Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. |
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema vita inayoendeshwa na Serikali ya awamu ya tano dhidi ya wala rushwa na wale wanaofanya ufisadi siyo nguvu ya soda kama wengi wanavyofikiri.
“Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kupambana na wala rushwa na mafisadi. Wala hatutanii. Hawa tutacheza nao na wala wasidhani vita hii ni nguvu ya soda. Tutaendelea kuwasaka hadi tufike mwisho,” alisema Waziri Mkuu wakati akizungumza na Watanzania waishio Zambia katika mkutano uliofanyika kwenye Ubalozi wa Tanzania jijini Lusaka, Zambia juzi jioni (Jumanne, Mei 24, 2016).
“Hatutaki tabia iliyokuwepo ya mwananchi anakuja ofisini kutaka huduma lakini hasikilizwi hadi atoe chochote, sisi hiyo tabia hatutaki kuisikia kabisa. Tumedhamiria kurudisha heshima kwenye utumishi wa umma na nimeanza kupata faraja kwani sasa hivi (nimeambiwa) katika baadhi ya taasisi unasikia mtu akiulizwa una shida gani, nenda pale, jambo ambalo zamani halikuwepo, alisema.
Alisema Serikali imeamua kupigia debe dhana ya utumishi wenye uadilifu kwa sababu huo ni utamaduni mpya. “Ni kipindi kigumu kidogo cha mabadiliko lakini tumesimamia mabadiliko haya na ndiyo maana watumishi wote tumewasisitizia kuwa suala la uaminifu, uadilifu na uwajibikaji ni muhimu,” alisema na kuongeza:
“Hatutamvumilia mtumishi yeyote ambaye hatakuwa tayari kuwatumikia Watanzania au atakayeendekeza uzembe lakini pia hatutamuonea mtu yeyote. Hapa tunasisitiza usawa na hatutaki kutengeneza gap kati ya mwananchi mtumishi na wa mwananchi wa kawaida, tunataka kila mwananchi aione Tanzania ni nchi yake na kila kinachozalishwa ni sehemu yake. Tukifika hapo, tunaamini kila mmoja ataweza kuisemea nchi yake.”
Akizungumzia kuhusu ubadhirifu wa fedha za umma, Waziri Mkuu alionya kwamba Serikali imelipa kipaumbele suala la uaminifu na uadilifu kwenye fedha za Serikali na kwamba haitakuwa tayari kuona fedha hizo zikifujwa.
“Hivi sasa Serikali imetenga fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo na fedha hizo zitaenda vijijini. Tunataka zikafanye kazi iliyokusudiwa, na wale wadokozi wajue kuwa wamekalia kaa la moto,” alisema huku akishangiliwa.
Alisema watumishi wa umma wana wajibu wa kusimamia kazi zilizopangwa na kuhakikisha miradi iliyolengwa inakamilika. “Kama fedha zimeletwa kujenga zahanati simamia zahanati ijengwe na ni lazima zahanati hiyo ionekane,” alisema.
Alisema bajeti ya mwaka huu imeongezeka kutoka sh. trilioni 21 hadi trilioni 29 lengo kuu likiwa ni kuleta maendeleo kwa wananchi. “Ndiyo maana tumepandisha bajeti ya maendeleo kutoka asilimia 27 hadi asilimia 40. Ole wake atakayepokea fedha hizi halafu zisifanye kazi yake, ukiipoteza wewe utafute njia ya kwenda,” alisema huku akishangiliwa.
Akifafanua zaidi, Waziri Mkuu alisema vita inayoendeshwa imelenga kuifanya Tanzania ibadilike na itoke kwenye uchumi wa chini na kuingia uchumi wa kati. “Swali la msingi ni je tunafikaje hapo? Jibu ni kupitia uzalishaji wa bidhaa viwandani,” alisema.
“Nyote ni mashahidi wa jinsi ambavyo shilingi yetu imekuwa ikishuka thamani kulinganisha na dola ya Marekani. Tulitoka sh. 1,600/-, tukapanda hadi sh. 1,900/- na sasa tumefikia sh. 2,180/-. Hii ni kwa sababu tunaagiza zaidi bidhaa kutoka nje ya nchi badala ya kuzalisha, hatuwezi kuendelea hivi na ndiyo maana tumeamua kuwa nchi ya viwanda. Leteni mitaji nyumbani muwekeze,” alisisitiza.
Akijibu swali kuhusu Serikali kutafuta njia ya kutoa mikopo kwa Watanzania waishio nje ya nchi, Waziri Mkuu alisema mkopo ni mkataba kati ya taasisi ya kifedha na mkopaji kwa hiyo Serikali haiwezi kubeba dhamana hiyo. “Benki wanataka ijue taarifa zako mkopaji, wanataka wajua dhamana zako ni zipi, wajiridhishe na shughuli unazofanya. Je panakopesheka hapo?,” alihoji.
Hata hivyo, aliwaeleza kwamba wakitaka kuwekeza nyumbani wanaweza kupata mikopo kutoka benki ya maendeleo ya kilimo (TADB), Benki ya Rasilmali (TIB Corporate na TIB Development). “Hizi benki ni za wakulima na wajasiriamali, na zina masharti yake, kwa hiyo ni lazima wakakague eneo lako au mahali unapofanyia biashara au wakague leseni yako na ukweli wa maombi uliyopelekea. Sasa ukiwa Zambia watawezaje kukukopesha? Kwa hiyo ukitaka fedha uwe nyumbani,” alisema.
Akijibu swali ni vipi Serikali itawasaidia wanadiaspora kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu wakiwa nje ya nchi, Waziri Mkuu alisema Serikali haijawahi kujaribu jambo hilo licha ya kuwa ilikwishapokea mapendekezo kadhaa kutoka nchi mbalimbali lakini kwa vile wameliuliza, yeye analibeba na kwenda kulifanyia kazi.
No comments:
Post a Comment