Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema uzito wa Rais John
Magufuli kumwajibisha Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga
kutokana na kutajwa kuhusika na Kampuni ya Lugumi inayodaiwa kulitapeli
Jeshi la Polisi, utasababisha waanze harakati za kumng’oa Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu
Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu aliwaambia waandishi wa habari
jana kuwa Rais John Magufuli hana budi kuchukua hatua haraka
kumwajibisha Waziri Kitwanga kama alivyofanya kwa watumishi wengine wa
umma katika operesheni ya kutumbua majipu.
Waziri Kitwanga
anadaiwa kuwa na hisa kwenye Kampuni ya Infosys Ips Tanzania Limited
ambayo ilipewa zabuni ya kutoa huduma za kitaalamu na Kampuni ya
Kimarekani ya Biometrica kuhusu uwekaji wa mashine za kielektroniki za
kuchukua alama za vidole kwenye vituo 108 vya polisi.
Mkataba wa kuweka
mashine hizo uliingiwa kati ya Jeshi la Polisi na Kampuni ya Lugumi
Enterprises ambayo ililipwa Sh34 bilioni kati ya Sh37 bilioni za
mkataba, wakati kazi ya kufunga mashine hizo ilifanyika kwenye vituo 14
tu hadi wakati Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
alipofanya ukaguzi.
Hata hivyo, kampuni hiyo inadai kuwa
Kitwanga, ambaye ni mmoja wa waasisi wa Infosys, alijiondoa kwenye
uendeshaji tangu mwaka 2010, wakati mkataba huo ulisainiwa mwaka 2011.
Chadema bado inaona kuwa Rais Magufuli anatakiwa kumwajibisha waziri huyo wa Mambo ya Ndani.
“Kama
Rais akishindwa kuchukua hatua katika hili, Serikali itang’oka
madarakani. Sisi Chadema tutaiondoa. Haiwezekani wakati Lugumi
inachunguzwa mhusika mkuu (Kitwanga) aendelee kuwa waziri, tena wa
wizara inayohusika na mkataba wa Lugumi,” alisema Mwalimu.
Mwalimu
alisema, Rais anapaswa kujitokeza hadharani na kueleza uhusiano wake na
Kitwanga na awaeleze Watanzania kuwa kutokana na uswahiba wao ndiyo
sababu ya kutomchukulia hatua.
“Mbona anawatumbua marafiki wa
wenzake? Kwa nini marafiki zake anashindwa kuwatumbua? Ukiwa kiongozi
mwenye kubagua katika uamuzi ni hatari kwa uchumi wa Taifa, ni sawa na
baba anayewabagua watoto wake matokeo yake ni kuzalisha chuki tu.”
Licha
ya Mwalimu kutotaka kuweka wazi mpango huo, kwa mujibu wa Ibara ya 53
A(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, Bunge
linaweza kupitisha azimio la kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu
endapo itatolewa hoja kupendekeza hivyo.
Kwa mujibu wa Ibara hiyo, hoja
ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu inapaswa kuungwa
mkono na wabunge wasiopungua asilimia 20 ya wabunge wote.
Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni 372, kati yao wabunge wa upinzani ni 118.
“Hilo
tutalifanya iwapo tu Rais atashindwa kumwajibisha Kitwanga. Ila huyu
waziri naye anapaswa ajipime mwenyewe ili kumlinda bosi wake (Waziri
Mkuu). Afanye kama Edward (Lowassa-waziri mkuu mstaafu) aliamua
kujiuzulu wadhifa wake ili kumlinda Jakaya (Kikwete-Rais wa Awamu ya
Nne) kwa kosa ambalo yeye hakulifanya,” alidai Mwalimu.
Mwalimu
alidai kwamba Serikali imezuia matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya
Bunge kuhofia uchafu wa viongozi, likiwamo sakata la Lugumi.
“Ndiyo
maana tunasema CCM ni ileile maana wametumbua majipu, sasa imebaki
mitoki. Ni kama imewashinda maana ipo sehemu mbaya,” alisema.
Licha
ya mkakati huo wa Chadema, Aprili 19 mwaka huu, Kitwanga alisema kuwa hahusiki katika sakata hilo na juzi alijibu hoja ya
Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) lililomtaka ajiuzulu, akisema
hawezi kuwajibu watoto ili kuonyesha tofauti yake na wao.
Katika
maelezo yake, Mwalimu aliorodhesha utumbuaji ambao Rais Magufuli
ameufanya tangu aingie madarakani, ukiwamo wa watendaji waliofanya
vurugu tu katika vikao kwa kusisitiza kuwa ni ajabu kuona mpaka sasa
hajamchukulia hatua yoyote Kitwanga wakati ukweli uko wazi kuwa
anahusika na sakata la Lugumi.
Baada ya ripoti ya CAG kuibua udhaifu huo
kwenye mkataba, Kamati ya Hesabu za Serikali ya Bunge iliunda kamati
ndogo kufuatilia tuhuma hizo baada ya kutoridhishwa na maelezo ya Wizara
ya Mambo ya Ndani na Jeshi la Polisi kuhusu mkataba huo.
Kampuni
ya Infosys ni wakala wa kampuni maarufu duniani ya kutengeneza kompyuta
ya Dell, ikijihusisha na usambazaji wa vifaa hivyo, matengeneza na
utoaji huduma za kitaalamu.
Kaimu katibu mkuu huyo wa Chadema
alisema, chama hicho pia kinajipanga kuanza ziara yake nchi nzima na
ajenda kuu itakuwa kuanika mambo yote mabaya yanayofanywa na Serikali.
1 comment:
Akili za kichadema shida sana.
- kwanza tuonyeshe connection ya Kitwanga na Lugumi.hasa unaposema kuwa Infosys iliingia mkataba na Biometrica ya Marekani na sio Lugumi.
-Pili kama Kitwanga alijitoa Infosys 2010 na mkataba kati ya Biometrica na Infosys uliingiwa 2011, sasa Kitwanga anaingiaje japo?
Sasa ninaona ni kwanini Chadema waliona huyu jamaa (Mwalimu) hafai kuwa katibu mkuu wa chama.
Post a Comment