumeonyesha mfano
tunaviomba vyama vingine viige mfano huu ili tuwasaidie watu wenye
mahitaji ya damu,” alisema Kileo.
Alisema zaidi ya wanachama 40 wakiwamo viongozi wa Chadema wamechangia damu na kwamba mchakato huo utakuwa wa mara kwa mara.
Mbunge
wa VitiMaalumu, Ruth Molel alisema wabunge wa Chadema wanaoteuliwa wana
taalumu zao na hawabahatishi kupata nafasi hizo kama Mlinga
anavyodhani.
“Nimeumia nilivyosikia kauli hii ikitolewa na kijana yule ambaye ni kama mwanangu, kiukweli hajatutendea haki kina mama.Inaonyesha jinsi gani bado ana fikra za mfumo dume,”alisema Molel.
Ofisa
Habari wa MNH, Neema Mwangomo alisema kwa siku hospitali hiyo inahitaji
damu kwa wastani uniti 80 hadi 100 lakini zinazopatikana ni 40.
Hata
hivyo, Mwangomo aliwashukuru viongozi Chadema kwa moyo wao na kuwataka
Watanzania wengine kujitokeza kutoa damu katika hospitali hiyo.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake