Chama cha Wananchi (CUF)
kimesema kitawashtaki Mahakama ya Kimataifa (ICC) viongozi wa Serikali
ambao walitumia mamlaka yao vibaya wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka
jana, wakiwamo Waziri wa Mambo ya Ndani na Mkuu wa Jeshi la Polisi
(IGP), Ernest Mangu.
CUF, chama kikuu cha upinzani visiwani Zanzibar
kinachodai kuwa mgombea wake wa urais alishinda kwenye uchaguzi huo
uliofanyika Oktoba 25, 2015, kimesema kwa sasa kinatumia kampuni mbili
za kisheria, moja ya ndani na nyingine ya nje, kuwasaidia katika
kushughulikia suala hilo.
Mbali na vigogo hao wawili wa Serikali, chama
hicho kimesema hatua hiyo pia itawahusisha viongozi na watumishi wa umma
ambao hawakuchukua hatua kwa dhuluma iliyofanywa kwa Wazanzibari wakati
na baada ya uchaguzi.
CUF imesema hatua hiyo itachukuliwa baada ya
jana kuzindua ripoti yake ya uvunjwaji wa haki za binadamu visiwani humo
wakati wa uchaguzi huo.
Mbali na kuwafikisha ICC, Mazrui alisema tayari
chama hicho kimeanza kuchukua hatua stahiki ili kuwafikisha viongozi
hao kwanza mbele ya Mahakama Kuu ya Tanzania kwa kutochukua hatua dhidi
ya uovu uliokuwa unafanywa Zanzibar wakati wa kipindi hicho.
Iwapo CUF
itatekeleza azima hiyo, itakuwa tukio la kwanza kwa Tanzania kupeleka
viongozi wake kwenye mahakama hiyo inayopingwa na viongozi wa Afrika
wanaodai kuwa wana vyombo vyao vya kushughulikia haki za binadamu.
Tayari viongozi wawili wa Kenya, Rais na makamu wake wameshafikishwa
kwenye mahakama hiyo, lakini kesi dhidi yao ilikosa nguvu baada ya
mashahidi kukataa kwenda kutoa ushahidi.
Katika Uchaguzi Mkuu uliopita,
mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Salim Jecha Salim alifuta matokeo
ya urais, wawakilishi na madiwani Oktoba 28, mwaka jana siku ambayo
alitakiwa atangaze mshindi wa mbio za urais.
Alifuta wakati matokeo ya
majimbo 31 kati ya 40 yameshatangazwa na kubakia majimbo tisa ambayo
matokeo yalishabandikwa vituoni.
CUF ilidai kuwa ilishinda na Jecha
alipotangaza uchaguzi wa marudio, chama hicho kilijitoa na hivyo CCM
kushinda viti vyote.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Naibu katibu mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alisema chama
chake kinakamilisha ripoti ya ukiukwaji wa wa haki za binadamu
uliofanywa wakati wa mchakato huo ambao chama hicho kina ushahidi wa
kutosha.
Alisema ripoti hiyo ina matukio yote yaliyotokea kuanzia
uandikishaji, kampeni, kuahirishwa kwa uchaguzi na hata kurudiwa.
“Hakuna mtu aliyechukuliwa hatua za kisheria
ili kutenda haki kwa waathirika,” alisema akizungumzia vitendo vya
wananchi kupigwa na askari, kurushiwa risasi za moto, kubambikiwa kesi,
mashambulizi yaliyofanywa na mazombi na uchomaji nyumba za wafuasi na
ofisi za wafuasi wa chama.
Shaweji Mketo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CUF
alifafanua kuwa licha ya viongozi hao wa wizara na Jeshi la Polisi
kuanza kushtakiwa kwenye mahakama za ndani, ICC itawahusisha watu wengi
zaidi.
Alisema juhudi za makusudi zimechukuliwa na chama hicho
kuwatafuta washauri wa masuala ya kisheria na uendeshaji wa ICC ili
kukusanya ushahidi wa kutosha utakaowatia hatiani wahusika wote.
“Waziri, IGP na baadhi ya askari watahusika. Tunayo majina yao na
uchunguzi wetu utakapokamilika tutawataja,” alisema Mketo.
Kuhusu waziri
atakayehusika kwenye mashtaka yatakayofunguliwa ICC endapo vigezo
vitatosha ni wale waliokuwa kwenye nafasi hiyo wakati hayo yakitokea.
“Zipo kampuni mbili zinatushauri na kutusaidia kukusanya ushahidi,”
alisema bila kuzitaja, lakini akafafanua kuwa moja ni ya nje na nyingine
ya ndani.
Alisema hazitaji majina kwa kuwa Serikali inaweza ikaingilia
kati na kukwamisha mchakato mzima.
Baada ya uzinduzi wa ripoti hiyo
uliofanyika jana, Mazrui alisema wamepanga kumuandikia barua Rais John
Magufuli na kumkabidhi nakala kwa kuwa ni Amiri Jeshi Mkuu, ajue
kinachoendelea ndani ya utawala wake.
Alisema ripoti hiyo pia itapelekwa
kwenye jumuiya, taasisi na mashirika ya kimataifa yanayotetea haki za
binadamu ulimwenguni.
Alisema CUF imebaini mipango ya Serikali ya
kutaka kuwakamata viongozi wake wa Zanzibar na “kuwaweka kwenye magereza
ya Bara ili kuwanyamazisha Wazanzibar”.
Ili kuongeza uwazi kwa
wanaharakati wa ndani, alisema ripoti ya chama chake sambamba na
vielelezo vyote muhimu, itapelekwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala
Bora, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Kituo cha Huduma za
Sheria Zanzibar (ZLSC) na taasisi nyingine zinazojishughulisha na
masuala ya haki za binadamu nchini.
Ili kuongeza uwajibikaji, alisema
jopo la mawakili wa chama chake linashirikiana na wanasheria wabobezi wa
kimataifa ili kukamilisha taratibu zitakazowezesha kuchukuliwa hatua
kwa watu wote ambao walichochea au walitoa maagizo yaliyosababisha
makosa dhidi ya binadamu.
“Tumeshamuandikia barua IGP na waziri. Hiyo ni
moja ya hatua muhimu kabla hujawashtaki,” alisema.
Waziri hakupatikana
kuthibitisha kupokea barua hiyo. IGP alisema hajaipata ripoti hiyo,
hivyo hawezi kusema chochote juu ya madai yaliyosemwa na CUF. “Nikiipata nitaijibu,” alisema kwa kifupi.
Naibu katibu mkuu wa CCM-Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema hujuma ni sehemu ya siasa za kila siku
visiwani humo.
Alibainisha kuwa chama chake ambacho kimekuwa
kikitangazwa mshindi tangu siasa za ushindani ziliporejeshwa mwaka 1992,
kimekuwa kikihujumiwa tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi na
kutoa rai kwa CUF kuchukua hatua kama ina uthibitisho.
“Makosa yote ya
jinai yanashughulikiwa na vyombo vya dola. Kinachohitajika ni ushahidi
wa kutosha,” alisema Vuai.
Pia alitahadharisha dhidi ya siasa za chuki
ambazo alisema zinaenezwa visiwani humo licha ya kuwa pazia la Uchaguzi
Mkuu limeshafungwa. “Wapo viongozi wanaenda misikitini kuhubiri
uongo… hii si sawa,” alisema.
Kuhusu hatua za zinazotarajiwa kuchukuliwa
na CUF alisema viongozi wa chama hicho wanajua kuwa wamekosea, hivyo
wanajaribu kutafuta namna ya kuwatuliza wanachama wao hasa wale
waliopoteza nafasi zao za uwakilishi kwenye Baraza la Wawakilishi.
“Viongozi wanahangaika. Jinamizi la kususia uchaguzi bado
linawaandama. Hawaeleweki na ndiyo maana wanajaribu kote kote,
Mahakamani na misikitini. Huko ni kutapatapa,” alisisitiza Vuai.
CHANZO: MWANANCHI
2 comments:
Hivi CUF haina wanasheria? You don't need to be a lawyer to recognize that the ICC route is not going anywhere. Hivi hawafahamu hata mamlaka/mandate ya ICC ni nini? Ama they are merely playing politics to be in the limelight? Wajinga kweli ndio waliwao?
Mkataba wa ICC upo wazi: Taifa liwe "unable or unwilling" ku posecute kesi hiyo. Wakati huo huo tunaambiwa hatua za kuwasilisha mashtaka hayo Mahakama Kuu ya Tanzania ndio ziko mbioni!!!? Sasa utasemaje Taifa utadhibitisha vipi Taifa halina uwezo ama dhamira wakati kumbe hata kesi haijafika mbele ya vyombo vya juu vya sheria? Ama ndio kuchanganya watu ili kudai "sisi Bwana tulifanya kila tuloweza bali Serikali imekula njama na wakubwa? Huhitaji mnajimu kujua hili la ICC halifiki mbali!!! Danganya toto tu!
Post a Comment