ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, May 15, 2016

MAMBO SITA NJIAPANDA KWA MAGUFULI

Rais John Magufuli anahaha kurejesha uadilifu na nidhamu ya utumishi serikalini kwa kuwaondoa waliotumia vibaya madaraka yao, lakini wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema kuna mambo ambayo yatampa wakati mgumu kuyashughulikia.
Dk Magufuli ambaye aliingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 1995, alikuwamo katika Serikali iliyoundwa na Rais mstaafu Benjamin Mkapa (1995-2005) na aliteuliwa katika Baraza la Mawaziri chini ya Rais mstaafu, Jakaya Kikwete (2005-2015).
Baada ya kuteuliwa na CCM kuwa mgombea urais na hatimaye kushinda, Dk Magufuli ameanzisha kile anachoita kutumbua majipu, yaani kufumua uozo uliotengenezwa kwa kiasi kikubwa na awamu zilizopita kwa kuwatimua wakurugenzi na watendaji wa idara mbalimbali ambao sasa ni zaidi ya 160.
Katika hatua hiyo, wachambuzi wanasema Dk Magufuli atakuwa njiapanda katika mambo mbalimbali ambayo yalitokea katika wizara alizokuwa akiziongoza.
Hata hivyo, wachambuzi wa masuala mbalimbali waliozungumza na gazeti hili, walisema huenda Rais Magufuli akiwa waziri alikuwa akitekeleza wajibu na maagizo ya marais wa wakati huo.
Walisema kama hakuwa anatekeleza maagizo hayo, ataweza kushughulikia baadhi ya kasoro zilizojitokeza, lakini kama mambo yaliyotokea katika wizara hizo yalikuwa na baraka zake, atakuwa njiapanda kushughulikia.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili wachambuzi hao walisema Rais yeyote duniani ni lazima atumie busara ya hali ya juu kushughulikia kashfa zinazowahusisha vigogo wa Serikali, waliopo nje au watu maarufu ili kuepusha mpasuko serikalini au katika chama chake.
Wizara alizoongoza
Pamoja na kutaka kusimamia ukweli, Rais Magufuli inadaiwa atakuwa njiapanda kuwachukulia hatua maofisa wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi waliotia hasara nchi walipokamata meli ya uvuvi ya China, wakaacha ikaoza bandarini, ikazama; Serikali ikashindwa kesi na ikatakiwa kulipa fidia ya Sh1.3 trilioni.
Katika Wizara ya Ujenzi pia atakuwa njiapanda kushughulikia suala la uuzwaji wa nyumba za Serikali kati ya mwaka 2000 na 2005. Baadhi ya nyumba zilizouzwa zilikuwa katika maeneo nyeti na ilidaiwa kuwa nyingine ziliuzwa kwa watu ambao hawakustahili.
Pia, atakuwa njiapanda kumwajibisha ofisa yeyote aliyehusika na ununuzi wa boti mbovu ya kusafirisha abiria kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo. Kivuko hicho kilichonunuliwa kwa Sh7.9 bilioni kinatembea polepole na hata Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alipokuwa anafanya ukaguzi mwaka jana, kivuko hicho kilikuwa hakijafanya kazi mwaka mzima.
“Kivuko kilikabidhiwa bila hati ya makabidhiano Novemba 17, 2014, baada ya ucheleweshwaji wa siku 16; Pia nilibaini kwamba mpaka wakati wa ukaguzi, Agosti 2015, hati ya makabidhiano ilikuwa haijatolewa na mzabuni,” ilieleza ripoti ya CAG.
Vilevile, kuna uwezekano Rais Magufuli akawa njiapanda kuhusu malipo yaliyofanywa na Wakala wa Barabara (Tanroads), kwa makandarasi waliomaliza kazi zao, licha ya kuwapo dosari zilizobainishwa na CAG.
Mathalani, CAG anasema, “Wakati wa ukaguzi nilibaini kwamba baadhi ya mikataba haikukamilika kwa muda uliopangwa kutokana na kuchelewa kwa ulipaji wa fedha. Pia, nilibaini kwamba ucheleweshwaji wa malipo ya kati ya mikataba 16 ulisababisha ulipaji wa riba kiasi cha Sh5,616,652,022 na Dola za Marekani 686,174.86,” anasisitiza CAG.

Mambo mengine
Katika kipindi chote cha utawala wa awamu ya nne, Dk Magufuli anajua nchi ilikuwa kama shamba la bibi lisilo na mtu wa kulinda mali za umma, kiasi kwamba mashirika ya Pride na Uda yaliyoanzishwa na Serikali yamebinafsishwa katika mazingira ya kutatanisha.
Ripoti ya CAG inasema shirika la Pride lililoanzishwa na Serikali mwaka 1993 kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wajasiriamali, liliondolewa kwenye daftari la msajili wa hazina na kupewa watu binafsi.
Hadi sasa Serikali haina mpango wa kulirejesha mikononi mwake shirika hilo lililoanzishwa kwa msaada wa Shirika la Misaada la Norway (Norad).
Pili, ni utata unaolikabili Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda) lililokuwa linamilikiwa na Serikali Kuu (asilimia 51) kwa ushirikiano na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam (asilimia 49), lakini katika hali ya kushangaza inaonekana kampuni hiyo imeuziwa asilimia 51, jambo ambalo bado Watanzania wanasikilizia hatua za Rais Magufuli.
Mambo mengine yanaelezwa kuwa magumu ni ufisadi katika kashfa zilizoitikisa nchi, ambazo maazimio ya Bunge hayakutekelezwa yote likiwamo suala la Richmond na Dowans.
Pengine mtego mpya kwa Rais ni mkataba iliopewa kampuni ya Lugumi Enterprises wa kufunga mashine za kutambua na kuhifadhi alama za vidole katika vituo vya polisi 108, na kiongozi huyo wa nchi bado hajalizungumzia.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imechunguza na kubaini kwamba kampuni hiyo imefunga vifaa katika vituo 14 tu na vingi kati ya hivyo havifanyi kazi, huku ikiwa imelipwa Sh34 bilioni kati ya Sh37 bilioni.
Maoni ya wachambuzi
Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe alisema, “Unajua uchunguzi wa CAG ulifanywa wakati Rais akiwa waziri na inamtaja moja kwa moja. Sasa kama atachukua hatua au hatochukua hilo tusubiri tuone.”
Zitto alisema kati ya mambo ambayo Rais ameyafanyia kazi yaliyotajwa katika ripoti hiyo ni sakata la Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) tu, ambayo ilishindwa kusimamia mkataba wa utekelezaji wa mfumo wa usimamizi wa mawasiliano ya simu (TTMS) na kusababisha nchi kupoteza mapato ya takriban Sh400 bilioni kwa mwaka.
Kutokana na suala hilo, Aprili 27 mwaka huu, Dk Magufuli alivunja Bodi ya TCRA na kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dk Ally Simba.
“Ukirejea katika ile boti. Rais akiwa waziri yeye mwenyewe ndiye aliyeinunua na kuizindua na inaonekana wazi kuwa kuna Sh9 bilioni zilipotea chini ya utawala wake. Tunapaswa kuhoji MV Dar es Salaam iko wapi?” alihoji Zitto.
Zitto alisema mwaka 2011, CAG alitoa ripoti iliyoonyesha kuwa iliyokuwa wizara ya Rais Magufuli ilitumia Sh242, bila kuwapo maelezo na baada ya kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuunda timu ya uchunguzi ilibaini Sh87 bilioni zilitolewa hazina bila kuwa na uthibitisho katika matumizi, huku akisisitiza kuwa sasa ni wakati wa Rais kuonyesha kuwa anajua masuala hayo na kuchukua hatua stahiki.
Mchambuzi wa masuala ya siasa na utawala, Bubelwa Kaiza alisema Rais ndiyo anaongoza Serikali na kusaidiwa na mawaziri hivyo, jambo linalofanywa na waziri linakuwa na baraka ya Rais.
“Ukienda kinyume na Rais kuna mawili, ujiuzulu au uvumilie maelezo yake. Wizara ya ujenzi wakati ule iliyokuwa inatekeleza mambo mbalimbali ya nchi ilikuwa chini ya Kikwete na pengine (Magufuli) alilazimika kufanya aliyoyafanya kwa sababu ya maelekezo tu ya Rais.”
Alisema Rais ndiye anayetoa mwongozo kwa watendaji wake jinsi ya kuendesha mambo mbalimbali serikalini, huku akimtolea mfano mawaziri walioteuliwa na Rais Magufuli kwamba wanafanya kazi kwa kiwango cha juu kutokana na kasi ya rais huyo.
“Kuna wakati Rais Magufuli akiwa waziri alipiga marufuku malori yanayozidisha uzito kupita katika barabara zetu. Nadhani unakumbuka jinsi Mizengo (Pinda-Waziri Mkuu mstaafu) alivyoingilia na kupinga agizo hilo, huku rais akikaa kimya tu,” alisema.
Alisema kama Jakaya Kikwete alishindwa kumchukulia hatua Rais Magufuli kwa mambo ambayo yalitokea katika wizara yake, maana yake ni kwamba yeye ndiye aliyetoa baraka zote.
Akizungumzia kashfa mbalimbali zinazowataja vigogo wa serikalini kuhusika alisema, “Rais Magufuli wakati akiwa waziri alikuwa akiyajua masuala hayo, hivyo anaweza kuchukua hatua zinazostahili kwa maslahi ya Taifa. Hata hili la kampuni ya Lugumi, uchunguzi utafanyika na ukweli utabainika.”
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Hamad Salim alisema, “Waziri anaweza kutekeleza jambo kwa amri ya Rais na hawezi kupinga, kazi yake ni kushauri tu. Kwa msingi huo hatuwezi kujua yaliyotajwa na CAG yalitokana na maamuzi ya nani. Rais Magufuli wakati huo akiwa waziri au rais wa wakati huo.”
“Kama Rais Magufuli ataitumbua wizara ya ujenzi tutajua wazi kuwa yalikuwa maamuzi yake,” alisema Hamad.

No comments: