Na Benedict Liwenga, Dodoma.
SERIKALI imesema itaendelea kusogeza huduma za Zimamoto na Uokoaji kwa wananchi kwa jinsi hali ya upatikanaji wa fedha itakavyoruhusu.
Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mhandisi Hamad Masauni wakati akijibu swali la Mbunge wa Tunduma, Mhe. Frank Mwakajoka ambaye alitaka kujua ni lini Serikali itapeleka huduma za Zimamoto katika Mpaka wa Tunduma ili kuokoa mali za wafanyabiashara wanaosubiri kuvuka pindi ajali ya moto inapotokea.
Mhe. Msauni ameeleza kuwa, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma lina Kituo katika eneo la mtaa wa Kilimanjaro, Wilaya ya Momba katika Mkoa wa Songwe kinachohudumia Wilaya yote ukiwemo Mpaka wa Tunduma.
"Kwa sasa Kituo hiki kina gari moja lililopo matenegenzo Jijini Mbeya, hata hivyo askari wanaendelea kutoa elimu ya Kinga na tahadhari ya Majanga ya Moto na utumiaji wa vifaa vya huduma ya kwanza vya uzimaji moto", alisema Masauni.
Aliongeza kuwa, sambamba na ukaguzi wa majengo ya kutoa ushauri kwa kandarasi au makampuni ya ujenzi kuhusu ujenzi bora wa miundombinu yenye usalama kwa umma.
"Ni azma ya Serikali kupeleka huduma ya Zimamoto katika maeneo yote ya nchi ikiwemo Tunduma, hata hivyo azma hii nzuri inategemea na upatikanaji wa rasilimali fedha, Serikali itaendelea kusogeza huduma za Zimamoto na Uokoaji kwa wananchi kwa jinsi hali ya upatikanaji wa fedha itakavyoruhusu", aliongeza Masauni.
No comments:
Post a Comment